Makala

ULIMBWENDE: Epuka matumizi holela ya vipodozi

October 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

USIPOVITUMIA vipodozi jinsi ipasavyo, unaweza ukapata madhara mengi; tena makubwa.

Machache kati ya hayo ni kansa ya ngozi, matatizo ya maini, ubongo, mapafu na mfumo wa damu; ngozi kuungua, ngozi kuwasha sana, upofu, upotevu wa fahamu wa mara kwa mara, uziwi, kuumwa kichwa, kizunguzungu, fangasi na magonjwa mengine kwenye ngozi, aleji ya ngozi, kuchubuka kwa ngozi, mabaka mwilini, chunusi kubwa kubwa, ngozi kuwa nyembemba sana na laini kiasi na mengineyo mengi.

Vipodozi vitakavyokuharibu

Haviendani na ngozi au mwili wako. Kwa mfano, mtu mwenye uso au ngozi ya mafuta mafuta akitumia kipodozi kilichotengenezwa mahususi kwa ajili ya ngozi kavu, basi kinaweza kumletea chunusi nyingi na matatizo mengine. Usitumie kipodozi chochote ambacho sio kwa ajili ya aina ya ngozi au mwili wako.

Vina kemikali ambazo ni sumu na hudhuru mwili wa binadamu na viungo vyake. Mfano ni Mercury (Zebaki), Hydroquinone na Betamethason.

Vimeharibika au muda wake wa matumizi umeisha. Hivi vinakuwa havikupi garantii ya ubora, ufanisi wala usalama. Hivi navyo ni hatari kwa afya yako na unafaa kuviepuka.

Vipodozi ambavyo vimepigwa marufuku, havijaidhinishwa na kusajiliwa na KEBS. Hivi navyo, havina garantii ya ubora, ufanisi wala usalama. Usivitumie.

Matumizi yake hayaendani na mahitaji ya mtumiaji. Ni vyema kuvielewa vizuri vipodozi au kupata ushauri wa ni aina ipi ya vipodozi vya kutumia kulingana na matatizo au mahitaji yako.

Usitumie vipodozi ambavyo haviendani na tatizo au hitaji lako, maana utakosa matokeo unayoyahitaji, utapoteza pesa, muda na vinaweza kukuletea matatizo mengine ambayo haukuwa nayo.

Unashauriwa usitumie kipodozi chochote ambacho sio salama hata kama kinakuletea matokeo mazuri kwa haraka. Matatizo mengi ya vipodozi visivyo salama huwa ni makubwa na hayatibiki kirahisi, na mengine yanaua au kukusababishia ulemavu wa kudumu.

Yanaweza kuja haraka au polepole, kwa hiyo hata kama huyaoini kwa sasa basi baadaye yatafika. Furahia ujana, furahia uzee. Vipodozi vibaya vinaweza vikakuzeesha haraka na kukupa matatizo mengi sana baadaye na kukuongeza kadhia za uzeeni.

Onana na wataalamu wa urembo na vipodozi, pata ushauri. Kwa maelezo zaidi na ushauri juu ya vipodozi na kuufanya mwili wako uwe ni wa kupondeza, wasiliana na wataalamu.