Wafanyabiashara wanaoshiriki mtandao wa chakula wapigwe jeki
WAWEKEZAJI, mashirika na kampuni wametakiwa kupiga jeki kifedha wafanyabiashara wanaoshiriki kwenye mtandao wa uzalishaji na usambazaji chakula.
Himizo hilo limetolewa na BoP Innovation Center (BoPInc), shirika lisilo la kiserikali na linalosaidia wajasiriamali na kampuni kutoa msaada kwa jamii.
Akizungumza Jumatano, Mei 21 kwenye kongamano la Financing Agri-Food Systems Sustainably (FINAS 2025), katika Ukumbi wa KICC, Nairobi, Vivian Chumba afisa kutoka BoPInc alisema kampeni kuangazia baa la njaa na uhaba wa chakula Kenya na Bara Afrika kwa jumla itafanikishwa kupitia wawekezaji, mashirika na kampuni kupiga jeki wanaoshiriki mtandao wa uzalishaji chakula.
Wanashirikisha wafanyabiashara na wakulima – ambao ni nguzo kuu katika kuhakikisha watu wanapata chakula.
Bi Vivian aliambia wajumbe na waliohudhuria kongamano la FINAS mwaka huu, kwamba wahisani na wathamini wakijitokeza kusaidia serikali na washirika kwenye sekta ya kilimo, ajenda kuziba mwanya wa uhaba wa chakula itakuwa rahisi kufanikishwa.
“Wawekezaji, muwapige jeki wafanyabiashara wa chakula na wakulima… Wafadhili, nanyi (kama vile mashirika ya kifedha na benki) boresheni sheria zenu za kutoa mikopo na ufadhili, ili iwe rahisi kuinua wanaochangia kuhakikisha tunapata chakula,” afisa huyo alisema.
Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/habari/marufuku-ya-waziri-kagwe-kuhusu-macadamia-yasambaratisha-bei/
FINAS 2025, lengo lake kuu ni kujadili na kuainisha mikakati kupiga jeki kifedha sekta ya kilimo na mtandao wa chakula.
Kwa muda mrefu, wakulima hasa wa mashamba madogo wamekuwa wakilalamikia kukosa mikopo kutoka kwa mashirika ya kifedha na benki kwa sababu ya kukosa dhamana (collateral) na mdhamini (guarantor).
BoPInc, ambayo ni taasisi huru na yenye makao yake nchini Uholanzi, imekuwa ikipiga jeki wajasiriamali katika sekta za chakula, maji, na nishati.
Ikiwa inafanya kazi katika nchi 26, pia inaunga mkono mashirika yasiyo ya kiserikali, biashara changa, biashara ndogo na za kati (SMEs), pamoja na kampuni kubwa za kimataifa katika kufanikisha biasharana kuinua jamii.
“Tunafanya kazi na SMEs zaidi ya 1,000 Barani Afrika, na tunaomba wadauhusika wengine waungane nasi kufadhili wafanyabiashara ili kuboresha uchumi,” Vivian alihimza.
Kongamano la FINAS 2025 lilianza mnamo Jumanne, Mei 20 na kuendelea hadi Mei 22.
Kaulimbiu yake ikiwa, “Taking Ownership: Rethinking Sustainable Financing for Africa’s Food Systems,” ilileta pamoja viongozi, mashirika na kampuni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kujadili mikakati kuboresha sekta ya kilimo kupitia ufadhili.
Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Mutahi Kagwe akifungua rasmi kongamano hilo mnamo Jumanne, Mei 20, aliahidi kuhakikisha sekta ya kilimo inapata angalau asilimia 10 ya mgao wa bajeti ya kitaifa kila mwaka.
Bw Kagwe alilalamika kwamba sekta hiyo inaendelea kupitia changamoto kwa sababu ya ufadhili mdogo, licha ya mchango wake mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Kenya.
Aidha, Waziri aliahidi kushinikiza nyongeza ya mgao wa bajeti kutoka asilimia 3 ya sasa hadi asilimia 10 ya bajeti ya kitaifa.
“Licha ya kuchangia asilimia 50 ya Pato la Taifa (GDP) —asilimia 22.5 moja kwa moja na kati ya asilimia 25 hadi 30 kwa njia isiyo ya moja kwa moja, sekta ya kilimo inapokea mgao wa asilimia 3 pekee ya bajeti ya kitaifa kwa sasa. Hili halikubaliki. Ninajizatiti kuongeza mgao huu hatua kwa hatua hadi kufikia asilimia 10,” aliahidi.
Waziri Kagwe alisema kuwa ongezeko hilo litaisawazisha Kenya na Azimio la Malabo (2014) na Azimio la Kampala la Januari mwaka huu, 2025, maazimio ambayo yanapendekeza serikali za Bara Afrika zitenge asilimia 10 ya bajeti zao za kitaifa kwa kilimo.