Makala

VIJANA NA ZARAA: Wadau wahimiza vijana kujitosa katika kilimo cha kahawa, wasitegemee serikali

March 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

KILIMO cha kahawa nchini hakitarudia hali yake ya zamani ikiwa vijana hawatahusishwa kikamilifu, wadau wanasema.

Ili kuhakikisha sekta hii imefufuka, serikali inapaswa kuweka sera za kuvutia vijana na kuwapa motisha waweze kukikumbatia.

Wanasema kwa miaka mingi, wakulima wa kahawa humu nchini wamekuwa wakikosa kunufaika na mabadiliko katika sekta hiyo na kuimarika kwa bei katika soko la kimataifa kwa kulaza damu na kupuuza mumea huo.

Wengi wao, wanaeleza wataalamu, ni wazee huku vijana wakipuuza sekta hii kwa sababu ya kukosa kuungwa mkono na serikali.

Washikadau katika sekta ya ukuzaji na uuzaji wa kahawa wanasema kuwa ni kwa kuimarisha ukuzaji wa zao na kuwapa shime wakulima wadogo ili waweze kupata faida ya jasho lao.

Na katika harakati za kuinua ukuzaji wa zao hilo muhimu, washikadau wameanza kampeini kabambe ili kuimarisha sekta hii ambayo miongo mitatu iliyopita ilikuwa tegemeo la watu wengi na kuchangia katika uchumi wa nchi.

“Ninasikitika kufichua kuwa wakulima wa mashamba madogo ambao walichangia sekta hii wametelekeza mashamba yao ya kahawa na kuanza kupanda mimea mingine. Huenda nchi hii ikakosa pesa nyingi wakati huu ambao bei ya kahawa katika soko ya kimataifa inaendelea kuimarika,” Bw Jeremy Block, mkurugenzi wa kampuni ya C Dorman, amekuwa akinukuliwa akisema mara kwa mara.

C Dorman imekuwa ikiandaa kahawa kwa soko la humu nchini na kimataifa kwa miaka mingi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyu wakulima wa mashamba madogo ya kahawa kote nchini wanatoa thuluthi mbili za kahawa nchini.

Takwimu zaonyesha kuwa wakulima wa mashamba madogo walivuna tani 2229 huku vyama vya ushirika vikitoa tani 1021.

Katika kipindi hicho wenye mashamba makubwa na wastani walichangia tani 391 na 380 mtawalia.

Kiwango cha uzalishaji kilishuka huku wakulima waking’oa kahawa na kushiriki katika shughuli zingine za kibiashara.

Bw Block anakiri kuwa sera duni na ufisadi zilichangia katika hali hii huku wakulima wakikosa imani na mawakala wao.

“Nchi hii ilikuwa na uwezo wa kuimarisha ukuzaji wa kahawa na kupigana na ufukara, lakini sera mbaya na ufisadi zilifanya mambo kuwa kinyume,” asema na kuongeza kuwa kahawa ya humu nchini inapendwa sana katika soko ya kimataifa.

Asema ipo haja ya kuweka mikakati thabiti ili kulinda wakulima na upunjaji wa mawakala.

“Serikali inapaswa kuendeleza mpango wa “kusafisha” sekta hii kama ilivyofanya ilipopiga marufuku kampuni saba zilizokuwa zikiwanyanyasa wakulima,” asema na kuongeza kuwa wakulima wanaweza kurudia kilimo cha kahawa kama miaka ya zamani.

Wakulima na washikadau wengine wameonyesha kuridhika na mpango wa kuweka huru soko ya kahawa ingawa kiwango cha uzalishaji kingali cha chini. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuwahimiza vijana kushiriki kilimo cha kahawa ili kuendeleza ukuzaji wa zao hilo.

Mwaka jana, serikali ilitoa kitita cha Sh3 bilioni kusaidia wakulima mashamba madogo ya kahawa katika juhudi za kufufua sekta hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Serikali wakulima wengi wa kahawa ni watu wa umri mkubwa huku vijana wakipuuza mumea huo wakisema hauna faida ya maana. Wataalamu wa kilimo na biashara wanasema bei ya kahawa imeimarika na wanakadiria kuwa itanawiri katika siku zijazo.

“Ni hii ndio sababu vijana wanapaswa kushiriki kilimo ili wavune kutokana na kuimarika kwa bei na kuchangia katika uchumi wa nchi,” asema Bw Roy Kamau ambaye ni mwanauchumi.

Na imebainika kuwa vyama vya ushirika vinavyoshughulika na kahawa vimekubwa na mizozo ya uongozi jambo ambalo linachangia kudorora kwa ukuzaji wa kahawa.

Ni migogoro ya vyama iliyofanya waziri wa vyama vya ushirika Peter Munya kuingilia kati na kuleta mabadiliko katika sekta hiyo. Wakulima tuliozungumza nao walisifu hatua ya waziri na wakamtaka awe jasiri ili kupigana na mabwenyenye walionuia kuangamiza sekta hiyo

“Hatua ya waziri inafaa hasa wakati ambapo shirika lilikubwa na madeni,” asema mkulima John Katiku ambaye ni mwanchama wa chama cha ushirika cha Muthunzuuni wilayani Machakos.

Na hatua ya serikali ya kuweka huru uuzaji wa kahawa imeleta matumaini kuwa wakulima.

Anasema ipo haja ya vijana wengi kukumbatia kilimo cha Kahawa ikiwa sekta hii itarudia hali yake ya zamani na kuwa fahari kwa nchi.