UMBEA: Nyumba ni kwa ajili yako na mumeo, hukuolewa na ukoo!
Na SIZARINA HAMISI
PURUKUSHANI na mshikemshike katika baadhi ya ndoa huchangiwa na kuchochewa zaidi na baadhi ya ndugu wa karibu.
Ndugu hawa hujumuisha wazazi, kaka na dada za wahusika kwenye ndoa. Na mara nyingi wanaochukua nafasi ya kwanza kuwa vivuruge wa ndoa za ndugu ni akina dada ambapo huamua kuleta valangati kwa mawifi zao, wale waliofunga ndoa ama kuishi na kaka zao.
Baadhi ya akina dada hawa wamekosa utu. Maneno yao huwa yanatawaliwa na cheche na ukali mithili ya ndimi za moto. Kwao hakuna jema wala zuri, bali kila siku ni kusaka na kutafuta yaliyo mabaya kutoka kwa wake za kaka zao. Huwa wamejaa kiburi na ujeuri kwa wake wa kaka zao.
Kabla hujamvamia na kuanza kumchambua wifi yako, jichunguze kwanza mwenyewe, ukoje? Ukikosea huwa unakubali kosa na kuomba msamaha au unafanya kiburi?
Kwa upande wenu akina dada mlioolewa na kukuta mume ana dada zake, ni vizuri kuwaelewa dada wa waume mnapoolewa.
Inawezekana tangu ulipokwenda kijijini kwa mumeo (ukweni) ulishaona baadhi ya tabia za wifi yako ambazo kwa namna moja ama nyingine zilikukwaza. Hivyo mumeo atakapokupa taarifa ya ujio wa wifi yako, usionyeshe kukasirika, kwa sababu kama ukionyesha umekasirika, anaweza akahisi jambo fulani baya kwako.
Pengine atahisi humpendi dada yake hivyo hata siku akikukosea na kumwambia, ataamini ni fitina au chuki zako binafsi.
Siku wifi yako anapokuja nyumbani, kuwa wa kwanza kumkumbusha mumeo kwenda kumpokea, weka maandalizi motomoto na onyesha furaha ya ujio wake.
Mkikutana kituoni mkumbatie na uonyeshe kuwa unajisikia furaha kumuona. Ukimfanyia hayo, hata kama alikuwa na lake moyoni, atajifikiria kwanza kabla hajaanza kukutendea yasiyofaa. Hata hivyo, kama ana ukorofi wa asili, hii haiwezi kuwa dawa, anaweza akatafuta visa vitakavyokuudhi baadaye.
Kitu muhimu kabisa kufanya baada ya kuona wifi yako amekukosea ni kuzungumza naye. Inawezekana anaweza kuanza kuwa na maneno ya hapa na pale au anaanza kuwa na wivu usioeleweka, pengine alimwambia mumeo kuwa una tabia mbaya au vyovyote katika kukuharibia ndoa yako.
Usionyeshe chuki, zungumza naye taratibu. Mweleze jinsi unavyompenda na kuuthamini uhusiano wenu. Ikiwa utatumia lugha nzuri naamini atakuelewa lakini kama siyo muelewa, ataendelea na chokochoko zitakazokukera.
Iwapo yote hapo juu hayakufua dafu, unapaswa kukaa chini na mumeo na kumweleza juu ya jambo hili. Kukaa kwako kimya na kumvumilia kutakuwa hakuna maana, kwa sababu ni rahisi ndoa yako kuvunjika.
Usimfiche chochote, hata kama aliwahi kukutolea maneno machafu kwa mumeo, usijali; zungumza taratibu bila jazba huku ukitumia hoja kuliko maneno matupu.
Nyumba ni kwa ajili yako na mumeo. Kuolewa hakumaanishi kwamba umeolewa na ukoo mzima na kila mmoja anaweza kukuchamba.
Huna budi utambue haki yako na kama mumeo ana mapenzi ya dhati kwako, atakupa kipaumbele na kufanya maamuzi sahihi kwa heshima na sababu ya kuilinda ndoa yenu.
Utambue kwamba wanaume si watu wa kukurupuka, mara zote kama utazungumza kistaarabu ukitumia hoja, ni wazi kuwa atakuelewa na kutafuta njia mbadala za kutatua tatizo.
Kumbuka ukitumia kauli chafu au kukaripia, utamfanya ahisi kuwa una chuki na ndugu yake na unataka kuwagombanisha. Usiruhusu fikra hizo akilini mwake.
Kumbuka kwamba mumeo anamfahamu vizuri zaidi dadake na yuko kwenye nafasi nzuri zaidi kuweza kuleta suluhu ya mgogoro.