Akili MaliMakala

Wadudu wanaosaidia kukabili mabadiliko ya tabianchi

Na LABAAN SHABAAN October 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WADUDU maarufu Black Soldier Flies (BSF) wanasaidia katika juhudi za kukabili athari mbaya za mabadiliko ya hali ya anga.

BSF ni wadudu weusi ambao huwa chanzo cha chakula chenye virutubisho vya protini; wadudu hawa huliwa na mifugo kama vile kuku, nguruwe na samaki.

Zaidi ya hao, nzi weusi huzalisha mbolea ya kiasili inayoimarisha kilimo na afya.

Sammy Kanyuira ni mkulima na mtaalamu wa kilimo ambaye hufuga BSF na kuwatumia kama lishe ya mifugo eneo la Sagana, Kaunti ya Kirinyaga.

“Uzuri wa kilimo hiki ni kwamba kinasaidia ulimwengu katika harakati ya kupambana na athari ya mabadiliko ya hali ya hewa,” anaeleza.

“Vile vile ni njia mbadala kwa wafugaji wa nguruwe, ndege na samaki kupunguza gharama ya chakula kwa asilimia kubwa sana.”

Kulingana na wataalamu, teknolojia ya BSF inaweza kupunguza utoaji wa gesi za greenhouse ikilinganishwa na njia nyingine ya kutengeneza mbolea.

Wadudu hawa kadhalika hugeuza uchafu wa kikaboni ambao unatupwa ovyoovyo katika mazingira na kuwa chakula cha mifugo ama mbolea.

Utafiti umeonyesha kuwa BSF wameibuka kuwa muhimu katika kupunguza utoaji wa gesi ya amonia ambayo ni hatari kwa mazingira.

Mchakato huu wa kibayolojia hutoa gesi kidogo ya amonia kuliko mtindo mwingine wa kuzalisha mbolea maarufu vermicomposting.

Ubadilishaji wa kibayolojia unaotokana na BSF hutoa amonia kidogo kuliko mboji kupitia uozeshaji wa malighafi kutoka shambani na sokoni.

Ufugaji wa nzi hawa weusi ni wenye uendelevu na huwa na athari kidogo sana ya kiikolojia.

Malisho na mbolea

Ingawa ufugaji wa BSF haueleweki sana na wakulima wengi, ni suluhu bora kwa changamoto za ufugaji na uzidishaji wa mapato.

Kanyuira anafafanua jinsi BSF inavyoweza kuboresha uzito wa mifugo kama nguruwe, kuku, na samaki kwa hadi asilimia 26.

“Katika mazingira ya kiuchumi ambapo asilimia 70 ya mapato ya wakulima yanaenda kwenye malisho, BSF inatoa njia ya kupunguza gharama na kuongeza faida,” anakiri.

Kulingana na Kanyuira, vijana na kina mama wana nafasi nzuri ya kunufaika na mfumo huu wa kilimo biashara.

Yeye hutumia mbolea kutoka kwa BSF kukuza miti ya matunda kama vile michungwa na migomba.

“Ninatoa wito kwa vijana na wanawake kuzamia kilimo hiki cha kisasa,” Kanyuira anafafanua.

“Kupitia mafunzo, wanaweza kuelewa jinsi ya kutengeneza malisho ya mifugo kwa kutumia BSF, na hivyo kuongeza uzito wa mifugo yao na kwa njia hiyo, kuzidisha mapato.”

Wadudu hawa wanakula uchafu wa sokoni, na hivyo kuunda mbolea yenye virutubisho vingi; hii ni njia endelevu ya kutatua tatizo la taka na kuboresha udongo.

Kanyuira anafahamisha kuwa iwapo mkulima yeyote ana nia ya kuanzisha ufugaji wa BSF, hatahitaji uwekezaji mkubwa.

“Wakulima wanaweza kutumia vifaa vilivyopo nyumbani kama miti na mabati kuunda mazingira mazuri ya kuhifadhi wadudu. Hata katika maeneo ya mijini, ni rahisi kuanzisha kilimo hiki bila haja ya kuwa eneo kubwa.”

Sammy Kanyuira aonyesha chungwa lililokuzwa kutumia mbolea inayokuzwa kwa mbolea itokanayo na BSF. Picha|Labaan Shabaan