• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 10:55 AM
USWAHILINI: Kujisitiri mwanamke wa Uswahili kiini si dini, ni utamaduni!

USWAHILINI: Kujisitiri mwanamke wa Uswahili kiini si dini, ni utamaduni!

Na LUDOVICK MBOGHOLI

KILA jamii ulimwenguni ina msingi wa itikadi ambayo ndiyo chimbuko mahususi la kuendeleza utamaduni wake.

Hali hii ambayo ni kigezo cha kiasili, ndiyo kiini asilia cha ‘jadi’ kinachozingatiwa na jamii mbalimbali.

Hata hivyo, desturi za kimila katika jamii kadha za Pwani zinawiana mno na sheria za kidini, hasa za Kiislamu.

Huenda zikawa za kweli kutokana na sababu zinazotolewa na jamii za watu wa bara na watafiti wa lugha kwamba asilimia kubwa ya wanajamii wa Pwani ni waumini Waislamu.

Hata hivyo kwa jamii za Pwani, madai ya kumezwa kwa utamaduni wa Wapwani na Uislamu si kweli, kwani desturi, mila na utamaduni hauna kigezo chochote ambatanishi cha kuuwianisha na ‘dini’ au ‘dhehebu’.

Dhamira ya makala haya ya leo ni kuangazia utamaduni wa Wapwani unaohusu mavazi ya mwanamke, hasa aliyeolewa.

Jamii za Pwani zinaamini kuwa mwanamke aliyeolewa hastahili kuishi katika mazingira ovyo, hivyo ili kuijenga taswira kamili ya kifamilia, ni sharti mwanamke aliyeolewa ajielewe hayupo tena katika kidato cha ujanani.

Kuusitiri mwili

Ili kudumisha heshima, nidhamu na adabu kwa mumewe, na hasa katika ndoa yake, mwanamke hulazimika kuvaa mavazi bora ya kuusitiri mwili wake ili kuepuka janga la matamanio ya wanaume.

Ni ada ya Pwani mwanamke kuhakikisha haonekani maungo yake ya mwili, hasa maungo yanayovutia matamanio ya mwanamume.

Baadhi ya viungo maalumu vya mwili wa mwanamke ambavyo havipaswi kuonekana hadharani ni kichwa (isipokuwa usoni), sehemu za mikono (isipokuwa viganjani), sehemu za miguu (isipokuwa wayo na kisigino), kifua na eneo zima la makalio.

Mwanamke akitembea Pwani (awe kaolewa au hajaolewa) akiwa kavaa mavazi yasiyositiri maungo (kama tulivyotaja juu), basi kulingana na mila, desturi na tamaduni za Wapwani huonekana kama maaluni.

Aidha, mwanamke kama huyo hutengwa na kuepukwa, kwani tayari amepotoka na kupotosha jadi na asili ya ‘adabu za mwanamke’.

Hata hivyo, kulingana na mabadiliko ya ulimwengu kwa jamii za kisasa, mavazi ya sitara yanapuuzwa huku ikidaiwa ‘mavazi hayo ni maalumu tu kwa wanawake wa jamii za waumini Waislamu’.

Ingawa hivyo, mtazamo huu unapingwa na Waswahili wenyewe, wanaodai kuwa ni ada ya tangu jadi kwa wanawake Wapwani kuvaa mavazi ya kuwasitiri maungo.

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Hii hapa nususi ya usahihi wa baadhi ya...

VITUKO: Baada ya dhifa ya Sindwele, Pengo afumaniwa na mke,...

adminleo