Makala

UTU: Mwanamke aliyewapa damu watu mahututi mara 61

January 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MAGDALENE WANJA

MARA ya kwanza kwa Bi Aisha Dafalla kutoa damu alikuwa na umri wa miaka 17, na alizirai papo hapo baada ya zoezi hilo.

Hii ilitokana na uoga mwingi uliompata kwani hii alikuwa angali mtoto pamoja na kuwa mara ya kwanza kuhisi damu yake mwenyewe ikitolewa.

Bi Dafalla alikuwa katika kidato cha tatu na alikuwa ameandamana na wenzake kwani walimwambia kuwa wangepewa soda na mkate baada ya kutoa damu.

“Baada ya tukio hilo, niliogopa sana zoezi la utoaji damu na niliapa kutoshiriki tena kwa kuhofia maisha yangu,” alisema Bi Dafalla.

Hii ilikuwa hadi mwaka 1986 wakati rafiki yake alipomjia akitaka amsaidie kutolea nduguye damu kwani alikuwa amuhusika na ajali mbaya barabarani.

Alimuomba amtolee nduguye damu kwani ana uwezo wa kumchangia mtu yeyote. Baada ya kulifikiria suala hilo, alikubali kutoa damu na zoezi hilo likafaulu.

“Nilifurahi sana kwamba niliweza kuokoa maisha ya mgonjwa huyo na nikaamua kujitolea kuokoa maisha zaidi,” akasema Bi Dafalla.

Kuanzia siku hiyo, Bi Dafalla ambaye ana umri wa miaka 55 sasa, alianza kutoa damu mara tatu kila mwaka.

Bi Aisha Dafalla alipohojiwa na Taifa Leo Dijitali mjini Nakuru. Picha/ Maggy Wanja

Hii imemfanuya kutambulika kama mwanamke ambaye ametoa damu mara nyingi zaidi kufikia mwaka 2016 na huduma ya Kenya National Blood Transfusion Service.

“Nilishangaa sana kwani sikutarajia kuwa kuna rekodi zinazowekwa kuhusu wanaotoa damu,” alisema.

Kufikia sasa Bi Dafalla ametoa damu mara 61, akichukua nafasi ya pili nchini baada ya Bw Kennedy Alpha Sanya ambaye ni afisa wa polisi mwendesha mashtaka katika mahakama ya Nakuru.

 “Nimeifanya kama ibada kuta dau na huwa nachukua mapumziko wakati ambapo nina uja uzito ama ninaponyonyesha,” alisema.

 Bi Dafalla alitoa changamoto kwa wanawake kuwa mstari mbele katika kutoa damu kwani wanawake wengi hujipata matatani haswa wanapohitaji msaada.

 “Wanawake wajawazito, wagonjwa wa saratani, manusura wa ajali na wagonjwa wengine ni baadhi ya wanaohitaji damu zaidi na iwapo kuna ukosefu, kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza maisha,” aliongeza.

Bi Dafalla pia aliipa changamoto jamii yake akiwemo mwanawe mwenye umri wa miaka 23 na marehemu mumewe.

“Mwanangu ametoa damu mara 10 sasa natumai atafuata nyayo zangu nitakapoacha kutoa damu sababu ya umri,” aliongeza Bi Dafalla.

Aliongeza kuwa kuifanya ibada kutoa damu kunasaidia katika kumpa binadamu muongozo wa kuishi maisha kwa uangalifu.

Hii ni kwa sababu unapoifanya tabia, utakuwa muangalifu haswa kwa vyakula.

“Kutoa damu ni mojawapo ya mambo ambayo hunifanya kuridhika haswa kwa kujua kuwa anaokoa maisha ya watu, wengine amabo siwafahamu,” aliongeza Bi Dafalla.