Makala

Waapa kuacha pombe baada ya kupofuka ulevini

March 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 4

LUCAS BARASA NA GEORGE MUNENE

BAADHI ya watu walionusurika kufa baada ya kunywa pombe katika Kaunti ya Kirinyaga, sasa wanasimulia masaibu yaliyowapata.

Ingawa wamepofuka, wanamshukuru Mungu kuwa wangali hai.

“Sitawahi kunywa pombe tena.” Ni maneno yaliyomtoka kinywani Mzee Joseph Gichamba,72, ambaye ni kipofu baada ya kunywa pombe iliyoshukiwa kuwa na sumu eneo la Kangai, Kirinyaga na kusababisha vifo vya watu 17.

Sammy Ngari Nthiga,35, alirudia maneno yale yale baada ya kupofuka alipokunywa pombe hiyo.

Gichamba na Nthiga ni miongoni mwa watu watano waliopoteza uwezo wa kuona baada ya kunywa pombe iliyo na sumu kwenye baa katika vijiji vya Kangai na Kandogu ambavyo viliwapoteza watu sita Februari 5, 2024, huku wengine 11 wakifariki siku iliyofuatia.

Baa ya California iliyoteketezwa katika kijiji cha Kangai, Kerugoya, Kaunti ya Kirinyaga mnamo Februari 7, 2024. PICHA | GEORGE MUNENE

Taifa Leo ilivitembelea vijiji hivyo ambavyo vilikuwa vitulivu, eneobunge la Mwea mnamo Jumatatu na kuwapata manusura hao, jamaa na marafiki wa waliofariki bado wanajaribu kung’amua matukio yalivyo.

Mbali na watu 15 kutoka eneo la Kangai na wawili wa Kandogu waliofariki, kunayo makaburi mengine ambayo wanaume na wanawake, wazee na vijana walizikwa hapo kutokana na pombe hiyo.

Wanakijiji hao wanasema walizika kimyakimya wengine waliofariki baada ya kunywa pombe hiyo ili kuepuka mzozo na serikali.

Bw Gichamba akiwa ameketi chini ya kivuli katika shamba lake, alisema amehuzunika baada ya kupoteza uwezo wa kuona na rafikiye wa kike alifariki akinywa pombe hiyo katika Baa ya California ambayo wakazi hao waliivamia baadaye na kuteketeza baada ya vifo hivyo.

“Ninamshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yangu ingawa siwezi kuona tena,” Bw Gichamba alisema.

“Sasa nimekosa maana kwani siwezi kujisimamia mwenyewe. Mke wangu alikufa miaka tisa iliyopita. Mwanamke niliyekuwa nikiishi naye pia alikufa baada ya kunywa kileo. Sasa nimelazimika kumtegemea mwanangu ambaye hufanya kazi za kawaida kwa kila kitu,” akaendelea kusimulia.

Bw Gichamba alisimulia jinsi alivyoenda kwenye baa hiyo na rafiki yake wa kike na kuanza kunywa pombe pamoja.

Baadaye alijiondoa kwa vile alikuwa na kazi ambayo haikuwa imekamilika na kumwacha mpenziwe Stella Muthoni kwenye baa.

Alipofika nyumbani, alihisi maumivu ya tumbo na kugundua kuwa haoni vizuri.

“Nilipofika nyumbani, nilijihisi vibaya na nikakimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Kerugoya na kuwekewa maji. Nilipokuwa nikipelekwa hospitalini niliona kidogo lakini nilipoachiliwa nilikuwa kipofu kabisa,” alisema.

Aliingiwa na hofu zaidi aliposikia kwamba baadhi ya wanakijiji waliokuwa wamelazwa katika wadi moja naye wameaga dunia.

“Nilipoambiwa kuwa wanakijiji waliokunywa pombe katika baa moja wamezimia, nilipatwa na wasiwasi na kuanza kumwomba Mungu na akasikia maombi yangu, namshukuru Mungu kwamba ingawa sioni, niko hai,” alisema.

Bw Gichamba alijuta kwamba alikuwa amepoteza uwezo wa kuona kutokana na kunywa pombe mbaya.

“Kwa kweli nilikuwa nimenunua glasi moja ya pombe hiyo kwa jina la utani Wajackoya kwa Sh50. Kama kawaida, nilipewa glasi nyingine iliyojaa kinywaji hicho bila malipo ambayo ilinipiga teke na kurudi nyumbani,” alisema.

Bw Gichamba alisema amekuwa akinywa pombe kwa miaka mingi lakini hajawahi kuuziwa vileo ‘mbaya’.

Bw Gichamba aliomba serikali kuondoa pombe yenye sumu kutoka vijijini ili kuepuka visa hivyo.

Mwathiriwa mwingine ni Bw Nthiga ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye shamba, kunyunyizia mimea maji ili kupata riziki yake ila kwa sasa anamtegemea pakubwa mamake Veronica Micere.

“Mamangu ambaye ni mjane sasa ananishughulikia, ananipikia chakula na kunipeleka kliniki. Siwezi kujifanyia chochote kwa sasa… najuta kwa nini nilikunywa pombe hiyo,” alisema.

Ana matumaini kwamba atapona kabisa na kuanza kuishi maisha ya kawaida bila utegemezi kwa mara nyingine tena.

Bw Nthiga anapanga kumrudisha mke wake ambaye alitoroka nyumba ya ndoa kufuatia ugomvi wa kinyumbani.

“Kabla ya tukio mke wangu alitoweka nyumbani baada ya kutofautiana namim Nikipata nafuu nitamrudisha pamoja na mtoto wangu,” alisema.

Bw Nthiga alikuwa ameungana na marafiki zake katika baa hiyo mwendo wa saa kumi na mbili na nusu jioni ili kukata kiu yake.

Baada ya kujiburidisha, jamaa huyo alirejea nyumbani na wakati wa kulala alihisi dalili sawa na mwezake Bw Gichamba.

Kulipokucha alijipata akipoteza kuona.

“Rafiki yangu alikuwa na gari na nilipomweleza jinsi nilivyokuwa ninajisikia, alikubali kunipeleka hospitalini. Nilipofika hospitalini, niliwekewa dripu mara moja kwa sababu nilikuwa naishiwa maji mwilini kwani nilikuwa naendesha. Hivyo ndivyo nilivyonusurika,” alisema Bw Nthiga.

Bw Nthiga alikuwa akifurahia unywaji pombe lakini hakuhisi kuwa siku moja mambo yangebadilika na kuwa mabaya zaidi kutokana na kileo cha bei nafuu.

Mamake Nthiga anafurahia kuona mwanawe akiwa hai.

Bi Micere alisema familia nyingi zilibaki kwenye mshangao kwa kupoteza wapendwa wao.

“Nahisi vibaya ninapoona baa zikiendeshwa vijijini. Naunga mkono msako unaoendelea dhidi ya baa za vijijini na operesheni hiyo iendelee,” alisema Bi Micere.

Ingawa hivyo alisema tangu mwanawe anywe pombe hiyo yenye sumu, amekuwa akitumia pesa nyingi kwa matibabu.

“Mara nyingi mimi hutumia Sh1,000 kukomboa gari la kumpeleka kliniki. Pia natumia Sh900 zaidi kwa ajili ya dawa zake. Mimi ni mkulima mdogo na kutafuta fedha hizi ni kazi kubwa kwangu,” alisema mama huyo wa watoto wanane.

Mbunge wa Mwea Mary Maingi aliidhinisha utoaji wa leseni kwa baa kurejeshwa kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni Dhidi ya Unywaji Pombe na Dawa za Kulevya (Nacada) ili kuepusha kaunti kutoa leseni hizo.

“Kuna mgongano mkubwa wa kimaslahi. Gavana anaweza kukataa kuingilia baa ili asiwaudhi wapigakura wake. Masharti yote ambayo baa zisiwe karibu na taasisi za umma, shule, maeneo ya makazi na makanisa yanapaswa kuzingatiwa,” alisema Bi Maingi katika mahojiano katika afisi yake ya Hazina ya Maendeleo ya Eneobunge (NG-CDF0 huko Mwea.

Bi Maingi alishinikiza kupigwa marufuku kwa utengenezaji wa vileo vya kizazi cha pili na cha tatu akitaka biashara hiyo nzima kupigwa marufuku kutoka utengenezaji hadi unywaji.

Taifa Leo imebaini kuwa baa iliyosababisha mauaji ya watu 13 imezungukwa na nyumba za makazi. Hii ilifanya iwe rahisi kwa wanakijiji wengi kupata pombe ya bei nafuu ambayo pia iliwaacha wengine wengi vipofu hafifu na wengine vipofu kabisa.

Familia zimebaki na uchungu na kiwewe. Kutajwa kwa neno pombe haramu katika kijiji katika Kaunti Ndogo ya Mwea-Magharibi, husababisha hofu nyingi.