Wanafunzi wanaotaka kujiunga na CBC kufanya mtihani Juni
BARAZA la Kitaifa la Mtihani Kenya (Knec) mwezi ujao litatoa mtihani wa ustadi kwa wanafunzi wanaotaka kujiunga na mtaala mpya wa Umilisi na Utendaji (CBC) ili kupima uwezo wao wa kufanya Mtihani wa Kenya Junior Secondary Education Assessement (KJSEA).
Afisa mkuu mtendaji wa Knec, Dkt David Njengere alisema mtihani huo utafanywa mtandaoni.
Mtihani huo unalenga watoto waliotoka nchi za kigeni au wale ambao wanasoma chini ya mifumo mingine ya elimu.
‘Hii inalenga watoto waliotoka nchi za kigeni na ambao wanataka kufanya mtalaa wa CBC. Tofauti na kasumba kwamba elimu inayozingatia ujuzi na uwezo sio maarufu, tuna watoto wengi sana kutoka nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Australia, Canada, Amerika wanaotaka kujiunga na mfumo huo wa CBC,’ alisema Dkt Njengere.
Kwa mujibu wa ratiba na maelekezo ya mtihani wa mchujo wa 2025, watahiniwa watapewa somo la hisabati, Kiingereza, sayansi jumuishi na Kiswahili.
Watahiniwa wote waliolengwa waliosajiliwa lazima waripoti katika vituo vyao vilivyoteuliwa mnamo Juni 9, 2025, kwa maelekezo ya majaribio ya mtandaoni kabla ya mtihani halisi.
Dkt Njengere alisema watahiniwa hao watapewa matokeo na hati za matokeo mara baada ya kumaliza mtihani. Hizi zitatiwa saini ipasavyo na wakurugenzi wa elimu wa kaunti ndogo (SCDE) kwa madhumuni ya usajili wa KJSEA.
Majaribio yatawekewa muda na hakuna muda wa ziada utakaoruhusiwa. Muda anaochukua mtahiniwa kusoma maswali utakuwa sehemu ya muda uliopangwa isipokuwa pale ambapo maelekezo maalum yanaonyesha vinginevyo.