• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
WALLAH BIN WALLAH: Guru mfia lugha anayeyabeba majukumu ya asasi za serikali

WALLAH BIN WALLAH: Guru mfia lugha anayeyabeba majukumu ya asasi za serikali

Na CHRIS ADUNGO

TUNAPOVUTA taswira ya safari ya makuzi ya Kiswahili katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, hapana shaka kwamba mchango wa Guru Ustadh Wallah Bin Wallah unaonekana kuwa na taathira kubwa mno katika sera na maendeleo ya lugha hiyo ambayo kwa sasa ni kiwanda kikubwa zaidi cha maarifa, ujuzi, ajira na uvumbuzi.

Mwenge aliouwasha Wallah Bin Wallah katika ulingo wa ufundishaji, uandishi, usomi na utafiti wa Kiswahili tangu afyatue msururu wa vitabu Kiswahili Mufti, unazidi kuangaza ndani na nje ya Afrika. Kupitia mbinu ya kalamu yake, Guru Ustadh anazidi kupanda na kuotesha mbegu za mapenzi ya dhati kwa Kiswahili katika mioyo ya wengi. Si walimu, si wanafunzi, si mimi na wewe!

Baadhi ya ‘hao wengi’ ndio watakaotuzwa na WASTA Kituo cha Kiswahili Mufti katika kongamano la leo la kuadhimisha miaka minane ya Tuzo za Kumi-Kumi katika eneo la Matasia, Ngong mjini.

Mbali na kufundisha, kulea, kukuza na kueneza matumizi mufti ya Kiswahili, WASTA hutambua ukubwa na upekee wa mchango wa watetezi wa lugha hiyo.

Ari ya wapenzi wa Kiswahili kushiriki hafla ya kutolewa kwa tuzo hizo hurahisisha hata zaidi juhudi za makuzi na maenezi ya Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Afrika Mashariki.

“Huhitaji kushikwa mkono, uvutwe hadi mahali unapoelewa fika kwamba mambo mazuri hutendeka. Mambo mazuri siku zote huwavutia watu. Tuzo za WASTA ni wazi kwa yeyote anayekichapukia Kiswahili,” anasema Guru Ustadh.

Mbali na kutuzwa, wote ambao huhudhuria Kongamano la Tuzo za Kumi-Kumi huondoka kituoni WASTA wakijihisi kuzaliwa upya katika ulingo mpana wa Kiswahili. Wao husalia na alama ya kudumu milele katika kumbukumbu za maisha yao.

Masuala ibuka katika ulingo wa lugha huzungumziwa kwa kina huku msisitizo ukielekezwa pia katika kujadili nafasi ya Kiswahili katika vita vya kukabiliana na kasi ya maendeleo ya teknolojia katika mazingira mapya yenye kuchochea uvumbuzi.

Kupitia Tuzo za WASTA, washiriki hujadili mada zinazohusu mustakabali wa utaifa na urasmi wa Kiswahili huku wakipigia chapuo maendeleo ya lugha hiyo. Kongamano lenyewe huamsha upya ghera ya watumiaji wa Kiswahili katika jitihada za kuleta mapinduzi kwa utamaduni wa lugha.

Washiriki hupata motisha, msukumo, kariha na ilhamu ya kuuthamini Umoja wa Afrika Mashariki. Si ajabu kuelewa kiini cha wigo wa Tuzo za Kumi-Kumi kupanuka zaidi kila mwaka hadi kuwafikia wapenzi wa Kiswahili kutoka mataifa ya Tanzania, Zanzibar na Rwanda.

 

MAJUKUMU MAZITO

Si jambo dogo la kufanyiwa masihara wala kuchukuliwa vivi hivi tu kwa mtu mmoja (Guru Ustadh Wallah Bin Wallah) kujitokeza, bila ya kuungwa mkono na yeyote, kutumia rasilmali na fedha zake binafsi kubeba na kuyatekeleza majukumu mazito ambayo ni ya kiwango cha yale yanayostahili kuendeshwa na asasi pamoja na taasisi za serikali!

Sawa na WASTA Kituo cha Kiswahili Mufti, Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) pia husambaza habari na matokeo ya utafiti kwa kutumia machapisho mbalimbali na teknolojia ya mtandao wa kompyuta kuhusu vipengele mbalimbali vya Kiswahili na masuala yanayohusiana na lugha hiyo. CHAUKIDU huelimisha umma kuhusu umuhimu wa kujivunia, kuendeleza na kuheshimu Kiswahili.

Pia hushauri na kushinikiza serikali za nchi ambamo Kiswahili kinazungumzwa kutambua thamani iliyobebwa na maliasili hii ili kuunda sera mwafaka za kuendeleza lugha kadri ya uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya serikali na watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, kisayansi na kielimu.

Hakuna nishani iliyo bora, tuzo iliyo nzito na hisani iliyo na thamani kubwa zaidi kwa wapenzi wa Kiswahili kwa sasa kuliko maamuzi na hatua ya kimakusudi ya kuunga mkono jitihada za Guru Ustadh Wallah Bin Wallah katika kuhimiza matumizi ya Kiswahili Mufti katika shughuli zote rasmi na za kawaida.

Kuhusu kinachompa msukumo wa kuwazawidi maelfu ya wapenzi na watetezi wa Kiswahili kila mwaka, Wallah Bin Wallah anakiri kwamba moyo wa binadamu siku zote huhitaji kuhimizwa.

“Kiungo teketeke na laini zaidi ndani ya mwili wa binadamu ni moyo wake. Ajabu ni kwamba kiungo hicho kina uwezo wa kuwa kigumu hata kuliko mfupa iwapo mwanadamu hatatuzwa pamoja na bidii zake kutambuliwa. Anayetambua kipaji chako na kukuonesha namna ya kukitumia kwa manufaa yako na jamii pana inayokuzingira ndiye rafiki bora zaidi maishani,” anasema Doyen huyo wa Kiswahili.

Ikiwa Idara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), awali ikiitwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), ni miongoni mwa taasisi kongwe zaidi za lugha nchini Tanzania na Afrika Mashariki. Madhumuni yake ni kusimamia shughuli za maendeleo ya Kiswahili.

Kwa pamoja na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), TATAKI pia ni mlinzi wa usanifu wa Kiswahili nchini Tanzania. Kwa sasa, inafundisha Isimu, Fasihi na Historia ya Lugha ya Kiswahili.

Inafundisha Kiswahili kama lugha ya pili hasa kwa wageni kutoka nje ya ulimwengu wa Waswahili na kuendeleza utungaji wa kamusi mbalimbali zinazohusiana na taaluma za Kiswahili.

Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) ilianzishwa mnamo 1979 kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili ndani na nje ya Zanzibar.

Inajishughulisha na kuratibu, kuendesha mafunzo ya Kiswahili visiwani Zanzibar, kuhariri miswada mbalimbali ili kuthibitisha ufasaha wa Kiswahili na kufanya tafiti za Kiswahili katika Sarufi na Fasihi. TAKILUKI inatoa ushauri wa kitaaluma kwa watunzi wa vitabu ili waweze kuandika kazi zenye ubora, na kushirikiana na wadau wengine wa Kiswahili kuandaa na kuendesha semina, warsha na kozi fupi za Kiswahili.

CHAUKIDU kilicho na makao makuu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Amerika huwaleta pamoja wakuzaji wa Kiswahili duniani kote kwa nia ya kuchochea kasi ya malengo mahususi kama vile kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambapo lugha hii inatumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote; mathalan uandishi na utangazaji wa habari, uandishi na uchapishaji wa vitabu na majarida pamoja na utayarishaji wa safari za mafunzo katika Afrika Mashariki na Kati.

You can share this post!

Mganga wa Kangundo ndani kwa wizi wa magari

KAULI YA WALIBORA: Wahariri wana nafasi aali ya kuinua...

adminleo