Makala

VYAMA VYA KISWAHILI: Jopo la Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Kyeni, Machakos lulu halisi ya lugha Mashariki

July 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

VYAMA vya Kiswahili vina dhima teule katika shule yoyote.

Huwa vinatoa jukwaa la kukuza vipawa mbalimbali vya wanafunzi katika ubunifu, uandishi, ulumbi na ushairi.

Kimojawapo cha vyama hivi ni Jopo la Kiswahili lililoasisiwa na walimu na wanafunzi katika Shule ya Msingi ya Kyeni, Kaunti ya Machakos mnamo 2001.

Jopo hili la Kiswahili lina majukumu manne makuu: kuwapa wanafunzi nafasi ya kuwafunza wenzao walio na udhaifu katika lugha ya Kiswahili, au katika mada ambazo zinawatatiza; kuwapa nafasi wanafunzi kujadili masuala tata ya lugha; kuandaa hafla za Kiswahili na mijadala kwa kuhusisha shule mbalimbali za upili na kuchapisha ‘Jarida la Utukufu wa Kiswahili’.

Jarida hili hushughulikia masuala ya lugha, fasihi, msamiati na burudani katika Kiswahili; na makala huchangiwa na wanafunzi wa shule mbalimbali, walimu, wataalamu na wapenzi wa Kiswahili kutoka maeneo tofauti ya Kaunti ya Machakos.

Dhima ya jarida ni kuzua mijadala muhimu katika Kiswahili, kuwapa wanafunzi wenye ari ya kuandika kwa Kiswahili jukwaa la kuchapisha makala mafupi na vilevile kujadili matumizi fasaha ya istilahi teule katika lugha hii inayozidi kukua kwa kasi.

Isitoshe, huwapa walimu nafasi ya kuchapisha makala yenye uketo kuhusu masuala ibuka katika mtaala na Kiswahili kwa jumla.

Kupitia Jopo la Kiswahili, walimu na wanafunzi wa Kyeni sasa wana jukwaa bora zaidi la kuzamia usomaji wa magazeti ya Taifa Leo kupitia Mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG).

Kupitia mradi huu, NMG inayatumia magazeti ya Taifa Leo kuimarisha viwango vya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili na masomo mengine katika shule za msingi na upili.

Bi Catherine Musyoka ambaye ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Kyeni anakiri kwamba matokeo bora yaliyojivuniwa na wanafunzi wake katika mtihani wa KCPE 2018 ni zao la NiE.

Kwa mujibu wa mwalimu huyu, wengi wa wanafunzi wake wanaothamini na kuchangamkia usomaji wa Taifa Leo na kushiriki Shindano la Uandishi wa Insha hudumisha umahiri wao katika lugha kwa kukwangura alama za juu zaidi katika mtihani wa KCPE Kiswahili.

Anaungama kwamba majaribio hayo ya mitihani ni daraja halisi la mafanikio kwa wengi wa wanafunzi wake ambao wamechochewa kutia fora katika lugha ya Kiswahili.