UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vibainishi vya kimsingi katika Nadharia ya Utambulisho
Na MARY WANGARI
KATIKA kufafanua nadharia ya utambulisho, lugha ya mzungumzaji ni kibainishi muhimu sana.
Vibainishi vinginevyo vinavyotumika katika kuukamilisha utambulisho wa mtu ni pamoja na:
i. Uchumi
ii. Siasa
iii. Utamaduni
iv. Historia ya jamii
v. Dini
vi. Mavazi
vii. Vyakula
Kwa mintarafu hii, ni dhahiri kwamba ni vigumu kubainisha utambulisho wa mzungumzaji kwa kutumia lugha peke yake bila uchanganuzi wake kwa kuzingatia jamiilugha anayotoka ambako masuala ya utamaduni, mila na desturi ni sehemu muhimu na kiungo cha umoja wa jamiilugha hiyo.
Ni muhimu kuelewa kwamba lugha ya mzungumzaji na utambulisho wake ni mambo mawili ambayo hayawezi katu kutenganishwa. Ni kama pande mbili za sarafu moja.
Uhusiano wa lugha na utambulisho unaelezwa vizuri kwa kutumia nadharia za Giles (1982).
Dhana ya Mawasiliano/ Ishara Matamshi
Wataalamu anuwai wamejitokeza na fasili tofauti tofauti kuhusu dhana ya mawasilano.
Fluharty na Ross (1966:2), wanafafanua dhana ya mawasiliano kama uwasilishaji wa ujumbe kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine kwa kutumia ishara au nyenzo fulani.
Isitoshe, wanadai kwamba mtuma ujumbe huufumbata ujumbe wake katika nyenzo fulani na kuutuma kwa mpokeaji.
Naye mpokeaji huzifumbata nyenzo hizi ili kuupata ujumbe uliotumwa. Naye Stumai (1990), anaiona dhana ya mawasiliano kuwa ni pana na maana yake hutegemea mazingira.
Kimsingi, anaeleza mawasiliano kama usafirishaji wa ujumbe, watu, mizigo, na kadhalika kutoka upande mmoja wa nchi hadi mwingine.
Kwa upande wake Tuli (1985:7), anaeleza kuwa mawasiliano ni njia zozote zinazowawezesha wanadamu kuathiriana. Aidha, katika hali ya ufinyu wake, anaendelea kueleza mawasiliano kama usafirishaji wa habari au ujumbe kama vile mawazo, maarifa, ujuzi na kadhalika miongoni mwa watu.
Nao Bateman na Zeithaml (1993:5), wanafafanua kwamba mawasiliano ni upelekaji wa habari na maana kutoka kwa chama kimoja hadi kingine kwa kutumia ishara za kushirikiana.
Aghalabu kuna mtuma-ujumbe ambaye huuanzisha mfumo huu kwa kupitisha ujumbe kwa mpokeaji; mtu ambaye ujumbe unamlenga.
Marejeo
Kei K.J. (2002). “Nafasi ya Kiswahili Katika Ujenzi wa jamii Mpya ya Afrika Mashariki.” Nordic Journal of African Studies, ( pp 185-197). West Port, CT: Praeger.
Mathooko, M. (2007). Isimu jamii; Misingi na Nadharia. Nairobi: Njogu Books.
Njogu, K & Chimera, R. (1999). Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.