UMBEA: Siku zote usilolijua haliwezi kukuathiri, hivyo tuliza boli!
Na SIZARINA HAMISI
BINADAMU huwa hachungiki, ukijaribu kufanya hivyo, bila shaka utajiumiza moyo wako na huenda usifanikishe azma yako.
Shida hii ipo zaidi kwa wapenzi, ambao wengi hupenda kufuatilia mienendo ya wapenzi wao ili kuwa na uhakika kwamba hawatendewi yasiyofaa huku wakichekelewa machoni.
Awali niliwahi kufanya mazungumzo na baadhi ya wapenzi kuhusu suala la usaliti.
Baadhi walikiri kwamba kuna uwezekano mkubwa wapenzi wao wanawasaliti lakini wenyewe wanadai ni mambo ambayo wakiyafuatilia sana wanaweza kujikuta wanaachana wakati huenda bado wanapendana.
Wapo waliokiri kwamba wanajua wapenzi wao wana wasichana wengine lakini wameamua kufumbia macho jambo hilo sababu wanaonyesha heshima na hawajafanya mambo hayo mbele ya macho yao.
Wakasema siku zote usijiaminishe kwamba mumeo ama mkeo ni mwaminifu asilimia zote, kwani siku ukweli utakapokufikia, unaweza kupoteza fahamu.
Amani yao kwa walio katika kundi hili ni kwamba wenzao wanawaheshimu na pia hawajawahi kuwafumania.
Kwa upande mwingine, wapo wale wanaoamua kuwa wapole kwani wanajua bayana wakiamua kufuatilia watapata wanachotafuta, watagombana na wenzao na hatimaye wanaweza kuachana.
Kwamba ukimfuatilia sana mpenzi wako unatafuta sababu ili muachane, iwapo hauko tayari muachane ni vyema ukamuamini na kama huko pembeni ana michepuko, hiyo inamhusu yeye na wala sio jukumu lako kufanya upelelezi.
Janga hili lipo pia kwa akina dada, kwani wapo wanaume ambao wanashuhudia wake zao ama wake wa wenzao ambao wakiwa nyumbani wanajiheshimu na kuwa wake wazuri sana, lakini huko pembeni kuna michepuko lukuki.
Kwamba mke ameolewa, anaheshimika na anaonyesha upendo wa hali ya juu kwa mumewe, lakini anachepuka kwa siri na kufanya yale yasiyofaa nje ya ndoa yake.
Katika mazungumzo na kaka mmoja, akaniambia kwamba amewahi kupigwa na butwaa siku alipomuona mwanamke mmoja ambaye anamjua na ambaye ametulia kwa mumewe na asiyekuwa na muda na michepuko akiingia lojingi na mwanaume mwingine ambaye pia alikuwa anamfahamu.
Hali halisi iko hivyo siku hizi. Kuna ambao walifikia hatua ya kukiri kwamba wapenzi wao wanawasaliti na wao pia wanachepuka. Huu mwenendo unaonyesha jinsi mapenzi ya usaliti yamekuwa kama ugonjwa kwa wengine. Wengine wanadhani kuwa na michepuko nje ya ndoa ni kujidhihirisha uanaume ama uanamke.
Kuaminiana kuna umuhimu
Muhimu kwa wale walio kwenye uhusiano ni kumwamini mwenzako kwa kiwango kinachostahili. Sio kwamba umuamini hata kama unaona anakuchezea makida makida, la hasha! Muamini pale ambapo una sababu ya kufanya hivyo.
Ukiona dalili za wazi kwamba anakusaliti, ukafuatilia na kugundua ni kweli ana mtu au watu wengine unaochangia nao penzi, haifai kuvumilia. Kuwa kwenye uhusiano sio lazima kusalitiwa na wala sio lazima kumfuatilia mwenzako kila wakati.
Kwani pia kumfanyia mwenzako ukachero, hakutakupatia suluhisho la kudumu sababu binadamu huwa na mbinu nyingi.
Kuna msemo usemao ukimchunguza sana bata huwezi kumla.
Kwenye mapenzi nako ni hivyo, ukimchunguza sana mpenzi wako huwezi kudumu naye. Hii ni kwa sababu ukiamua kufuatilia sana nyendo za mpenzi wako kuna mambo utayabaini na utashindwa kuendelea kuwa naye.
Kwa maana hiyo ni muhimu kujenga hisia za lazima kwa mpenzi wako ili uwe na amani. Hii kufuatiliana kwa wapenzi hakuna tija na kwamba kufanya hivyo unaweza kumpa hisia mpenzi wako kwamba humpendi na unatafuta sababu za kuachana naye.
Siku zote usilolijua haliwezi kukuathiri, hivyo wakati mwingine ni muhimu kujitunza, kujilinda na kuhakikisha kwamba unakuwa salama katika uhusiano.