• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
UMBEA: Penzi linapochuja, thamani  yako pia huwa imechuja

UMBEA: Penzi linapochuja, thamani yako pia huwa imechuja

Na SIZARINA HAMISI

KATIKA harakati zangu za kuzungumza na watu mbalimbali, niliguswa na dada mmoja hivi majuzi.

Nilikutana na dada huyu katika pilkapilka zangu za hapa na pale. Alinifuata faragha na kunitolea machungu yaliyo moyoni mwake. Na kubwa lililomtatiza ni jinsi ndoa yake inavyoelekea kuporomoka.

Akanieleza jinsi mapenzi yalivyonyauka na hatimaye kuisha kabisa kati yake na mumewe. Na alitaka kujua iwapo ndoa inaweza kuwepo bila mapenzi kati ya mume na mke.

Penzi likichuja ni rahisi sana kujua. Lakini pia wapo baadhi ambao hata penzi lichuje, wanakosa kuelewa ama kujua ndoa inaelekea kuporomoka. Jambo kubwa linalojitokeza mapenzi yanapoelekea kuisha ni mwenzako kukosa kabisa hamu nawe.

Kama alikuwa na kawaida ya kurudi nyumbani, ratiba yake itabadilika. Si ajabu akawa anarudi usiku kila wakati. Mara nyingi mwenzako anapoanza hivi, anakuwa ameanza kukosa hamu ya kukuona ama kuwa karibu nawe. Hivyo atachelewa kurudi ili kupunguza muda wa kuwa nawe.

Penzi linapochuja ni hatari kwani hata ukiwa na shida ya muhimu kwa mwenzi wako, anaweza akakataa kukusaidia. Hatakuwa na mvuto wa kimapenzi na wewe kama ilivyokuwa mwanzoni. Kwa maneno mengine, hatakukumbusha wala kutaka kushiriki nawe tendo la ndoa.

Hata ukiamua kumuuliza kinachoendelea, bado hatakuwa na msisimko ambao uliuzoea kwake. Inawezekana kabisa akakuambia hawezi kufanya hivyo kwa kuwa amechoka! Kwa wapenzi ama wanandoa hiyo ni dharau.Kadhalika penzi linapokuwa limechuja, hata thamani yako pia inakuwa imechuja. Mapenzi ya kweli yaliyokuwa zamani, sasa yanakosa nafasi kwako.

Nini husababisha mapenzi kuchuja?

Kitu cha msingi zaidi baada ya kuona kabisa mwenzi wako amebadilika na kugundua kwamba hayo yamesababishwa na kuchuja kwa penzi, lazima akili yako ifanye kazi sana. Unatakiwa kujua sababu iliyofanya penzi kuchuja.

Mara nyingi, mwenzi wako anapopunguza mapenzi, lazima kulikuwa na mambo ambayo alikuwa akiyapata kwako na sasa anayakosa. Lakini kama haitakuwa hivyo, basi huenda atakuwa amepata mwingine nje ambaye ndiye anayempa upofu na kukuona wewe takataka.

Sababu hizo mbili zinatosha kabisa kukufanya uanze kujichunguza upya na kuangalia mustakabali wa penzi lako. Je, ni mambo gani hayo ambayo ndiyo yaliyosababisha mpenzi wako kupunguza penzi?

Kuna sababu nyingi za kuwa katika hali hii. Nayo sababu kubwa ni wanandoa kubadilika. Mfano, kuna wanaume wengi mnalala mkiwa mnanuka, hamuogi. Hata kukumbatiwa inatia kinyaa, unanuka. Kujaliana ninakosema ni pamoja na kupata muda wa kuzungumza, muulize mwenzi wako anafikiria nini, pale unapomwona ana mawazo mazito. Ndoa huendeshwa kwa kauli nzuri, sio ubabe kama wanavyofanya baadhi ya wanaume.

Kuingia kwenye ndoa hakuna maana kuwa utaishi maisha mazuri sana. Utambue kwamba hakuna miujiza katika ndoa. Iwapo unataka ndoa yako ishamiri, iwe nzuri na yenye kuridhisha, huna budi ufanye kazi ya ziada kuiweka mahali unapotaka. Na kazi hii inajumuisha mawasiliano, kusamehe, kuelewa na kukubali yake ambayo huwezi kuyabadili. Ukitarajia ndoa yako ijitengeneze yenyewe, utaishia kuishi kwenye ndoa mfu kila siku. Kazi kwako mwanandoa.

[email protected]

You can share this post!

Raila, Mudavadi kujipima nguvu Matungu

Wakili aliyejisalimisha ICC asalia pweke Kenya ikijitenga