Makala

UMBEA: Wengi waanguka kimapenzi katika kuchagua wenzi sahihi

December 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SIZARINA HAMISI

MAPENZI ni sanaa rafiki zangu.

Ili uweze kuwa msanii kamili katika tasnia hiyo ni vyema kutafuta kuwa bora zaidi kila siku. Uwe mshindi siku zote, mwenye kumridhisha mpenzi daima, mwenye kumfanya afurahie kuwa na wewe.

Lakini katika kutafuta ubora, suala la kujiangalia na kuhakikisha unajenga maisha yako yajayo sawasawa ni lazima. Watu wengi waanguka kimapenzi sababu ya kukosea katika kuchagua wenzi sahihi.

Iwapo bado hujafunga ndoa, huu ni wakati wako sahihi wa kufanya uchaguzi bora ambao hautakuwa na majuto hapo baadaye. Usilenge zaidi leo, wakati unaona wazi kesho ina utata na inaweza kuleta majuto.

Ujue kwamba maisha utakayoishi kesho ni matokeo ya jinsi unavyoishi leo. Wakati mwingine unakuwa na mpenzi wako, ana kasoro lukuki, kila siku ugomvi, hakuna uelewano. Lakini kila unapotaka kuachana naye, hisia kali za mapenzi dhidi yake zinakuzidi na unajikuta ukiendelea na penzi la mateso.

Huu si wakati wa kunyanyasika katika mapenzi, ni muda ambao unatakiwa kuangalia vyema tabia na mwenendo wa mpenzi wako. Kama hairidhishi, usijiumize, chukua hatua ya moja kwa moja huku ukizingatia kwamba, maisha yako yatakayofuata yatakuwa bora ukijivunia ujana wako.

Kama ni kulia, basi lia mara moja lakini uishi kwa furaha katika ulimwengu wa mapenzi.Ukikosea kuchagua, ufahamu kwamba maisha yako yatajawa na machozi. Utalia kila siku, ukinyanyasika sababu ya mapenzi.

Haitakuwa vibaya uachane na fikra potofu. Hata kama unapendwa sana, anajua mapenzi sana, ana faida gani kama kila siku ameendelea kukuumiza? Kukunyanyasa? Kukusimanga? Haoni faida yako, anakudharau waziwazi? Kwa nini uendelee kukaa kifungoni wakati kuna njia?

Lengo hapa sio kufundisha watu kuachana, isipokuwa ningependa kuona wapenzi wanatoka katika utumwa wa mapenzi na kuwa na amani.

Pamoja na yote, mwamuzi wa mwisho wa maisha yako ni wewe. Hatatokea mtu wa kukupangia maisha bora hapo baadaye, yote hayo unapaswa kufanya peke yako. Chagua maisha uyapendayo na uishi katika msingi huo.

Ni vyema ujue umejipangaje maisha yako ya baadaye? Kwamba maisha yako baada ya leo ni yapi? Unahitaji kuishi maisha gani? Maana kama ukiwa hujui unataka kuishi vipi, utakuwa unakwenda tu, bora siku zisogee na mwishowe utajikuta ukijuta.

Utu wako utapimwa kwa jinsi ambavyo unajithamini mwenyewe na unapochukua hatua pale unapoona mwenzako anakukandamiza sababu tu umeamua kumpenda. Usiache akudhalilishe na kukutweza, sababu tu unampenda. Akusasambue sababu tu unamjali na kumuenzi. Kama hali imefikia pabaya, jiweke pembeni na inusuru roho yako dhidi ya majuto. Haitakuwa vibaya ukalivua hilo pendo la zamani na kutakasa moyo wako.

Hakuna kosa kupenda, lakini pia kupenda isiwe taabu.

[email protected]