Makala

VYAMA VYA KISWAHILI: CHAKISAJO; nguzo imara inayothibiti Kiswahili St Josephs Girls Kakamega

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Mtakatifu Yosefu, Kakamega kiliasisiwa mnamo Januari 12, 2019 kwa lengo la kuinua viwango vya lugha ya Kiswahili shuleni pamoja na kuwaunganisha wanafunzi, walimu, wafanyikazi na jamii nzima kwa kutumia lugha adimu ya Kiswahili.

Shule ya wasichana ya Mtakatifu Yosefu Kakamega inapatikana katika eneo la Murram, Wadi ya Shirere, Lurambi kwenye Barabara Kuu ya Kakamega-Mumias.

Ni shule ya Kikatoliki inayoongozwa na watawa wa Mtakatifu Maria, Kakamega.

Ni miongoni mwa shule zinazotia fora katika mitihani ya kitaifa na viwango vya nidhamu katika kaunti nzima ya Kakamega na janibu za Magharibi ya Kenya.

CHAKISAJO kilizinduliwa rasmi na Bw Emmanuel Viambaka katika hafla ya kufana iliyoandaliwa kwenye ukumbi wa bwalo shuleni humu.

Licha ya kuwa chama kichanga, CHAKISAJO tayari kina wanachama zaidi ya 50 wakiwemo walimu, walezi, wanafunzi, wafanyakazi na wakaazi wa eneo zima la Shirere.

Baadhi ya walezi wa chama hiki ni Bi Esther Ayuma (Mkuu wa Idara ya Lugha), Bi Mercy Kerreh na Bw Ing’ahu Gabriel. Chama pia kina wahusika kutoka idara nzima ya Lugha shuleni wakiwemo Bw Andati Justus, Bw Litali Justine na Bi Yvone Nekesa.

Wawakilishi wa vidato ni pamoja na; Margret Nanyama na Mwanaamisi Omar (Kidato cha Kwanza), Linah Khatonde (Kidato cha Pili), Atieno Rose (Kidato cha Tatu) na Kadenyi Lynette (Kidato cha Nne).

Wawakilishi wa vidato tofauti wana majukumu kadhaa ikiwemo kuwashauri wanafunzi wenzao kutilia maanani dhima ya Kiswahili nchini.

Wawakilishi hawa wamechangia pakubwa kujenga mtazamo chanya kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wenzao.

Chama kinazidi kutekeleza majukumu mengi mno nje ya darasa yakiwemo kuandaa midahalo shuleni kila Jumanne alasiri. Midahalo hii hushirikisha walimu, wanafunzi na wapenzi wa Kiswahili kutoka eneo hili.

Kitengo cha SJEB FM kina wanahabari mahiri wakiongozwa na Jadema Whitney.

Hawa husoma mkusanyiko wa matukio shuleni na habari nyingine kisha kuwasilisha gwarideni kila Jumatatu na Ijumaa.

Pia kuna kitengo cha ucheshi na mashairi ambacho huwatumbuiza wageni katika hafla tofauti shuleni na hata nje ya shule.

Wanafunzi pia wameshiriki katika tamasha mbalimbali zikiwemo tamasha za muziki na drama hadi kufikia kiwango cha kitaifa.

Juhudi hizi zote zimetokana na uongozi bora wa Mtawa Phoebe Anyango ambaye ni rasi wa shule akishirikiana pakubwa na Naibu wake Bi Wilmina Makondo.

Licha ya mafanikio haya, CHAKISAJO kinapitia changamoto mbalimbali zikiwemo; mtazamo hasi miongoni mwa wanafunzi na walimu.

Hili huathiri sana kiwango cha matokeo ya somo la Kiswahili katika KCSE.

Ukosefu wa hela za kukiimarisha chama na kuandaa warsha, midahalo na makongamano makubwa pia ni changamoto.

Hata hivyo, chama kinajitahidi kwa vyovyote vile kuipa lugha ya Kiswahili hadhi inayostahiki shuleni na hata nje ya shule.