WAKILISHA: Mlezi wa vipaji vya usemaji na ulumbi
AMEJITWIKA jukumu la kukuza vipaji vya usemaji na sanaa miongoni mwa vijana, katika harakati za kuwasaidia kujua jinsi ya kuwasilisha mawazo yao mbele ya watu.
Ni kazi ambayo Bw Abraham Opondo, 26, anafanya kupitia Campde Voices, mradi alioanzisha na ambao mbali na kusaidia vijana kukuza vipaji vyao katika masuala ya mijadala, unawasaidia kutambua vipaji vyao katika sanaa.
Shughuli hizi anaziendeleza kupitia vitengo vitatu: Young Debaters’ Society (debating program), Young Stars (creative arts program) na Fun Zone (mentorship program).
Kupitia vitengo hivi wao hutembelea shule mbali mbali katika kitongoji duni cha Kibra, jijini Nairobi na kaunti zingine ambapo kufikia sasa uwepo wao umehisiwa katika kaunti kumi nchini.
Nia yao kuu ni kuwapa wanafunzi mafunzo ya jinsi ya kujieleza kupitia mijadala na sanaa.
Ni mafunzo yanayowezesha vijana kusema vyema mbele ya watu.
“Naamini kuwa mtu akiwa na ujuzi wa kusema mbele ya watu, pia viwango vyake vya kujithamini vinaongezeka,” aeleza.
Mbali na kuwakuza kimawazo, mafunzo haya yanasaidia vijana kuwa na ujuzi wa kuafikiana hasa katika masuala ya ajira.
“Hii inamaanisha kwamba wanaweza kuafikiana na waajiri wao kuhusu mazingira ya kazi na hata mishahara wanapotaka kuajiriwa,” asema.
Kulingana na Bw Opondo, pia, vijana wanaojitolea kufanya kazi nao wanaelewa majukumu ya kusaidia jamii baada ya kufanikiwa.
Ili kuendeleza shughuli hizi wameshirikiana na shule kadha wa kadha zinazowasaidia kuandaa hafla kubwa kama vile za mashindano ya mijadala.
“Kwa mfano, shule ya Alliance High School huandaa mashindano yetu ya mijadala ya muhula wa kwanza kwa jina The Bush Debates. Kwa upande mwingine shule ya upili ya wasichana ya Pangani huandaa mashindano ya mijadala ya muhula wa pili kwa jina Pangani Debates. Mashindano haya huvutia shule 20 kila moja huku wanafunzi 30 kutoka kila taasisi inayowakilishwa wakishiriki,” aeleza.
Kwa upande mwingine shule za msingi za Lavington na Toi huandaa hafla yao ya sanaa kwa watoto, ambapo wanafunzi wanapata fursa ya kuonyesha ujuzi wao na kukutana na vigezo vyao maishani.
“Hayaishii tu hapo kwani wakati wa likizo sisi huandaa mikutano na watu wenye ushawishi katika jamii ili kuwanasihi wanafunzi na hivyo kuwazuia wasijihusishe na maovu katika jamii,” aeleza.
Ili kufikia hadhara zaidi, yeye huwa na kipindi katika kituo cha redio cha kijamii cha Pamoja FM kila wiki ambapo wanafunzi wanapewa jukwaa la kujadili masuala yanayowaathiri kila siku.
Ni suala ambalo limekuwa na matokeo kwa wanafunzi kwani wao huwasiliana na takriban wanafunzi 2,000 kila mwaka kupitia vyama mbali mbali.
“Hii inamaanisha kwamba tumewasiliana na zaidi ya wanafunzi 10,000 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo kati yao, 317 wamerejea ili kutoa huduma zao kusaidia wanafunzi wengine,” aeleza.
Kutambuliwa
Pia ametambuliwa kutokana na juhudi zake hizi.
Kwa mfano, mwaka wa 2013 alishiriki katika shindano la majadiliano la the Pan-African Debating Championships lililoandaliwa eneo la Calabar, nchini Nigeria.
“Pia nimeshiriki katika mawasilisho kuhusu vijana na demokrasia, katika Africa Leadership University forum mjini Kampala, Uganda,” aeleza.
Isitoshe, 2015, alitambuliwa na Ignite the Youth Africa kwa kuwa sauti ya wasio na sauti.
Mzawa wa mtaa wa Kibra, Bw Opondo anasema kwamba ndoto hii ilianza miaka mitano iliyopita.
“Matukio ya mwaka wa 2007 yalinifungua macho baada ya kushuhudia majirani zangu wakiuana kwa sababu ya siasa,” aongeza.
Wakati huo alikuwa katika kidato cha kwanza ambapo alikumbana ana kwa ana na matatizo ambayo asema yangetatuliwa tu kwa mazungumzo.
“Ni wakati huo ambapo penzi la kutaka kuanzisha jukwaa la mazungumzo lilikolea ndani yangu,” aeleza.
Bw Opondo anasema kwamba anatamani kushuhudia vijana wa Afrika wakijihusisha zaidi katika kuangazia matatizo yao na anaamini kwamba sauti zao zinapaswa kusikika.
Kupitia juwaa hili anatumai kufikia vijana katika sehemu zingine nchini na kuwahusisha katika masuala ya umuhimu sio tu hapa nchini, bali ulimwenguni kote.