USWAHILINI: Taswira ya mandhari ya kupendeza ya mji wa Lamu
Na HAWA ALI
KUSAFIRI kwa mashua hadi kwenye bandari ya Lamu ni mojawapo wa mandhari ya kupendeza ya mji wa Kiswahili wa Lamu.
Upepo huvuma bila kukoma kutoka Bahari ya Hindi iliyo kubwa ya rangi ya samawati. Mawimbi mepesi ya feruzi huosha fuko zenye mchanga mweupe.
Majahazi ya mbao ya muundo wa kale hunyiririka kandokando ya pwani, huku matanga yake yenye umbo la pembetatu na ya rangi nyeupe yakifanana na vipepeo wanaopuruka. Yakiwa yamepakiwa samaki, matunda, nazi, ng’ombe, kuku, na abiria, yaelekea kwenye bandari ya Lamu.
Gatini, michikichi inayovuma kwenye upepo mwanana wenye joto hutokeza kivuli kidogo kwa wanaume wanaopakua shehena kutoka kwenye meli za mbao.
Soko limejaa pilikapilika za watu wenye kelele wanaofanya biashara ya kubadilishana bidhaa. Wafanyabiashara hao hawatafuti dhahabu, pembe za tembo, au watumwa, bali ndizi, nazi, samaki, na vikapu.
Chini ya kivuli cha mwembe mkubwa, wanaume wanasokota kamba ndefu za makonge na kushona matanga ya vitambaa yanayoendesha majahazi yao ya mbao.
Barabara ni nyembamba na zimejaa watu wanaoelekea kila upande. Wafanyabiashara waliovalia kanzu ndefu kubwakubwa waita watu kutoka kwenye maduka yao yasiyo na mpangilio, wakiashiria wateja waje na kujionea bidhaa zao.
Punda, anayejikaza kuvuta mkokoteni wa mbao uliojaa magunia mazito ya nafaka, apita katikati ya watu wengi. Wakazi wa Lamu waelekea kutoka upande mmoja wa kisiwa hadi mwingine kwa miguu, kwa kuwa hakuna magari ya kusafiria kisiwani. Njia pekee ya kufika kisiwani ni kwa kutumia mashua.
Jua lifikiapo upeo katikati ya mchana, wakati huonekana kuwa umesimama.
Katika joto kali, ni watu wachache ambao hutembea, na hata punda husimama bila kusonga wakiwa wamefunga macho yao kabisa ili kujituliza na joto hilo.
Jua lianzapo kushuka na halijoto kupungua, kisiwa hicho chenye utulivu hujaa utendaji.
Wafanyabiashara hufungua wazi milango yao mizito iliyochongwa kwa mbao ili kuanza biashara, na taa zao zitaendelea kuwaka hadi usiku wa manane. Wanawake huosha watoto wao na kuwasugua kwa mafuta ya nazi mpaka ngozi zao zinaanza kung’aa.
Wanawake huanza kutayarisha chakula wakiwa wamekalia mikeka iliyofumwa kwa makuti ya nazi.
Hapa wanawake bado hupika kwa kutumia mafiga, wakitayarisha vyakula vyenye ladha tamu vya samaki waliokolezwa vikolezo vyenye kunukia vizuri na wali uliopikwa kwa tui. Watu ni wenye urafiki, wakarimu, na wapole.
Ijapokuwa Lamu haina fahari kama zamani, utamaduni wa Kiafrika wa zamani uliokuwako kabla ya Karne ya 20 ungali unastawi hapa.
Chini ya jua la kitropiki, maisha yanaendelea kama yalivyokuwa karne nyingi zilizopita. Ukiwa hapa unaweza kuona mambo ya kale na ya wakati wa sasa pia. Kwa kweli, Lamu imeokoka enzi iliyopita kwa njia ya kipekee, ni kisiwa ambacho kimedumu bila kubadilika.