Afya na JamiiMakala

Vyakula vinavyosaidia kukabili changamoto ya kukosa usingizi

Na MWANDISHI WETU May 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KUNA baadhi ya watu ambao inapowadia wakati wa kulala, wao hukumbwa na changamoto ya kupata usingizi mzuri. Ikiwa wewe ni mmoja wao, basi unapaswa kujua kwamba kuna vyakula ambavyo vinaweza kukusaidia wakati huu. Hivi ni pamoja na;

Maziwa yaliyopashwa moto: Maziwa yana viwango vya juu vya kemikali ya tryptophan, aina ya amino acid ambayo hubadilika na kuwa serotonin.

Serotonin inajulikana kutokana na sifa zake za kutuliza ubongo, na hivyo kukusaidia kulala vyema.

Ukitaka kuimarisha sifa hii waweza ongeza kungumanga, iliki au hata kitunguu saumu kwenye kikombe cha maziwa. Cheri: Tunda hili lina kemikali ya melatonin, aina ya homoni inayozalishwa na tezi ndogo zinazopatikana kwenye ubongo, na ambazo hudhibiti jinsi tunavyolala na kuamka. Wataalam wanasema kwamba kula kati ya cheri 10 na12 kwaweza kusaidia kupata usingizi bora.

Ndizi: Ndizi zina viwango vya juu vya madini ya magnesium na potassium ambayo husaidia kutuliza misuli.

Aidha, chakula hiki kina kiwango kizuri cha kabohaidreti ambazo huchochea usingizi.

Lozi: Mbali na kuimarisha nguvu za ubongo, lozi huchochea usingizi.

Sawa na maziwa, lozi huwa na kemikali ya tryptophan ambayo hutuliza ubongo na neva.

Kwa upande mwingine, madini ya magnesium ni muhimu katika kuthibitisha mpigo wa moyo.

Chokoletiza utusitusi: Aina hii ya chokoleti huwa na kemikali ya serotonin ambayo husaidia kutuliza akili na neva zako, na hivyo kuchochea usingizi.

Shayiri: Chakula hiki hushibisha upesi na hivyo ni mwafaka katika kupunguza uzani.

Mbali na hayo, shayiri ina kemikali ya melatonin ambayo itakusaidia kulala upesi.