Makala

WAKILISHA: Ajitolea kukabili janga la Ukimwi

March 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

TAFITI kadha ambazo zimefanywa katika siku za hivi majuzi kuhusu virusi vya HIV zimeonyesha kwamba idadi ya maambukizi miongoni mwa vijana imekuwa ikiongezeka.

Na mojawapo ya sababu kuu ambazo zimeonekana kuchangia hali hili ni vijana wengi kutofahamu mengi kuhusu virusi hivi.

Ni kutokana na sababu hii Kimutai Kemboi, 28, aliamua kujitwika jukumu la kuhamasisha watu kuhusu maradhi ya Ukimwi, kazi ambayo amekuwa akiifanya tangu mwaka wa 2017.

Hasa masuala anayozungumzia ni mbinu za kutumia ili kujikinga kutokana na virusi hivi ikiwa ni pamoja na kondomu, dawa za kujilinda iwapo umo katika hatari ya kuambukizwa, yaani Pre-Exposure Prophylaxes (PrEP) na dawa za kujilinda iwapo tayari umejiweka katika hatari ya maambukizi, Post-Exposure Prophylaxis (PEP).

“Azma yangu ni kuwajulisha vijana kuhusu hatari zinazowakumba, jinsi ya kujilinda kutokana na maradhi haya, cha kufanya wakijiweka kwenye hatari ya maambukizi na hatua za kuchukua wakishaambukizwa,” aeleza Kemboi.

Hasa amekuwa akitumia mitandao ya kijamii Facebook, Instagram na Twitter ambapo ameunda jukwaa linalowapa vijana fursa ya kujadiliana kuhusu maradhi haya. Hata hivyo Facebook inapendelewa zaidi ambapo ana takriban wafuasi 11,000.

“Sababu yangu ya kutumia mitandao ya kijamii ni ili kuwafikia vijana wengi sio tu hapa nchini bali pia katika sehemu zingine duniani. Pia, hapa ni rahisi kwa vijana kuzungumza kwa uwazi, suala linalofanya iwe rahisi kupata taswira kamili ya hali ilivyo,” aeleza.

Kando na mitandao ya kijamii, ameelekeza kampeni zake katika vikao vingine vinavyoleta vijana pamoja kama vile taasisi za kimasomo, makanisa na vikundi vya kijamii.

“Nimetembea na kuhutubia vijana katika taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na shule za upili za wasichana za Mary Mount Girls, Molo na Tumutumu Girls, Kaunti ya Nyeri. Aidha, nimehudhuria makongamano kadha ya vijana katika kaunti za Machakos na Makueni,” aeleza.

Kadhalika anawaunganisha wahusika na mashirika ili kupokea usaidizi wanapohisi kwamba masuala yanayoangaziwa ni magumu kuelewa.

Na tayari shughuli hizi zinazidi kuvuna matunda ambapo amekuwa akipokea pongezi kutoka kwa baadhi ya vijana walionufaika na ushauri wake.

Ari kaitoa wapi?

Msukumo wake ulitokana na kwamba akiwa shuleni, masuala kuhusu HIV hayakuzungumziwa sana.

“Niligundua kwamba kulikuwa na fikra potovu kuhusu maradhi haya, suala lililokuwa likiweka vijana hatarini,” aeleza.

Hata hivyo baada ya kufanya utafiti, anasema kwamba alipata ufahamu zaidi na hivyo akaona haja ya kuwanufaisha wenzake.

“Baada ya kutambua kwamba taarifa hizi zingewasaidia vijana, niliamua kujitwika jukumu la kuanza kuwaelimisha,” aongeza.

Kulingana naye vijana hupitia mabadiliko mengi wanavyozidi kukua, suala linalowaweka katika hatari ya kuambukizwa na hivyo wanahitaji mwongozo.

Lakini anasema kwamba haijakuwa rahisi hasa ikizingatiwa kwamba mara nyingi inamlazimu kutumia pesa zake ili kuendeleza kampeni hizi.

Licha ya kwamba hapokei malipo yoyote kutokana na jitihada zake, Bw Kemboi anasema kwamba kamwe hatalegeza kamba katika jitihada hizi.

“Kwa kusaidia vijana kuepukana na virusi hivi, najua kwamba nimeokoa kizazi na kwangu hilo ni zaidi ya pesa,” aeleza.

Kwa sasa anatumai kuangamiza unyanyapaa dhidi ya wale ambao tayari wamembukizwa na kuendeleza kampeni hizi katika sehemu zingine nchini na hata ulimwenguni.