Makala

Wakazi katika ngome ya Ruto walalama kuhusu ahadi hewa

Na ERIC MATARA December 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKATI wa kampeni zake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022, Rais William Ruto alitaja miradi muhimu ambayo angepatia kipaumbele aliyoahidi kutekeleza katika eneo la South Rift katika mwaka wake wa kwanza ofisini.

Miradi hiyo inayolenga kuboresha maisha ya wakazi ni pamoja na Bwawa la Itare linalogharimu Sh38 bilioni, uboreshaji wa barabara kuu ya Rironi-Nakuru-Mau Summit, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Lanet na eneo la Viwanda la Egerton.

Zaidi ya miaka miwili ya urais wake, ahadi hizi kwa kiasi kikubwa hazijatekelezwa. Wakazi katika eneo la South Rift wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu muda wa utekelezaji wa miradi mikubwa waliyoahidiwa.

Katika kaunti ya Nakuru, Rais Ruto aliahidi kufufua Bwawa la Itare linalogharimu mabilioni lililokuwa limekwama chini ya uongozi wa rais Uhuru Kenyatta kufuatia madai ya ufisadi. Hata hivyo, miaka miwili ya uongozi wake, ujenzi haujaanza tena.

“Bwawa la Itare lilikusudiwa kusuluhisha suala la uhaba wa maji huko Nakuru na kaunti jirani. Bado tunasubiri ujenzi urejee kama alivyoahidi Rais. Wakati huo huo, tunaendelea kuteseka na tumelazimika kuchimba visima ili kukabiliana na uhaba wa maji,” alisema Bw Joseph Mutai, mkazi wa Kuresoi Kusini.

Bi Alice Korir, mkazi wa Kuresoi Kaskazini alikuwa na maoni sawa. “Mradi huu umecheleweshwa kwa muda mrefu. Kuukamilisha kutasuluhisha kabisa suala la uhaba wa maji Kuresoi, Nakuru na kwingineko. Ninamwomba Rais William Ruto kufufua ujenzi huo bila kuchelewa,” asema.

Afisa mkuu kutoka Shirika la Maendeleo ya Maji la Rift Valley, alisema kuwa mipango ya kurejesha ujenzi wa bwawa imekamilika.

“Mwanakandarasi ataanza kazi karibuni. Ujenzi ulipaswa kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu,” afisa huyo alisema.

Katika ziara ya hivi majuzi, Msemaji wa Serikali, Bw Isaac Mwaura alifichua kwamba ujenzi wa bwawa hilo lililokwama utaanza tena ifikapo Desemba 2024.

Hata hivyo, uchunguzi ulibaini kuwa hakuna kazi iliyoanza katika eneo la Ndoinet, Kuresoi. Wakazi waliripoti kuwa hakuna shughuli katika eneo la ujenzi.

“Mwanakandarasi ameanza kukusanya vifaa na mitambo kwa ajili ya kufufua kazi za ujenzi. Ninataka kuwahakikishia wakazi kwamba mradi huo unaosubiriwa kwa hamu utaanza tena kufikia Desemba,” alisema Bw Mwaura wakati huo.

Uboreshaji wa barabara kuu ya Rironi-Nakuru-Mau Summit kwa gharama ya Sh160 bilioni pia umekwama.

Barabara hiyo yenye shughuli nyingi ni hatari kwa ajali imepewa jina la ‘mtego wa kifo.’ Wakazi kama John Langat, mtoa huduma ya kwanza kwa waathiriwa wa ajali za barabarani katika eneo la Ngata-Sobea-Salgaa, wanataka hatua za haraka zichukuliwe. Uboreshaji uliopangwa wa Uwanja wa Ndege wa Lanet huko Nakuru pia umekwama.

Mradi huo unaolenga kukuza utalii na kilimo ulipangwa kukamilika Agosti 2021. Vile vile, mradi wa Egerton Agro-City Park unaotazamiwa kuwa kitovu cha viwanda katika kaunti ya Nakuru haujaanza kutokana na mizozo ya umiliki wa ardhi.

Katika Kaunti ya Narok, ahadi za kujenga kiwanda cha kusindika maziwa kwa gharama ya Sh750 milioni kupitia kampuni New Kenya Cooperative Creameries (KCC) bado haijatekelezwa.

Wakazi kama Mary Kudate wamekata tamaa.

“Mradi huu unaweza kubadilisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa huko Narok, kuongeza uzalishaji na kuweka pesa zaidi katika mifuko ya wafugaji,” alisema Bi Kudate.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA