Makala

Wananchi watakiwa kutoa maoni kuhusu kutambuliwa kisheria kwa wazee wa kijiji

Na STEVE OTIENO April 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI inaunda sera ya kuwapa wazee wa kijiji mamlaka za kisheria katika utawala wa kitaifa.

Kwa miaka miwili iliyopita, serikali imekuwa ikifikiria kukweza majukumu ya viongozi hawa wa mashinani kwa kuandaa Mswada wa Sera ya Serikali ya Kitaifa kuhusu Utawala Vijijini.

Wakenya wana nafasi ya kutoa maoni yao kuanzia Aprili 15, 2025 waamue iwapo umefika wakati wa wazee hawa kupewa majukumu rasmi, mamlaka na mishahara.

Viongozi hawa wa kijamii wamekuwa wakitatua mizozo, kukusanya wakazi kwa ajili ya mikutano, kukusanya takwimu na kutoa taarifa muhimu kuhusu hali ya usalama kwa mashirika ya serikali.

Majukwaa ya kupokea maoni ya umma yamepangwa katika maeneo kumi kote nchini kuwezesha shughuli ya wananchi kushiriki mjadala huu.

Jijini Nairobi, mikutano itaandaliwa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Pangani kushughulikia wakazi wa Nairobi, Kajiado na Kiambu.

Wakazi wa kaunti za Uasin Gishu, Nandi, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia, Turkana na Baringo watakusanyika ukumbini Uasin Gishu Multi-Purpose Hall.

Ukumbi wa Rift Valley Plenary Hall katika ofisi ya Kamishna wa Nakuru, utakuwa mwenyeji wa wakazi wa Nakuru, Bomet, Narok na Kericho.

Katika eneo la Magharibi, Ukumbi wa Mama Grace Anyango ulioko Kisumu utahudumia kaunti za Kisumu, Homa Bay, Migori, Siaya, Kisii na Nyamira.

Ukumbi wa Magharibi, Kakamega, utahudumia wakazi kutoka Bungoma, Busia na Vihiga.

Katika eneo la Kati, Kituo cha Utamaduni cha Nyeri kitaandaa kongamano la wakaazi kutoka Murang’a, Nyandarua, Laikipia, Kirinyaga na Samburu.

Huko Mashariki, Kituo cha Meru Technical Centre kitawezesha ushiriki kutoka Tharaka Nithi, Embu, Isiolo na Marsabit.

Katika eneo la Kaskazini Mashariki, jumba la Government Guest House, Garissa, litahudumia kaunti za Garissa, Wajir na Mandera.

Ukumbi wa Le Technish Kilimambogo ulioko Machakos utawakaribisha wakazi kutoka Kitui na Makueni.

Huko Pwani, Ukumbi wa Kijamii wa Tononoka jijini Mombasa utakuwa mwenyeji wa kongamano la wananchi kutoka Mombasa, Kwale, Kilifi, Lamu, Taita Taveta na Tana River.

Kwa muda mrefu wazee wa mtaa wamekuwa kimbilio kwa matatizo yanayokumba jamii na kuwa kiungo muhimu kati ya wakazi na mamlaka za serikali.

Licha ya umuhimu wao, wamekuwa wakifanya kazi bila kutambuliwa rasmi na malipo.

Mswada wa sera unanuia kuunda mfumo thabiti wa uongozi vijijini ukipendekeza ramani rasmi ya vijiji na vigezo vya wanaofaa kuwa wazee wa kijiji.

Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen amesifu mswada huu akiutaja kuwa wa mageuzi katika uafikiaji wa malengo ya ugatuzi.

“Utaimarisha utoaji huduma mashinani na kukuza ujumuishaji, umoja, na maendeleo endelevu,” akasema Bw Murkomen.