Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uigaji hauzuiliki katika ubunifu hasa wa kazi za fasihi

December 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ENOCK NYARIKI

KATIKA ubunifu wa kazi za fasihi – novela, riwaya, tamthilia au hadithi fupi – mwandishi hujikuta amemuiga mwandishi au waandishi wa kazi fulani.

Jambo hilo hutokea hivyo kusudi au hata bila kukusudiwa. Waama, haitakuwa sahihi kusema kuwa yupo mwandishi mmoja ambaye hakuathiriwa na kazi za mtunzi au watunzi wengine.

Vivyo hivyo, hayupo mwandishi aliyefanikiwa katika uandishi wake bila kuzisoma kazi za wengine. Uandishi mzuri hutokana na usomaji mpana wa kazi za watunzi wengine. Usomaji huo haukamiliki pasi na kuathiriwa na kazi hizo.

Waandishi huathiriwa na wengine kwa njia mbalimbali. Huathiriwa katika matumizi ya msamiati.

Baadhi ya maneno huenda si mapya lakini watangulizi huwa wameyatumia kwa namna fulani waliyoipendelea wenyewe.

Mfano mzuri ni wa matumizi ya neno ‘shangazi lake’ au ‘shangazi langu’ katika baadhi ya kazi za Shaaban Robert – mfano mzuri ukiwa ule wa ‘Siku ya Watenzi Wote’. Kimsingi, kivumishi kimlikishi na cha A-unganifu cha neno hilo shangazi kingetarajiwa kuwa ‘yangu’ na ‘ya’ katika mfuatano huo. Hata hivyo, Shaaban Robert, kwa sababu yake mwenyewe, ameamua kutumia ‘shangazi langu’ na ‘shangazi la’. Profesa Ken Walibora, katika riwaya yake ya awali ya ‘Siku Njema’ anaelekea kutekwa sana na matumizi ya ‘shangazi langu’ na ‘shangazi la’ jinsi yanavyojitokeza katika kazi ya Shaaban Robert.

Ijapokuwa mtu hawezi kudai umiliki wa msamiati fulani wa Kiswahili, namna ya kuutumia msamiati huo inaweza kuonyesha uigaji wa aina fulani.

Kwa mfano Profesa Said A. Mohamed ana mazoea ya kutumia neno ‘danda’ lenye maana ya kuenea au kukolea kwa kitu. Neno hili linajitokeza katika baadhi ya kazi za Shaaban Robert.

Uigaji mwingine hujidhihirisha kwa njia ya mtindo. Waandishi wanaweza kuigana kwa namna wanavyounda sentensi zao.

Profesa Said A. Mohamed anaelekea kuazima vipengele fulani vya kimtindo kutoka kwa Mohamed S. Abdulla.

Waandishi wote wawili wanayo namna fulani ya kuanza na kumaliza sentensi zao ambayo inaelekea kulingana kwa namna fulani.

Wote hutunga sentensi fupi zinazoanguka kwa makurubundi ya risasi. Kazi za Ben Mtobwa vilevile zinaelekea kuathiriwa na zile za marehemu Mohamed S. Abdulla kimtindo.

Uigaji mwingine huwa ni wa wahusika na uumbaji wa wahusika. Ingawa hapana mwandishi yeyote anayeweza kudai umiliki au ukiritimba wa majina hususan majina ya Waswahili, jinsi ya kuwaumba wahusika inaweza kuwafanya waandishi wawili kushabihiana kwa namna fulani.

Katika kazi ya Shaaban Robert ya ‘Wasifu wa Siti Binti Saad’ mwandishi anaelekea kumpa mhusika Siti Binti Saad sifa zenye upekee – sifa za kimalaika.

Wapo waandishi wengine ambao japokuwa wahusika wao ni tofauti sana kimajina, wamepewa sifa hiyo ya kimalaika inavyojitokeza katika diwani ya Sheikh Shaaban Bin Robert.

Mfano mzuri ni ule wa mhusika Zainabu Makame wa riwaya ya ‘Siku Njema’ ambaye sifa alizopewa zinashabihiana kwa hali zote na mhusika Siti Binti Saad.

Uigaji mwingine huwa wa kifalsafa. Kwa kutumia neno falsafa hapa ninamaanisha msimamo wa waandishi mbalimbali katika kazi zao. Je, ni mambo gani ambayo waandishi hao wanayaamini?

Ni upi msimamo wao kuhusu ulimwengu? Inawezekana Profesa Kezilahabi ameathiriwa kwa njia moja au nyingine na kazi za mwanafalsafa Kierkegaard, mzaliwa wa Copenhagen ambaye ndiye mwaasisi wa nadharia ya udhanaishi.

Uigaji hauepukiki katika ubunifu hususan ule unaohusiana na kazi za fasihi. Upo uigaji chanya ambao unakubalika.

Huu hutokea pale ambapo mwandishi ameathiriwa bila kukusudia. Hata hivyo, upo pia uigaji wa kikasuku ambapo mwandishi amebebwa mno na mwandishi mwingine hivi kwamba mwandishi wa pili hadhihiriki kabisa katika kazi yake.

Sharti pawepo na kipengele fulani kinachompa mwandishi upekee hata pale ambapo anaelekea kuathiriwa na kazi ya mwingine au za wengine.