• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umuhimu wa tafiti kuhusu umilisi wa lugha katika ufundishaji wa Kiswahili

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umuhimu wa tafiti kuhusu umilisi wa lugha katika ufundishaji wa Kiswahili

Na MARY WANGARI

KWA mujibu wa Mcmanara (2000), mitihani ya umilisi wa mawasiliano inafaa kupima uwezo wa mzungumzaji katika kiwango cha kanuni za lugha na vilevile katika kiwango cha uamilifu wa lugha.

Umilisi wa kiisimu haumaanishi kuwa mzungumzaji ana umilisi wa kutosha katika mawasiliano, hata hivyo. Ni dhahiri kuwa mitihani mingi ya umilisi wa mawasiliano hujikita katika kupima umilisi wa kiisimu ambao huchukuliwa kama msingi wa kufahamu lugha yoyote ile.

Umilisi wa kiisimu ndio nguzo ya umilisi wa mawasiliano ndiposa ni muhimu kwa tafiti mwafaka kufanyiuka ili kuweza kubaini makosa ya kiisimu yanayojitokeza na jinsi makosa hayo yanavyoathiri umilisi wa kiisimu katika lugha ya Kiswahili.

Isitoshe, tafiti hizi kuhusu umilisi wa lugha katika Kiswahili zitawezesha kupendekeza njia ambazo walimu na wafundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa jumla, wanaweza kutumia kuimarisha umilisi wa kiisimu wa lugha ya Kiswahili katika taasisi za elimu nchini.

Kwa mujibu wa msomi Nunnan (2003), mtu ambaye anasitasita katika mazungumzo huonyesha umilisi wa kiwango cha chini katika lugha husika.

Aidha, kuonyesha matamshi mabaya ya maneno, kuchanganya na kuhamisha misimbo, kutofuata ruwaza maalum katika mazungumzo, na kiimbo kibaya. Nao ung’amuaji wa maana ya maneno ni baadhi ya vigezo ambavyo huonyesha badiliko la umilisi wa kiisimu katika lugha.

Mtaakamu huyo anafafanua kuwa mtu aliye na umilisi wa juu katika lugha hataonyesha upungufu huo lakini anaweza kuonyesha upungufu huo ikiwa umilisi wake ni wa kiwango cha chini.

Hata hivyo, mwanafunzi au mtu huyo anapozidi kusoma na kuimarika umilisi wake unaimarika na kisha anafuata sheria kamili za lugha.

Hivyo basi, pana haja ya kuwepo tafiti zitakazowezesha kuchanganua vigezo ambavyo huonyesha mabadiliko ya kiisimu katika lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi shuleni.

Hii hasa ni kwa kuzingatia kuwepo kwa lunga nyinginezo kama vile lugha ya kwanza, sheng’ na nyinginezo, zinazoathiri umilisi wa kiisimu katika Kiswahili hali inayojitokeza katika mtagusano wa lugha hizo na lugha ya Kiswahili.

[email protected]

Marejeo

Nunan, D. (2003). Practical English Language Teaching. Singapore: McGraw-Hill Education (Asia)

Mcdonough. S. (2002). Applied Linguistics in Language Education. Bodmin: MPG Books Ltd

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya umilisi wa lugha ya...

Wanavikapu wa ‘majuu’ wathibitisha kutambisha...