Umuhimu wa kusoma vitabu
Na MARGARET MAINA
Hukuongezea marifa mapya
Sababu maalum ya waandishi wa vitabu kuandika ni ili kuweka maarifa yao kwenye maandishi. Hivyo kwa kusoma vitabu, unapata maarifa mbalimbali yaliyowekwa kwenye kitabu husika.
Hukuwezesha kufikiri kwa kina
Kwa hakika vitabu huongeza sana uwezo wa kufikiri. Unaposoma vitabu unafahamu mambo ambayo yatakufanya ufikiri zaidi; mara nyingine kitabu kitakuacha na maswali ambayo yatakufanya utafakari kwa kina zaidi juu ya mambo mbalimbali.
Hukuongezea uwezo wa lugha
Mbinu mojawapo ya kuongeza uwezo wa lugha ni kusoma machapisho mbalimbali yaliyoandikwa kwa lugha unayotaka kujifunza.
Kwa kusoma vitabu utaongeza msamiati, utajifunza sarufi ya lugha au hata mbinu mbalimbali za matumizi ya lugha.
Unachotakiwa kuzingatia hapa ni kusoma vitabu bora mara nyingi kadri uwezavyo.
Hukuburudisha
Vitabu ni burudani ya kipekee na ya gharama rahisi unayoweza kutembea nayo pahala popote. Viko vitabu mbalimbali tena vya bei rahisi ambavyo vinaweza kukuburudisha na kukufurahisha.
Vitabu hasa vile vya kifasihi ni burudani ya aina yake. Unaweza kusoma vitabu vilivyochapishwa au vitabupepe kwa kutumia simu au kompyuta yako.
Hukuwezesha kutumia muda vizuri
Unapotumia muda wako kusoma vitabu, ni wazi kuwa hutopata muda wa kupoteza. Kusoma vitabu kutakufanya utumie muda wako kuongeza maarifa yako zaidi.
Huongeza uwezo katika fani ya uandishi
Huwezi kuwa mwandishi bora kama husomi vitabu vya waandishi wengine bora.
Ni lazima ujifunze namna waandishi wengine wanavyopanga mawazo, wanavyotumia lugha pamoja na mbinu nyingine za kiuandishi.
Huondoa msongo wa mawazo
Kusoma vitabu hukufanya uondoke katika lindi kubwa la mawazo yanayokutesa na kukutafakarisha juu ya mambo mengine. Waandishi wa vitabu hujenga mazingira ambayo msomaji hujihisi yumo ndani yake.
Hivyo kwa kusoma vitabu, utaliwazwa, utafarijiwa na hata kutiwa moyo huku ukihamishwa katika mawazo yanayokutesa.