Makala

Vijana wa mijini wakwama mashinani

January 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya vijana waliofika katika vijiji kujivinjari Krismasi na Mwaka Mpya wamezidi kukwama huko baada ya kuishiwa na pesa na kwa sasa wanauza baadhi ya bidhaa zao ghali kwa bei ya kutupa.

Wengine wanaonekana wakisaka ajira za muda kama vibarua ili wakusanye nauli.

Walio wabunifu zaidi wamejigeuza kuwa wahubiri ndani ya magari ya uchukuzi wa umma ilimradi wapate usafiri wa bure.

Simu za gharama ya zaidi Sh15,000 zinauzwa kwa Sh2,000 huku kompyuta za bei ya zaidi ya Sh30,000 zikiuzwa kwa Sh10,000.

“Hata kuna baadhi nimewaona mjini Maragua wakiuza nguo zao kama jaketi, long’i na mashati kwa bei iliyokatwa kwa asilimia 70,” akasema mshirikishi wa muungano wa wakazi Bw Mohammed Omar Maluki.

Bw Maluki alisema kwamba hata kuna wengine wanafanya wizi wa mimea na mavuno katika mashamba yao na kukimbia nayo sokoni ili wapate mapeni ya kuwawezesha kurejea mijini.

“Huwezi amini kwamba hawa ndio waliokuwa wakitesa wakinengua kila aina ya mitindo katika baa na disko za hapa, wakila vinono mitaani na kujifanya hata hawaelewi lugha za hapa vijijini. Leo hii ndio hao wamekuwa wapole na wanyenyekevu wakiomba, kukopa na kusaka wateja wa bidhaa zao wakiwa wasanifu kwa lugha ya mama,” akasema.

Wengine wanaonekana wakienda kazi za vibarua kama za kulima, kuchanja kuni, kuchota maji, kuchuna majanichai au kubeba chakula cha mifugo ili kujipa nauli na pia za matumizi wakirejea mijini.

“Sisi hata imetubidi tuuze kuku wetu watano kufanikisha safari ya kakangu kurejea jijini Nairobi. Baada ya kulewa, kukimbizana na disko na wasichana hapa kijijini, alimaliza pesa licha ya kwamba alitakiwa kuwa kazini Januari 8, 2024,” akasema msichana mmoja katika kijiji cha Kigumo.

Akaongeza: “Lakini akawa hana hata ndururu. Alisema atanunulia mamangu kuku wengine 10 mwishoni mwa Februari.”

Katika Kaunti ndogo ya Murang’a Kusini, tayari Naibu Kamishna wa eneo hilo Bw Gitonga Murungi ametoa onyo kwa wanaouziwa vitu kama simu na kompyuta wahakikishe wameandikiana mikataba ya mauzo kukiwa na mashahidi au wanunue katika vituo vya polisi ili kujiepusha balaa ya kesi.

“Tumegundua katika miji ya eneo hili kama Maragua, Kenol, Kambiti, Makuyu na kwingineko kuna watu wa mijini ambao wanauza simu, kompyuta, nguo, viatu na pia mikufu na saa. Wanaonunua wanafaa wajichunge hao watu wasiwauzie halafu wakimbie polisi baadaye waripoti kupotea kwa bidhaa hizo wameuza kwa hiari,” akatahadharisha Bw Murungi.

“Na unajua wakiripoti utasakwa na utakamatwa na kile kitakuokoa ni mkataba wa mauzo, mashahidi au nambari ya kitabu cha matukio katika kituo cha polisi,” akaongeza.

Msaidizi wa Kamishna katika tarafa ya Maragua Bw Joshua Okello alifichua kwamba visa vya warembo wa mijini kutapeli wanaume vimezidi.

“Warembo hao wanaingia mjini na kujifanya kama wanaosaka mapenzi. Katika kuchumbiwa hasa na wazee na walevi, wanapora au wanatapeli wanaume hao pasipo kutumia nguvu,” akasema Bw Okello.

Kwingine ambapo vijana hao wanasaka hela ni kupitia wakopeshaji almaarufu shylocks ambao wanawaagiza kutoa simu au kompyuta kama mdhamini.

“Unapata simu ya Sh20,000 inatolewa mkopo wa Sh5,000 huku kompyuta ya Sh40,000 ikilinganishwa na mkopo wa Sh15,000 na ambapo riba ni kati ya asilimia 40 na 70 katika kipindi cha mwezi mmoja,” akasema Bi Stella Mbithi ambaye hukopesha pesa katika mji wa Thika.

[email protected]