ULIMBWENDE: Cha kutumia ili kuondoa mikunjo ya ngozi
Na MARGARET MAINA
WANAWAKE wengi wanakabiliwa na tatizo la mikunjo katika ngozi.
Tofauti na mikunjo ya uzee, mikunjo hii hutokana na kuchoka kwa ngozi kunakosababishwa na mambo na shughuli mbalimbali.
Katika kupambana na tatizo hilo, unaweza kutumia vitu vya asili. Unaweza kutumia viungo vinavyopatikana jikoni kwako kukabiliana na kero ya mikunjo katika ngozi. Baadhi ya viungo hivyo ni pamoja na karoti, papai, mshubiri, parachichi, na maji.
KAROTI
Tumia juisi ya karoti kwa kupaka katika ngozi yako, hasa katika maeneo yaliyoathirika.
Karoti ina virutubisho muhimu kwa ngozi yako. Pia ina uwezo mkubwa wa kuondoa sumu ndani ya ngozi.
Pia inaweza kuondoa tatizo la mikunjo ya ngozi hasa sehemu za pembeni ya macho na shingo.
Namna ya kufanya
- chukua karoti, saga kwenye blenda kisha kamua ili kupata juisi yake
- tumia pamba kupaka katika maeneo yaliyoathirika, fanya hivyo mara kwa mara, itakusaidia kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo hilo
MAZIWA
Maziwa yana virutubisho vinavyosaidia katika kunawiri kwa ngozi.
Pia yana ‘Alfa-Hydroxide Acid’ ambazo zina uwezo mkubwa kuondoa seli zilizokufa mwilini.Yote haya husaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tatizo la mikunjo katika ngozi.
Unachotakiwa kufanya
- chukua maziwa kiasi na chovya pamba ndani yake, kisha paka maeneo yaliyoathirika
MSHUBIRI
- chukua jani la Aloe vera na kisha likate ili kupata utomvu wake
- chukua jeli hiyo na kisha paka sehemu iliyoathirika; tapunguza ama kuondoa kabisa tatizo hilo
PARACHICHI
Maski ya parachichi husaidia kuifanya ngozi iwe na mng’ao. Pia huchangia kwa kiasi kikubwa kuifanya ngozi iwe laini na nyororo.
Unachotakiwa kufanya
- chukua parachichi liloiva vizuri kisha saga hadi lilainike
- paka sehemu iliyoathirika na acha kwa muda wa dakika 10 kisha osha sehemu hiyo na uikaushe
PAPAI
Maski ya papai pia husaidia kuondoa tatizo hili.
Unachotakiwa kufanya
- chukua kipande cha papai kilichoiva na kuchanganya na kijiko kimoja cha unga wa ngano
- paka kweye sehemu iliyoathirika na kaa hivyo kwa dakika kadhaa
Mbali na kupaka pia unaweza ukatumia kula kwani lina Vitamin E kwa wingi, ambayo ni muhimu katika ukuaji wa ngozi.
MAJI
Kunywa maji mengi kwani husaidia kuifanya ngozi yako iwe na unyevu muda wote.