VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Njega Boys, Kirinyaga (CHAKIMANJE)
Na CHRIS ADUNGO
CHAKIMANJE ni chama ngangari katika ukuzaji na uenezaji wa lugha ashirafu ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Maghulamu wa Njega katika gatuzi la Kirinyaga.
Ni chama ambacho kimewawezesha wanafunzi wa Njega Boys kupiga hatua na kutia fora si katika makuzi ya Kiswahili tu, bali pia katika matokeo ya mitihani ya kitaifa ya KCSE.
Shule hii kwa sasa imekuwa miongoni mwa zile zinazojivunia matokeo bora zaidi katika kaunti nzima ya Kirinyaga.
CHAKIMANJE kiliasisiwa mapema mwaka huu na Bw Oloo Charles ambaye ni mwalimu wa Kiswahili shuleni Njega Boys.
Kikiwa chini ya ulezi wa Bw Oloo na Bi Nyoike Grace ambaye pia ni mkereketwa na mpenzi wa Kiswahili shuleni Njega Boys, CHAKIMANJE kwa sasa kinafadhiliwa na Bw Elias Gitobu (Mwalimu Mkuu), Bw Kimani (Naibu Mwalimu Mkuu) na Bw Tharao (Mkuu wa Idara ya Kiswahili).
Watatu hawa ni watetezi wakubwa wa Kiswahili na kila wazungumzapo, Kiswahili chao huvutia sana, utadhani wao huchemshiwa ili wanywe kamusi zote za Kiswahili asubuhi ya kila siku.
Malengo makuu ya CHAKIMANJE ni pamoja na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa dhati ndani na nje ya shule kwa kuwapa wanafunzi jukwaa la kuhudhuria makongamano na kuzuru shule mbalimbali za upili na za msingi ili kuwahamasisha wanafunzi kuhusu umuhimu wa Kiswahili kama somo na pia kitega uchumi.
Sanaa
Maazimio mengine ni kukuza vipaji vya usanii kupitia kwa sanaa za utambaji wa hadithi, uigizaji wa vitabu vya fasihi hasa tamthilia, riwaya na hadithi fupi zinazotahiniwa katika shule za upili na kukuza waandishi chipukizi wa mashairi na kazi nyinginezo bunilizi.
Isitoshe, huwaunganisha wanafunzi wote shuleni na kutoa fursa kwa wanachama kuwahamasisha wanafunzi wenzao wa shule za msingi na upili kuhusu umuhimu wa Kiswahili.
Chama hiki kwa sasa kipo chini ya uongozi wa Trajan Ndegwa (Mwenyekiti), Juma Baraza (Naibu Mwenyekiti), James Muriithi (Katibu Mkuu), Lewis Mwangi (Mwekahazina) na Sabastian Robert (Afisa Mwenezi na Uhusiano Mwema).
CHAKIMANJE pia kimeanza harakati za kuchapisha jarida la chama.
Dhima kuu ya jarida hili ni kuzua mijadala muhimu katika taaluma za Kiswahili na kuwapa wanafunzi nafasi ya kujieleza na kukuza vipaji vyao katika nyanja mbalimbali za utunzi.