USWAHILINI: ‘Mtori’ lishe bora ya kitamaduni kwa wajawazito Pwani
Na LUDOVICK MBOGHOLI
JAMII zinazoishi katika maeneo ya Pwani Magharibi, zimekuwa na itikadi ya kijadi ya kuhakikisha wajawazito wako katika hali salama ya kiafya kabla ya kujifungua.
Jamii hizi zinatilia maanani kuwa wanawake wajawazito wanastahili kutunzwa vyema kuliko wanawake wengine ambao hawajapata ujauzito.
Jamii hizi zinaamini mjamzito hawezi ‘kulea mimba’ ipasavyo ikiwa anapata lishe kiholela isiyoweza kustahimili machovu anayopitia.
Jamii za Wataita, Wapare, Wataveta na jamii ya Chagga kutoka mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania (inayowiana na jamii za pwani ya Kenya kuhusu kitamaduni), zilishikilia msimamo wa imani kali kuwa, ili mjamzito aweze kustahimili ulezi bora wa mimba changa hadi kufikia ukomavu, anapaswa kula chakula cha kumwezesha kuondoa uchovu na uchungu wa makuzi ya kitoto kichanga anachokokibeba tumboni.
Chakula bora cha kitamaduni kilichoidhinishwa na wazee wa kale enzi ya matambiko ya kimila ni mtori.
Mtori ambacho ni chakula kinachopendwa sana miongoni mwa jamii ya Chagga, ni mkorogo wa ndizi zilizopikwa na kuchanganywa na vipande vya nyama za utumbo wa mbuzi au ng’ombe, na ukikosekana utumbo, mjamzito hulazimika kuukubali mtori uliochanganywa na samaki.
Tamaduni za kale za jamii ya Wataveta, Wapare na Wataita kupitia wakongwe wanaoishi leo hii, zinashikilia kwamba mtori ni lishe muhimu kwa wajawazito, ingawa mabadiliko ya usasa na mambo ya kileo yanafanya lishe hii kuonekana kama iliyopitwa na wakati.
Yamkini, wataalamu na madaktari wakongwe wanaotoka katika maeneo ya jamii hizi tulizotaja, wanaamini kwamba lishe hiyo ya kitamaduni ni bora zaidi kwa wajawazito licha ya kutothaminiwa na kizazi mamboleo.
Hata hivyo, itikadi ya jamii hizi ni kuwa, ‘moyo’ wa mjamzito ukiwa haupendi ‘mtori’, anaandaliwa lishe ya ndizi ambazo hazijafanyiwa mkorogo ila tu kuchanganywa na nyama ya utumbo au samaki. Akikinai mchanganyiko huu, basi ale ndizi pekee na uji wa wimbi au ngano.
Huchukuliwa kwamba mchanganyiko huu humwongezea nguvu zaidi mjamzito na kumwezesha kustahimili mimba inayokua, akajihisi mwepesi bila kutatizika.
Wadadisi wanasema wakati wa kujifungua, mjamzito ‘husukuma mtoto’ kwa urahisi na haandamwi na uchungu mwingi wa uzazi.
Hata hivyo inadaiwa kwamba si ndizi zote huwafaa wajawazito. Ndizi muhimu zaidi ni ‘mshale’, inayopatikana kwa wingi Uchagani.