Makala

WAMALWA: Taifa lisilowekeza kwa utafiti haliwezi kukabili changamoto zake

November 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA STEPHEN WAMALWA

ALIYEKUWA Rais wa Afrika Kusini hayati  Nelson Mandela, aliwahi kusema kuwa “Elimu ni silaha au nyenzo muhimu sana inayoweza kutumika kuubadilisha ulimwengu.”

Huenda usemi huu ungepata mashiko katika taifa letu la Kenya ikiwa tungeutafakari na kufahamu uzito wake. Labda tungechukua hatua za dharura kuitekeleza hekima hii japo haikuwa kauli ya moja kwa moja kwa taifa letu.

Ninaamini kuwa utekelezaji wa usemi huu ungetuwezesha kujiuliza ni kwa namna gani nchi ingefaidi usomi wa wasomi wengi limbukeni, yaani wale ambao ndiyo kwanza wanaanza kuutumikiza ujuzi wao baada ya kuhitimu masomo yao vyuoni.

Huenda tungelitatua matatizo ya kisiasa, ya kiuchumi, ya kiafya, ya kijamii, ya kiutawala na mengi mengineyo yanayotishia kulibwaga taifa letu katika lindi la umaskini.

Yamkini baadhi ya vyuo visingelifunga idara na taasisi muhimu zinazofanya utafiti ili kushughulikia masuala yenye uzito katika jamii vikidai kuwa havina fedha za kuendesha shughuli za idara na taasisi hizi.

Huenda tusingelikutana na wasomi waliohitimu kuwa wahandisi wakiwa katika mapokezi ya mikahawa kuwapokea wageni.

Nina maana kuwa, hatungekuwa na wasomi ambao wanaazimia kujishughulisha na kazi yoyote tu hata kama hawakuisomea ili kuendeleza maisha. Wengine wanasema ni “kujishikilia tu tukingoja kuona itakuwaje.”

Ndiyo hali halisi tuliyo nayo nchini. Ndio ukweli mchungu unaoweza kuwauma baadhi ya wadau wakiusoma kwenye majukwaa kama haya.

Ni vyema tufahamu kuwa lengo kuu kwa taifa lolote kuwaelimisha wananchi wake huwa ni kutaka kuondoa ujinga na kuwasaidia wananchi hao kutatua changamoto zao katika maisha yao ya kila siku.  Ikiwa hili halifanyiki basi huenda tunakosea.

Tunahitaji kuikabili hali hii na kuanza kuona faida ya kuekeza katika utafiti wa kitaaluma. Baadhi ya nchi zilizoendelea sasa ziliwahi kuwa nchi maskini sana na zilitegemea misaada ya nchi zingine kufanikisha hali ya maisha ya watu wake.

Hata hivyo, baada ya nchi hizi kufanya maazimio ya kufadhili utafiti wa kitaaluma katika nyanja mbalimbali za maisha, hatimaye zilianza kubadili taswira ya nchi zao na sasa leo zinapigiwa mifano ya maendeleo ya kiuchumi. 

Nina uhakika kuwa watu wengi hawatafariki kutokana na magonjwa ikiwa utafiti utafanywa kujua chanzo cha magonjwa hayo. Wakulima watavuna kwa wingi ikiwa utafiti utafanywa kufahamu mbinu mwafaka za kutumikiza ujuzi wao mashambani.

Utafiti! Utafiti! Utafiti! Ndiyo hazina pekee kwa taifa kuweza kujua vyanzo vya matatizo yake na kufahamu namna ya kuyakabili matatizo hayo.

Mwandishi ni mhadhiri wa Lugha ya Kiswahili na Fasihi ya Kiafrika, Chuo Kikuu cha Mafunzo ya Kigeni cha Tianjin, Uchina.

[email protected]