UMBEA: Hakuna ushindi wa taji la ndoa uvumilie kushushwa utu wako
Na SIZARINA HAMISI
HAKUNA aliyewahi kupewa kombe la ushindi wa ndoa.
HIVYO huna haja ya kutafuta sifa, kuvumilia yasiyovumilika, kudhalilishwa ama kushushwa utu wako ili uendelee kuwa kwenye ndoa.
Haya maisha sio marefu sana, kwamba tunaishi kwa muda hapa duniani na baada ya hapo kila mmoja hufikwa na mauti. Ninaamini katika muda huu ni muhimu kuishi kwa furaha, amani na raha pia.
Kwani unapoamua kuvumilia kutendewa yasiyofaa ni kwamba muda unakwenda na siku zinasogea na muda wa kuwepo hapa duniani pia unapungua.
Ninaandika haya moyo wangu ukiwa umeinama kwa huzuni, kwani nimeshuhudia jamaa yangu akitaabika na kuteseka sababu ya kuvumilia mambo ambayo hayafai kuvumilika.
Na sababu alikuwa akificha, akitudanganya wakati mwingine, huku tukiona wazi kwamba mambo sio shwari, hivi sasa amelazwa hospitalini akiwa mahututi, anapumua kwa msaada wa mashine.
Ni wanawake wachache sana huweza kubaini mara moja wanapoanza kutendewa vitendo vya ukatili kwenye ndoa zao.
Hii ni kwa sababu vitendo hivi vya unyanyasaji vinahusisha kwa kiasi kikubwa kudhibiti fikra ya anayetendewa ukatili, ili asiweze kutambua mara moja kwamba yale anayotendewa sio haki.
Viashiria
Ili kuweza kubaini kwamba unaishi katika ndoa ya unyanyasaji, huwa kunakuwa na dalili ama viashiria ambavyo ukivitilia maanani unaweza kutambua kinachoendelea.
Kuhusu jamaa yangu, kulikuwa na dalili ambazo sisi tuliokuwa nje tulikuwa tunaziona, lakini hata tulipomweleza kwamba haya tunayoona sio ya kawaida, hakutaka kukubaliana nasi na akawahi kunieleza kwamba niache kuingilia maisha yake.
Jambo la kwanza ambalo lilianza kunitia hofu kwake ni jinsi ambavyo alikuwa akimuogopa mume wake.
Kwani kila alipokuwa akiingia ndani ya nyumba, alionekana bayana kukosa amani na wakati mwingine akaniharakisha niondoke sababu mumewe amerudi.
Nilipoonana naye baadaye, nikajaribu kumdadisi kwa nini anamuogopa mno mumewe, akanijibu kwa uhakika…“huwa hanipigi, kama unafikiria hivyo”.
Nikamwuliza iwapo hapigwi kwa nini anamuogopa. Ndipo akaniambia mumewe huwa hapendi atembelewe na ndugu ama rafiki zake, akidai… “wanamfundisha tabia zisizofaa”.
Halikadhalika anapotaka kwenda kuwaona wazazi ama ndugu zake wakati mwingine hukataliwa akiambiwa hakuna umuhimu wa kufanya hivyo, anaweza kuzungumza nao kwa simu na inatosha.
Jambo la kusikitisha ni kwamba kila mara nilipokutana naye alionekana bayana kukosa furaha na kawaida yangu huwa nadadisi.
Kuna wakati akanitaka nimpatie nauli ya kurudi nyumbani kwake, sababu hana pesa.
Nikataka kujua amefikaje hapo nilipokutana naye, akanieleza kwamba ametembea.
Nikashangaa sababu huyu jamaa yangu anaendesha biashara ambayo inamwingizia kipato kizuri.
Mume achukua pesa zote
Nikataka kujua iwapo biashara imeleta shida, akanijibu la hasha, isipokuwa mumewe amekuwa akichukua pesa zote za biashara bila kumuachia chochote.
Nikajaribu tena kwa mara nyingine kuzungumza naye ili aone kinachotokea katika maisha yake, hakuweza kutambua. Bali akaniambia nimuache aishi maisha yake.
Nikapotezana naye kwa muda mrefu kidogo na ndiposa hivi majuzi nikapigiwa simu usiku wa manane kwamba jamaa yangu yuko hospitali na hali yake ni mbaya.
Nikajikusanya na kwenda hospitali kumuona na hali niliyomkuta nayo imeniacha na huzuni mkubwa.
Pamoja na majeraha aliyokuwa nayo usoni na mwili mzima, uso wake ulizungumza mengi kwangu ingawa alikuwa amelala kitandani bila fahamu.
Iwapo nawe upo kwenye ndoa ambayo inahusisha yaliyomtokea jamaa yangu, tafadhali jitathmini, kwani maisha tunayoishi siyo ya milele. Huna budi kuishi kwa amani na furaha na sio kwa hofu na kunyanyaswa.