UMBEA: Upendo hauna husuda na huwa hauhesabu mabaya
Na SIZARINA HAMISI
KUPENDWA ama kupenda ni hisia zisizoelezeka kwa maneno.
Kupenda ni hisia ambayo haionyeshwi kwa maneno ama hisia pekee, bali pia hujumuisha vitendo na mienendo tuitendayo kwa wale tunaowapenda.
Upendo hujionyesha kwa njia nyingi; kwa ndugu zetu, rafiki zetu ama wapenzi wetu. Wengi huamini kwamba upendo huleta suluhu la changamoto nyingi katika jamii.
Iwapo unaishi na ni mtu mzima usiye na kasoro yoyote, ni lazima utakuwa umewahi kupenda ama kupendwa katika maisha yako. Mapenzi nayozungumzia hapa ni ya watu wawili wanaokutana na kupendana kwa maana ya kuwa na uhusiano wa ziada.
Wale ambao wamewahi kupata hisia hii, wanatambua kwamba kuna mvuto wa kipekee, hasa pale unapokuwa na mtu sahihi katika maisha yako.
Pamoja na yote haya, wapo wengine ambao wamekuwa na wakati mgumu ama kushindwa kuonyesha upendo kwa wawapendao na labda wakadhani wanaonyesha upendo kumbe sio hivyo. Ambapo pia wapo ambao hawajui jinsi ya kupenda na wamekuwa wakijikuta wakipoteza wawapendao mara kwa mara.
Hawa ni wale wasiodumu kwenye uhusiano na mara nyingine hubaki wanajiuliza sababu inayopelekea waachwe mara kwa mara.
Kuna jinsi mbalimbali za kuonyesha upendo kwa mwenzako, ambazo hupuuzwa na wengine na wengine wakazitilia maanani:
- Usikivu ama kumsikiliza mwenzako
Ni muhimu kumsikiliza mwenzako na sio kusikia. Nikimaanisha sikiliza zaidi na ongea kidogo, kwani ukifanya hivi utampatia nafasi mwenzako ya kutoa yote yaliyo moyoni na pia utapata nafasi ya kuelewa hisia zake.
- Uwe na mazoea ya kuuliza unachotaka na kusema asante
Haya ni mazoea rahisi ambayo unaweza kujifunza na kuyafanyia kazi kila siku. Hata hivyo wengi wetu hatuna utaratibu wa kuuliza tunapohitaji kitu kwa wenzetu wala kusema asante pale tunapopata kile tukitakacho. Kwamba unaona kila jambo ni haki yako na hauna sababu ya kusema asante. Ni vyema kuwa na mazoea ya kusema asante, ni neno dogo ambalo lina nguvu kubwa.
- Mwambie ama waambie wale unaowapenda, usipende kimyakimya
Eleza hisia zako kwa mwenzako, mweleze kwamba unampenda na jambo ambalo linakuvutia kwake. Ni vizuri kueleza hisia zako kwa wale walioleta tofauti chanya katika maisha yako. Siku hizi kuna mazoea ya kutuma ujumbe mfupi ama kupiga simu kuzungumza na walio karibu ya maisha yetu. Ni vyema upate muda mara kwa mara wa kuzungumza nao ana kwa ana. Mazungumzo ya uso kwa uso yanaleta ukaribu zaidi ya kutumia njia za kisasa za mawasiliano. Inapobidi, onana na unayeongea naye.
- Wakati mwingine jitolee kuwasaidia wale wenye uhitaji
Siku zote huwa na mtu anayehitaji jambo moja ama lingine. Unaposaidia watu wengine utajisikia vizuri katika nafsi yako. Yule unayemsaidia anaweza kuwa jirani yako, jamaa yako ama nduguyo ambaye alihitaji jambo ama kitu ambacho unao uwezo wa kumsaidia.
Unapojitolea kumsaidia mtu mwingine, usitarajie malipo kwa jinsi moja ama nyingine, kwani kama unatarajia malipo, bila shaka utakuwa hutendi hivyo kwa kujitolea.
- Iwapo unakuwa na wakati mgumu kueleza hisia zako kwa mwenzako, mwandikie barua
Mueleze yale yaliyomo moyoni mwako kumhusu na umuwekee barua hiyo mahali ambako anaweza kuiona. Kwani wengine ni rahisi zaidi kuandika kuliko kuzungumza.
- Katika yote jifunze kusamehe
Kama unapenda ama unampenda mtu utambue kwamba siku zote hawezi kuwa mtilimifu. Yapo mambo ambayo yatakukwaza, usiyaweke moyoni, mweleze inapobidi na uyaache yaende zake.
Upendo hauna husuda na huwa hauhesabu mabaya.