VIKEMBE: Martinelli kivuli chipukizi cha Ronaldo
Na CHRIS ADUNGO
TANGU ujio wa mkufunzi Unai Emery, mambo yameanza kubadilika uwanjani Emirates kwa kiwango fulani.
Sura mpya za wachezaji wachanga wenye kiu ya kujituma vilivyo zimeanza kujitokeza.
Isitoshe, urafiki na ushirikiano mkubwa kati ya Alexandre Lacazette, Nicolas Pepe na Pierre-Emerick Aubameyang katika safu ya mbele ya Arsenal ni jambo linalotarajiwa kuwakosesha wapinzani usingizi kwa muda mrefu ujao.
Hatua ya Emery kuwasajili wachezaji Matteo Guendouzi na Lucas Torreira imekuwa kiini cha kuboreka zaidi kwa ngome ya Arsenal ambayo itasalia kubebwa na chipukizi tele wanaojivunia utajiri mkubwa wa vipaji.
Kwa pamoja na Emile Smith Rowe, Robbie Burton, Folarin Balogun, Eddie Nketiah, Reiss Nelson, Bukayo Saka, Kieran Tierney, Joe Willock na Gabriel Martinelli ni miongoni mwa wachezaji wachanga wanaobeba mustakabali wa Arsenal migongoni mwao kwa sasa.
Akiwa mzawa wa eneo la Guarulhos jijini Sao Paulo, Martinelli, 18, alianza kupiga soka ya kitaaluma katika kikosi cha makinda wa Corinthians, Brazil mnamo 2010.
Baada ya kuwaridhisha kambini mwa kikosi hicho, alianza kuwa kivutio cha klabu ya Ituano, Brazil mnamo 2015 huku akinyemelewa pia na Manchester United na Barcelona waliomfanyia majaribio.
Mnamo Novemba 4, 2017, Martinelli alitia saini mkataba wa kurasimisha uhamisho wake hadi Ituano katika maelewano yalitoyarajiwa kumdumisha kambini mwa kikosi hicho hadi Oktoba 2022.
Mchuano wake wa kwanza ni kibarua kilichowakautanisha na Corinthians mnamo Machi 17. Alitokea benchi katika mechi hiyo na kuchangia bao la pili lililofungwa na Claudinho katika ushindi wa 2-1 waliousajili ugenini. Katika umri wa miaka 16 na miezi tisa, aliingia katika mabuku ya historia ya Ituano kuwahi kuwajibishwa na kikosi hicho katika Ligi Kuu ya Brazil.
Bao lake la kwanza katika kikosi cha watu wazima ndani ya klabu ya Ituano lilikuwa katika mechi ya ugenini iliyowakutanisha na Taboao da Serra mnamo Septemba 2018. Bao alilolipachika wavuni liliwachochea waajiri wake kusajili ushindi mnono wa 4-1 katika mchuano huo wa kuwania ubingwa wa kipute cha Copa Paulista.
Baada ya kuwa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Ituano, Martinelli alijizolea jumla ya mabao sita mwishoni mwa msimu wa 2018-19 na kuibuka mfungaji bora wa kivumbi cha Paulista kilichowashuhudia wakitinga hatua ya robo-fainali. Ushawishi wake ulidhihirika zaidi alipowasaidia Ituano kukizamisha chombo cha Bragantino 3-0 katika mchuano wa ugenini wa Ligi Kuu ya Brazil mnamo Machi 15, 2019.
Bao msimu wa kujifua
Baada ya utajiri wa kipaji chake kudhihirika katika kampeni za msimu uliopita, Martinelli alianza kuandamwa na zaidi ya vikosi 20 kote duniani. Ingawa hivyo, alihiari kujiunga na Arsenal chini ya mkufunzi mzawa wa Uhispania, Unai Emery.
Alifunga bao katika mchuano wa kujifua kwa msimu mpya wa 2019-20 na hivyo Kusaidia Arsenal kusajili ushindi wa 3-0 dhidi ya Colorado Rapids kutoka Amerika.
Aliwajibishwa na Arsenal kwa mara ya kwanza katika EPL mnamo Agosti 11, 2019, alipotokea benchi katika dakika ya 84 kujaza nafasi ya Henrikh Mkhitaryan aliyesajiliwa na AS Roma ya Italia kwa mkopo wa mwaka mmoja mwanzoni mwa msimu huu.
Arsenal walivuna ushindi wa 1-0 katika mchuano huo dhidi ya Newcastle United uwanjani St James’ Park.
Mnamo Septemba 24, 2019, Martinelli alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal dhidi ya Nottingham Forest walionyukwa 5-0. Alifunga mabao mawili katika mchuano huo wa kuwania ufalme wa Carabao Cup.
Ndiye aliyefungua na kufunga karamu hiyo ya mabao baada ya kushirikiana vilivyo na beki Calum Chambers.
Baada ya kula na kushiba sifa tele kutoka kwa kocha Emery na mashabiki wa Arsenal, Martinelli aliwajibishwa tena katika kivumbi cha Europa League dhidi ya Standard Liege ya Ubelgiji.
Alifunga mabao mawili na kuwasaidia waajiri wake kusajili ushindi wa 4-0 uwanjani Emirates.
Alicheka na nyavu za Liege kwa mara ya kwanza kunako dakika ya 17 kwa kukamilisha krosi ya Kieran Tierney kabla ya kuandaliwa pasi nyingine na Dani Ceballos. Tierney na Ceballos pia ni wachezaji wapya walioingia katika sajili rasmi ya Arsenal mwanzoni mwa msimu huu.
Ingawa ni mzaliwa wa Brazil, Martinelli ana usuli wake nchini Italia alikozaliwa babaye mzazi. Aliitwa kambini mwa Brazil mnamo Mei 20, 2019 kuwa sehemu ya kikosi ambacho kocha Adenor ‘Tite’ Bacchi alikitegemea pakubwa kunyanyua ufalme wa Copa America mwaka huu.