• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vizingiti vinavyowakabili wanafunzi katika kupata maarifa ya elimu shuleni

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vizingiti vinavyowakabili wanafunzi katika kupata maarifa ya elimu shuleni

Na MARY WANGARI

MWANAISIMU Mekacha (2000), anatoa hoja kwamba lugha ya kufundishia inapokuwa haieleweki vizuri kwa walimu na wanafunzi, huathiri ufanisi katika kutoa, kubuni na kuendeleza maarifa.

Nao Msanjila na wenzake wanadai kwamba, lugha ya kufundishia inapokuwa tofauti na lugha inayofahamika katika jamii nzima, walimu wanaoitumia lugha hiyo kufundishia hushindwa kujifungamanisha na wanajamii wenzao.

Isitoshe, wanaisimu hao pia wanadai kwamba, wanafunzi pia hushindwa kutumia lugha hiyo kung’ amua, kujieleza na kukuza fikra pevu zilizo msingi wa ubunifu na ugunduzi.

Machapisho ya wataalamu mbalimbali yamesomwa na kunukuliwa hasa yale yanayoendana na mada husika.

Maelezo hayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuelewa ni kwa jinsi gani lugha ya kufundishia inatakiwa iwe inafahamika vizuri kwa walimu na wanafunzi kuepuka athari za kukosekana kwa maarifa.

Ingawa wataalamu wanatofautiana katika kueleza athari za lugha, tofauti zao ni finyu zikilinganishwa na mchango waliotoa kwa utafiti wao kuhusu uhusiano wa lugha ya kufundishia na upatikanaji wa maarifa.

Kuna vizingiti kadha vinavyochangia wanafunzi kukosa maarifa ya elimu ya sekondari kwa namna inavyofaa.

Kwanza kabisa, ni kuhusu lugha inayomika kufundishia katika shule za sekondari kwa mfano nchini Tanzania ambapo idadi kubwa ya walimu na wanafunzi hawana ujuzi wa lugha husika.

Tafiti za wanaisimu mbalimbali zimeunga mkono hoja hii kwa njia ifuatayo:

Macdonald (1990) aligundua kwamba, ujuzi mdogo wa walimu katika lugha ya kufundishia katika nchi ya Botswana unawakosesha wanafunzi kupata maarifa ya kujua kusoma na kuandika katika lugha ambayo haikuzoeleka kwa wanafunzi na wao wenyewe wana ujuzi mdogo wa kuitumia kufundishia.

Utafiti uliofanyiwa nchini Botswana na Prophet na Dow (1994) ulibaini kuwa wanafunzi wa kidato cha kwanza waliofundishwa kwa lugha ya Kitswana walikuwa na uelewa wa kiwango cha juu zaidi wa seti ya dhana za kisayansi ikilinganishwa na wanafunzi waliofundishwa kwa Kiingereza.

Naye Wilmot, (2003) aligundua kuwa, lugha ya kuwafundishia wanafunzi nchini Afrika Kusini inapobadilishwa kutoka Kiingereza kwenda lugha-mame wanafunzi hufahamu mambo mengi zaidi na kujifunza vizuri zaidi wanapofundishwa kwa lugha waliyoizoea.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Bryman A. (2008). Social Research Methods. London: Oxford University Press.

Cummins, J. (2008). Teaching for transfer. Challenging the two solitudes assumption in Bilingual education.In J. Cummins & N.H Homberger (Eds), Encyclopedia of Language and Education, 2nd Edition,Volume 5. New York: Springer Science + Business Media LLC.

Enon C.J. (1995). Educational Research, Statistics and Measurement. Kampala: Makerere University.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Changamoto za kutumia lugha ya...

Unilever yajikakamua kupenya kwa soko la dawa ya meno

adminleo