Wajane washirikiana kujikimu kimaisha
Na SAMMY WAWERU
Ikiwa kuna tukio linaloumiza moyo maishani ni kupoteza mpendwa wako, jambo ambalo huacha mwathiriwa na makovu na majeraha ya moyo.
Baadhi ya wanaoachwa katika hali hiyo hupitia unyanyapaa, yaani kutengwa na wanafamilia na pia jamii. Isitoshe, kuna wanaodhulumiwa kwa njia tofauti, suala ambalo ni kinyume cha sheria.
Si kisa kimoja, viwili au vitatu…vimeangaziwa na vyombo vya habari wajane na mayatima kufurushwa walikoolewa na kuachwa, wamenyimwa urithi. Kwa hakika ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha.
Masaibu hayo si hekaya kwa Rose Ngunge, ambaye baada ya kumpoteza mumewe mwaka wa 2008 alipitia madhila chungu nzima.
Si kutimuliwa alikoolewa na pia kutengwa alikozaliwa, si kulala njaa, si kufungiwa alikoishi, si kunyimwa maji, si kunyang’anywa mazao ya kilimo aliyokuza mwenyewe…changamoto hizo zikiwa haba tu kuziorodhesha.
Ni madhila ambayo 2015 yalimchochea kuanzisha shirika lisilo la kiserikali, Bethel Widows & Orphans C.B.O, analosema limekuwa la manufaa tele kwa wajane na mayatima Nairobi.
“Kufuatia matatizo chungu nzima niliyopitia, nilijiweka kwenye kiatu cha wajane wenza, nikatafuta njia ya kuwanasua na pia kuwapa matumaini maishani,” Rose ambaye ni mama wa watoto watatu anasema.
C.B.O imekuwa katika mstari wa mbele kutafutia baadhi ya watoto yatima katika eneobunge la Kasarani, Nairobi, ufadhili wa masomo, ambapo hulipiwa karo kupitia hazina ya NG-CDF.
Rose, 53, pia anasema wajane hupokea mikopo ya serikali kama vile Uwezo Funds na Women Enterprise Fund & Affirmative Action Fund (NGAAF) kupitia Bethel Widow and Orphan C.B.O, inayowawezesha kuanzisha biashara na pia kujiimarisha kimaendeleo.
Mwaka wa 2016, mama huyo ambaye ni mcheshi na mkwasi wa utu, alianzisha mpango wa kutoa mafunzo ya kozi za kiufundi kwa wajane, anaosema umelenga kuwapa msingi kuwekeza katika biashara. “Kozi tunazowafunza zinawasaidia kujiendeleza kimaisha,” anasema.
Mafunzo yanayotolewa ni pamoja na utengenezaji wa kofia za nywele (wigs), ufumaji vikapu maarufu kama ‘viondo’, mikeka, bidhaa za shanga, ushonaji nguo kwa cherahani, uundaji sabuni ya majimaji, jiki na dawa za kuosha vyoo.
Shirika hilo pia hutoa mafunzo ya uokaji keki, kupika mahamri na namna ya kuunda maziwa ya mtindi, maarufu kama yoghurt. “Tuna wakufunzi ambao huja kutunoa makali,” Rose anaelezea.
Anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba C.B.O ilianza na wanawake 15 pekee, ambao kufikia sasa ni zaidi ya 100.
“Tulichanga kila mmoja Sh20, na kupata mfadhili aliyetununulia vifaa na malighafi ya thamani ya Sh2, 700,” Rose anadokeza.
Aidha, anasema walianza kwa kutengeneza sabuni, kisha mwaka wa 2017 wakaingilia ufumaji wa vikapu na pia utengenezaji wa mikeka. “Mwaka uliopita, 2019, ndipo tulianza uundaji wa wigs,” anaelezea.
Huku kundi hilo la wajane likiwa na kina mama walio kati ya umri wa miaka 32 – 86, Rose anasema limewazesha kujiendeleza kimaisha na pia kukimu mahitaji muhimu ya kimsingi.
Shughuli ya mafunzo hayo huiendeshea katika ukumbi wa kuwezesha vijana kujiimarisha eneo la Sunton, Mwiki, eneobunge la Kasarani. Pia, wana duka wanalokodi Sh5, 000 kwa mwezi na ambalo ni la ushonaji nguo.
Akiridhia jitihada za Bethel Widows & Orphans C.B.O, Mary Kisia mmoja wa wajane, anasema ameweza kukimu familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi. “Bidhaa tunazounda pia huziuza ili kuweza kulisha familia,” Mary anasema, kauli inayoradidiwa na Susan Wanjiru ambaye pia ni mjane.
Hata hivyo, safari ya shirika hilo haijakuwa mteremko. Rose Ndunge anasema ukosefu wa fedha za kutosha kununua malighafi ndiyo changamoto kuu.
“Soko lipo, ila hatuna uwezo kutengeneza bidhaa kwa wingi kwa sababu ya ukosefu wa fedha kununua malighafi na vifaa vingine muhimu vya kazi hii ya sanaa,” Rose akasema wakati wa mahojiano, ambapo tulipata kina mama hao wakijibidiisha katika gange tofauti.
Alisema wengi wao wana matatizo ya kiafya, akifafanua kuna wanaougua ugonjwa wa Ukimwi, Kisukari, ugonjwa wa Moyo na pia walemavu, kati ya matatizo mengine na kwamba kupata matibabu ni balaa.
“Tunaomba serikali na pia wasamaria wema, iwapo tutapata kituo maalum cha afya ili kuhudumia waliogonjeka itakuwa afueni. Wengi huhangaika kupata dawa hasa kipindi hiki cha Homa ya Corona (Covid-19),” Rose akaelezea maombi ya kina mama hao.
Hali kadhalika, alisema baadhi ya mashine – vyerahani wanavyotumia kutoa mafunzo ya ushonaji nguo aliazimwa na mama rafikiye. “Tungepata ukumbi mkubwa utakaositiri idadi kubwa, tutaweza kujiimarisha kimaisha na pia kuinua jamii,” akasema.
“Ikizingatiwa kuwa haya ni mafunzo ya sanaa, tutaweza kujiendeleza kimaisha na kusomesha watoto tulio nao shuleni na katika taasisi za elimu ya juu,” akaongeza Margaret Tariko.
Wakati wa mahojiano tulimpata Rose ambaye pia ni fundi wa nguo, akiwa na wajane kadhaa, akisema awamu ya kwanza huwa majira ya asubuhi na ya pili kuanzia adhuhuri.
Bidhaa wanazounda huziuza kati ya Sh50 na Sh6, 000. Hatua walizopiga mbele kimaendeleo, Rose anasema Dianah Kamande, mwasisi na mwanzilishi wa Come Together Widows and Orphans Organization – CTWOO, amekuwa wa mchango mkuu.
Dianah ambaye pia mjane na mwathiriwa wa dhuluma, ni mmoja wa wakurugenzi wa Bodi ya kupambana na tohara kwa wasichana na kina mama, FGM, nchini.
Mwaka wa 2012 mama huyo alitambuliwa na Rais (mstaafu) Mwai Kibaki, ambapo alipokea tuzo ya kiongozi wa taifa, HSC, inayopokezwa walioafikia makuu katika jamii.
Mbali na zawadi hiyo ya kiongozi wa taifa, Dianah ametambuliwa katika ngazi ya kimataifa.