• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
WAKILISHA: Mshairi chipukizi ajongea jukwaani

WAKILISHA: Mshairi chipukizi ajongea jukwaani

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA umri wa miaka 12 pekee amejiundia jina katika nyanja ya ushairi, suala ambalo limezidi kummiminia sifa tele sio tu shuleni anakosoma bali pia mtaani anakoishi huku akiwa kigezo cha wanafunzi wenzake na nduguze.

Jina lake ni Sharline Atieno, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi ya Mowlem Super Loaf, mtaani Dandora, Nairobi na ambaye ametia makali yake katika ushairi, uanamitindo, uchezaji densi na uimbaji.

Lakini japo amebarikiwa kwa vipaji mbalimbali, mashairi ndio kampa shavu.

Kufikia sasa anajivunia kutunga mashairi manne; Pamoja na Peace, Give me a Chance, Superstar na Confidence.

Kwa kawaida mashairi yake huzungumzia masuala ya kawaida maishani ambapo kila tukio analoliona na ambalo lina umuhimu kwa jamii, humpa kichocheo cha utunzi.

“Mara nyingi nawahimiza watu katika jamii kutokufa moyo licha ya magumu wanayopitia maishani,” anasema.

Weledi wake katika utunzi wa mashairi umemng’arisha mwaka huu huku akishiriki katika mashindano mbalimbali, vile vile kuzuru maeneo tofauti.

Bidii na ujuzi wake katika utunzi vilimfanya kumaliza katika nafasi ya pili katika kiwango cha kwanza na wa nne katika katika kiwango cha pili cha tamasha ya kitaifa ya drama mwaka huu.

Ustadi wake katika mashairi umemvunia heshima na umaarufu kochokocho kiasi cha kumhifadhia nafasi kama kiranja wa ushairi shuleni mwake. “Nilipewa wadhifa huo mwaka wa 2016, wakati huo nikiwa katika darasa la nne pekee. Katika nafasi hii, jukumu langu ni kufunza wanafunzi wenzangu jinsi ya kutunga n kukariri mashairi,” asema.

Pia, ametambuliwa na shoo za vipaji za ushairi na densi. Amefanya shoo katika mashindano mbalimbali kama vile East Africa’s Got Talent, Kenya National Archives, Kisumu na katika ukumbi wa Liberty Hall katika mtaa wa Pangani, Nairobi.

Aidha, ushairi umempa fursa ya kukutana na kuingiliana na watu kutoka ngazi tofauti maishani, bali na kumsaidia kusafiri katika sehemu mbalimbali.

“Nimepata fursa ya kusafiri katika sehemu tofauti ikiwa ni pamoja na Kisumu na Nakuru kwa sababu ya utunzi wa mashairi,” aeleza.

Agundua kipaji

Kama watu wengi waliobobea katika nyanja tofauti, Atieno aligundua kipaji chake cha ushairi akiwa na umri mdogo sana, huku wepesi wake wa kujifunza na kukumbuka mambo haraka ukichangia kasi yake ya kufanya vyema katika utunzi.

Kwa upande mwingine alianza kucheza densi akiwa darasa la nne, kipaji kilichoendelezwa alipojiunga na mafunzo ya ziada katika utunzi wa mashairi.

Ili kusawazisha kati ya masomo na utunzi wa mashairi, ametengewa muda shuleni wa kumwezesha kufanya majaribio ya kukariri mashairi yake. Aidha baada ya shule, jioni hufanya mazoezi ya densi pamoja na marafiki zake.

Kwa sasa ndoto yake ni kufanya maonyesho katika thieta mbalimbali ulimwenguni kote na kugusa nyoyo za watu kupitia ushairi.

“Ningependa kuwa kishawishi cha vijana na hata watoto wenzangu katika utunzi wa mashairi, hasa ikizingatiwa tasnia hii haijapewa uzito kama inavyostahili,” asema.

You can share this post!

Tumetoka mbali pamoja, Ruto amkumbusha Uhuru

MAPOZI: Nviiri

adminleo