Vita kanisani SDA vilivyosababisha waumini 10 kujeruhiwa
POLISI mjini Kisii wanachunguza kisa ambapo Wakristo kumi wa Kanisa la Kiadventista (SDA) la Nyabigena wanasemekana kujeruhiwa baada ya mapigano kuzuka kanisani humo Jumamosi iliyopita wakati wa ibada.
Chanzo cha machafuko hayo kinasemekana kusababishwa na mzozo unaohusisha makongamano mawili yanayong’ang’ania umiliki wa kanisa hilo.
Kulingana na Bi Martha Bosibori-mmoja wa waathiriwa- mzozo kati ya makongamano hayo umekuwepo kwa muda sasa. Kila kongamano linadai kumiliki kanisa hilo.
“Kulizuka fujo wakati mmoja wa wazee wa kanisa alipotangaza kwa waumini wengine kwamba kulikuwa na wasaliti waliokuwa wamehudhuria ibada ya Sabato iliyopita. Mara tu alipomaliza kutoa tangazo hilo, watu wasiojulikana walivamia kanisa na kuanza kuwavuruga waumini na kizaazaa kilishuhudiwa,” Bi Bosibori alidai.
Katika video inayoonyesha matukio yaliyojiri ndani ya majengo ya kanisa hilo, waliohusika katika machafuko hayo wanaonekana wakishambuliana kwa mateke na ngumi.
Viti vya plastiki vinatupwa kote huku wale wanaopigana wakijaribu kulimana visawasawa.
Wanawake wanasikika wakipiga nduru kwa kustaajabishia kile kilichowapata.
“Hili ni kanisa la aina gani sasa? Mbona unanipiga ninapojaribu kuwaokoa baadhi ya watu wetu?” Sauti ya mwanamke inasikika ikiuliza kwenye video hiyo.
Kufikia kuandikwa kwa taarifa hii, uongozi wa kanisa la SDA bado haukuwa umetoa taarifa yoyote kuhusu suala hilo.
Taifa Leo ilipowasili kanisani humo, ilikutana na kundi la wazee na wachungaji wakiwa wamejikita katika mkutano.
“Hebu kwanza tushauriane na tuone kama tutawahutubia,” mmoja wa washiriki wa mkutano huo alisema bila kujitambulisha.
Licha ya kufanya wanahabari wetu kusubiri nje ya kanisa hilo kwa zaidi ya masaa matatu, kundi hilo mwishowe halikufanya kweli kuhusu ahadi yao kwani halikutoa taarifa yoyote.
Badala yake wazee hao walisema tuje kuangazia maandamano ambayo walisema walikuwa wakiyapanga.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Nyamarambe Thomas Parkolwa, alithibitisha kutokea kwa hitilafu hizo na kusema wameanzisha uchunguzi wao.
“Tuliitwa huko baada ya mzozo kutokea. Si kazi yetu kuamua nani anamiliki kanisa lakini watu wanapokuwa na vurugu, tunapaswa kuwajibika. Maafisa wetu wamelishughulikia suala hilo na tumeanza uchunguzi. Tulipofika kanisani, hakuna mtu aliyekuwepo na walikuja kuripoti tu wakati mapigano hayo yalikuwa yameisha,” Bw Parkolwa aliambia Taifa Leo kwa simu.
Mkuu huyo wa polisi alikashifu kundi moja ambalo alisema halikuwa tayari kushirikiana nao.
“Tumejaribu kuwapatanisha, tumewaomba waangazie njia nyingine za kutatua mgogoro uliopo lakini kuna kundi ambalo halitaki kusikia chochote, wao ndio waliotoa video ya mapigano wakitaka isambae mitandaoni. Inasikitisha sana kwamba matukio kama haya yanaweza kutokea katika kanisa la kisasa,” kamanda huyo aliongeza.
Aliwataka wakaazi au mashirika mengine yoyote kutafuta njia zingine za kutatua migogoro badala ya kupigana.