Makala

Walemavu, kina mama, vijana waomba kuhusishwa katika Kongamano la COP29 Baku, Azerbaijan

Na WINNIE ONYANDO October 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HUKU ulimwengu ukijiandaa kwa kongamano la 29 la Mabadiliko ya tabianchi la Umoja wa Mataifa, maarufu kama COP29, Baku, Azerbaijan, Novemba 2024, mashirika mbalimbali yametoa wito kwa serikali kujumuisha vijana, akina mama na watu wanaoishi na ulemavu katika mazungumzo hayo.

Mwaka wa 2023, Rais William Ruto na viongozi kadhaa walihudhuria kongamano la mabadiliko ya tabianchi la COP28 na fedha zikatolewa na sera kadhaa kuundwa.

Hata hivyo, haijulikani ikiwa mwaka huu, serikali ya Kenya Kwanza itawapa nafasi vijana, akina mama na watu wanaoishi na ulemavu kuhudhuria mkutano huo.

Kando na hayo, swali linalozuka ni kama vijana wa Kenya, wanawake, na watu wenye ulemavu wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mijadala hii ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Je, sauti za makundi haya zimejumuishwa ipasavyo katika mazungumzo muhimu yanayoathiri mustakabali wao?

Shirika la Young Women’s Christian Association (YWCA) Kenya sasa inatoa wito kwa serikali kujumuisha na kuhusisha makundi hayo katika mazungumzo ya mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano wa kabla ya COP29 unaojumuisha akina mama na watu kutoka jamii mbalimbali. Picha|Winnie Onyando

Tangu kuzinduliwa kwake, shirika hilo limejenga msingi imara katika kusaidia wanawake, vijana, na makundi mengine yaliyotengwa ili sauti zao zisikike.

Katika mradi wake wa “Voices for Just Climate Action,” YWCA Kenya limeonyesha dhamira kubwa ya kuhakikisha kuwa vijana, wanawake, na watu wanaoishi na ulemavu wanajumuishwa katika mazungumzo ya baada ya Mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Kupitia juhudi hizi, imeonekana kwamba makundi haya yana mchango muhimu katika mchakato wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, ingawa mara nyingi sauti zao zimepuuzwa.

Kando na hayo, YWCA Kenya imekuwa ikifanya kazi na makundi haya kwa kujenga uwezo wao kupitia warsha za mtandaoni na mikutano ya hadhara.

Kupitia juhudi hizi, vijana, wanawake, na jamii za kiasili wamepata fursa ya kujifunza kuhusu masuala kama vile fedha zinazotolewa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na masoko ya kaboni, jambo ambalo linawapa ujuzi wa kushiriki kikamilifu katika mijadala muhimu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Lakini je, haya yanatosha?

Wakati juhudi za kuhusisha makundi haya zikiendelea changamoto bado zipo.

Changamoto kuu ni kwamba, licha ya vijana, wanawake, na watu wanaoishi na ulemavu kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, sauti zao hazijasikika kikamilifu.

YWCA Kenya, kwa mfano, imefanikiwa kusukuma mbele ajenda za sera za mabadiliko ya hali ya hewa kupitia ushiriki wao katika mijadala ya COP28 iliyofanyika Sharm El-Sheikh, Misri, lakini bado kuna pengo kubwa la uwakilishi.

Mkutano wa COP29 unatoa fursa nyingine ya kipekee kwa serikali kuonyesha uongozi wake katika kujumuisha makundi yote katika mazungumzo ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Ingawa hatua zimepigwa, hasa kupitia juhudi za YWCA Kenya na mashirika mengine, kuna haja kubwa ya kuhakikisha kuwa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu wanapata nafasi sawa na yenye maana katika mazungumzo haya.

Kenya ina uwezo wa kuwa mfano wa kuigwa Afrika ikiwa itawakilisha makundi haya.

Ni muhimu kuhakikisha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa sio tu ajenda ya ulimwengu bali ni suala linalojadiliwa na kutekelezwa kwa uwazi, ushirikishwaji, na usawa.