UMBEA: Dalili za msongo wa mawazo na jinsi ya kukabiliana nazo
Na SIZARINA HAMISI
MAISHA ni safari ndefu, ambayo pia wakati mwingine hugubikwa na changamoto nyingi.
Wakati mwingine inakuwa rahisi kutatua changamoto hizi, lakini wakati mwingine unaweza kujipata ukiwa umekwama, unajisikia hali ambayo sio ya kawaida.
Msongo wa mawazo ni hali ya maumivu au mfadhaiko wa kihisia au kisaikolojia unaotokana na hali, tukio au jambo ambalo ni gumu sana au lenye changamoto kubwa.
Tunasema una msongo wa mawazo pale ambapo unajisikia au unaona kama vile kila kitu kimekuwa kigumu.
Tunasema maji yamefika shingoni, unajikuta umekata tamaa na unaona dunia imekuinamia.
Ni pale unapohisi umezidiwa na hujui kama utaweza kupambana na changamoto na msukumo uliopo mbele yake.
Wapo watu waliopoteza maisha kwa kuzidiwa ama kushindwa kupata suluhu ya msongo wa mawazo.
Wapo waliotumia pombe, bangi na hata dawa za kulevya kujaribu kutibu hali hii.
Ili kuweza kupata suluhu ya shida hii inapokupata, ni muhimu pia kutambua dalili zake zinakuwaje.
Mambo yanayoweza kusababisha msongo wa mawazo ni kama matatizo ya kisaikolojia na afya ya akili, matatizo ya kiuchumi, magonjwa, kazi nyingi au matatizo kazini, kufiwa, mambo usiyokuwa na uhakika nayo kama vile kusubiri majibu ya mtihani au matatizo ya kimahusiano.
Ugonjwa haupo, lakini unaumwa
Dalili hizi zinaweza kuanza kwa kuhisi ni mgonjwa, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa na kushindwa kutuliza akili.
Mara nyingi hata ukienda hospitali na ufanyiwe vipimo vyote hutapatikana na ugonjwa, lakini utakuwa unajihisi unaumwa.
Iwapo upo kwenye ndoa, unaweza ukakosa kabisa hamu na mwenzako na hata usitamani suala zima la burudani.
Wapo wale wanaokuwa na hasira mfululizo bila sababu yoyote ya msingi na wengine utawapata wanang’ata kucha zao mfululizo hata kama hawana mazoea ya kufanya hivyo.
Hali kadhalika kama unakuwa unagubikwa na huzuni kila wakati, unajihisi umechoka bila hata kufanya kazi yoyote, hamu yako ya kula chakula imeongezeka kwa kiasi kikubwa ama kutoweka kabisa na halafu unajitenga kabisa na jamii, ni dhahiri kwamba unanyemelewa na msongo wa mawazo.
Pamoja na yote, unapoona unatumia pombe ama aina nyingine za vileo ili “kutuliza” mawazo yako na unataka kuwa kwenye hali ya kukosa ufahamu wakati wote, hizo pia ni dalili za msongo wa mawazo.
Hizi ni baadhi ya dalili ambazo huenda zinaweza kuashiria kwamba hali sio shwari.
Suluhisho pale unapojisikia hali hii, ni kufanya mazoezi. Mazoezi ni njia iliyothibitishwa kuwa na matokeo chanya katika kumfanya mtu ajisikie vizuri kihisia na kisaikolojia.
Kwa watu wengi, mazoezi ni njia tosha kabisa ya kuondoa msongo wa mawazo.
Ujipe muda wa kupumzika, kutafakari mambo yako na kufanya mambo yanayokupa raha kama kuogelea, kusikiliza muziki, kuangalia sinema, kusoma kitabu au jambo lolote lenye manufaa ambalo linakufurahisha.
Katika hili, usiwe mtu wa “ndio, ndio”. Usiwe unasema ndio kwa kila jambo.
Kama huwezi kufanya kitu fulani vizuri, au kama sio jukumu lako, tafuta njia nzuri ya kusema hapana na kutofanya jambo hilo.
Usinyamaze, ongea au sema yanayokusibu.
Usinyamaze na matatizo yako mwenyewe, ongea na mtu unayemwamini.
Elezea hofu na mawazo yako. Kama huwezi kuongea andika unavyojisikia kila siku.
Iwapo umejaribu mazoezi, kuzungumza na yule unayemuamini na bado unaona hakuna afadhali, ni muhimu kuonana na wataalamu wa saikolojia ambao watakusaidia kutatua tatizo hili kulingana na chanzo.
Pia wataalamu hawa watakutibu matatizo mengine ambayo mtu anaweza kuwa nayo kama hofu iliyopitiliza, sonona na matatizo mengine ya kisaikolojia.
Siku ya leo ikiisha haitarudi tena. Ishi kwa amani, furaha na bila kinyongo.