Makala

USHAURI: Ukitaka kunawiri katika ufugaji; hasa wa kuku, tafadhali jiundie lishe

September 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

SUALA la chakula cha mifugo nchini kuripotiwa kutofikia ubora wa bidhaa unaotakikana si geni.

Chakula ‘kikamilifu’ chenye madini faafu ni mojawapo ya vigezo muhimu kuzingatia ili kufanikisha ufugaji wa mifugo na kuku.

Baadhi ya wakulima wameishia kugura ufugaji wa ng’ombe na kuku kwa sababu ya matatizo ya ubora wa lishe.

Kabla kugundua siri ya kuimarisha mradi wake wa ng’ombe, Agnes Magara alikuwa amehangaishwa na suala la chakula duni na cha hadhi ya chini.

Mama huyu ambaye ni mfugaji wa ng’ombe wa kisasa wa maziwa katika Kaunti ya Kajiado, anasema alikuwa na mazoea ya kununua chakula cha madukani na kwamba ng’ombe mmoja alikuwa akizalisha chini ya lita tano.

“Nilikuwa nikipata hasara tupu kwani hawangeweza kujigharimia wenyewe. Maziwa niliyopata yalikimu familia yangu pekee,” aeleza Bi Magara.

Hata hivyo, changamoto hizo zilifikia ukingo alipogundua siri ni kujiundia chakula kwa malighafi yaliyopo; nafaka, majani na madini.

Aidha, ana mashine maalum ya kusaga na kujiundia lishe ya mifugo wake.

Mfugaji huyu ambaye kwa sasa ana takriban ng’ombe 34 wa maziwa anasema kwa siku, mmoja huzalisha wastani wa lita 24, mabadiliko haya yakichangiwa na wazo la kujiundia chakula mwenyewe.

“Katika chakula kingi cha maduka, maelezo ya madini yaliyotiwa huwa ya matangazo tu kukipigia upatu ilhali hakijaafikia ubora,” asema.

Mtaalamu John Momanyi kutoka Sigma Feeds -kampuni inayounda chakula cha mifugo, anasema ili mkulima alenge shabaha sharti chakula kiwe na madini kamilifu.

“Wengi wameacha ufugaji wa kuku na ng’ombe kwa ajili ya kuhangaishwa na chakula duni. Ni muhimu mfugaji awe makini kujua kampuni zinazotengeneza mlo ulioafikia vigezo faafu,” afafanua Bw Momanyi.

Simulizi ya Agnes Magara si tofauti na ya Bw Hesbon Asava kutoka Kaunti ya Vihiga ambaye aliasi ufugaji wa kuku wa nyama 2013 kwa sababu ya chakula cha hadhi ya chini.

Akilimali ilipotembelea mkulima huyu katika kijiji cha Kedeta, Kisienya, kaunti ndogo ya Vihiga, vizimba kadhaa vya kuku ni mahame.

“Nilijipa breki katika ufugaji wa kuku wa nyama miaka sita iliyopita baada ya kuanza kupata hasara kwa ajili ya kuhangaishwa na chakula duni, yaani kisichoafikia madini ya lishe ya mifugo na kuku,” akasema.

Bw Asava ambaye alikuwa afisa katika idara ya kilimo, aliacha gange hiyo mwaka 1992 ili kuvalia njuga kikamilifu ufugaji wa kuku. Anasema ilimgharimu mtaji wa 120, 000 kuanzisha shughuli hiyo.

“Awali, nilikuwa nikisambaza nyama katika mikahawa ya kifahari kama vile Golf, Royal na Sunset, eneo la Nyanza na Magharibi. Nikiondoa gharama ya matumizi; chakula, matibabu na leba, sikukosa kutia kibindoni zaidi ya Sh60,000 kwa mwezi,” afichua.

Hata ingawa baadhi ya vizimba vyake ni mahame, Asava anasema hajaasi ufugaji wa kuku.

“Breki niliyojipa ni kufanya utafiti namna ya kujiundia chakula changu na kilichoafikia ubora. Kwa sasa ninafuga kuku asilia wa kienyeji na unaelewa bei yao eneo la Magharibi haikamatiki. Pia, wananitagia mayai ambayo ni ghali,” adokeza.