Wanaoishi karibu na Uhuru na Moi walia kukosa maji kwa miaka 10
RICHARD MAOSI NA KEVIN ROTICH
Eneo la Mangu linalopatikana katika kaunti ndogo ya Rongai, Nakuru linazungukwa na makazi ya rais wa zamani Mzee Daniel Moi na rais wa sasa Bw Uhuru Kenyatta.
Licha ya Mangu kuwa miongoni mwa maeneo ya kutajika, kutokana na uwepo wa viongozi hawa, maisha ni magumu. Tatizo la ukosefu wa maji limewalemaza kwa zaidi ya miaka 10.
Bi Hellen Njeri, mkazi wa Rongai, anasema maisha katika eneo la Rongai ni sawa na kuishi jehanamu kwani hali ya ukosefu wa maji imesababisha ukame.
“Kila mara tunalazimika kununua maji kutoka kwenye maboma ya watu wanaomiliki visima ingawa maji hayo yamekolea chumvi kupita kiasi,” Bi Njeri akasema.
Anasema lita 20 za maji huuzwa kwa Sh15, na bei yenyewe ni ghali kwa sababu wakazi wengi ni wa kipato cha chini kutokana na shughuli wanazotekeleza kujikimu.
“Ninalazimika kununua zaidi ya lita 100 ya maji kila siku, lakini kiwango hiki bado ni kidogo sana,” aliongezea.
Anasema kuwa sio hakika kuwa wamiliki wa visima wataruhusu watu kuteka maji kutoka kwenye visima vyao, kwani baadhi yao huwanyima ruhusa ya kupata maji.
“Msimu wa kiangazi ndio matatizo huongezeka maradufu ndio maana wengi wetu hulazimika kusafiri masafa marefu kutafuta maji ambayo bei huwa juu,” aliongezea.
Lakini kufikia sasa msimu wa mvua umewapatia afueni wakazi wa Rongai angalau kupata maji ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
“Isitoshe tumekuwa tukiwasilisha malalamishi yetu kupitia ofisi ya mbunge wetu lakini hajaanzisha miradi yoyote ya kutusaidia,” akasema.
Bi Alice Kuria, mchuuzi wa mboga na matunda katika soko la Rongai anasema ni muda mrefu tangu ashuhudie maji yakichiriza kutoka kwenye mfereji wake uliokauka kitambo.
“Sina njia nyingine isipokuwa kununua maji kutoka kwa wachuuzi ingawa sio salama kwa matumizi ya binadamu,” Bi Kuria alisema.
Anasema anatumia hela nyingi kununua maji kila siku licha ya kuwa na miradi mingine ya kutekeleza kama kuwalipia watoto wake karo.
Hatua chache kutoka kwenye soko la Rongai Taifa Leo ilikutana na mzee Moses Njenga, mkulima anayekuza mahindi na kufuga ng’ombe.
Bw Njenga anasema amekuwa akipata matatizo ya kupata maji ya kuwanywesha mifugo wake.
“Mifugo kama ng’ombe wanahitaji maji mengi kila siku kinyume na binadamu ambao wanaweza kumaliza siku nzima bila kukata kiu,” alisema.
Alieleza kuwa kabla ya Rais mstaafu Daniel Moi kuondoka ofisini, wakazi walikuwa wakipata maji ya kutosha lakini mambo yalibadilika 2002.
“Tunasikia tu wakulima wa maua wamekuwa wakipewa kipaumbele, lakini pia sisi tunastahili kupewa nafasi sawa nao,” alisema.
Eliud Kimani, mwenyekiti wa miradi ya maji katika eneo la Mangu anasema tangu ahamie Rongai 1980, swala la ukosefu wa maji halikuwahi kushuhudiwa.
Anawalaumu matajiri wanaotumia hongo kubadilisha mikondo ya maji, hadi ielekee kwenye mashamba na maboma yao bila kujali maslahi ya maskini ambao ni wengi.
“Kabla ya 2002 tulikuwa tukipata maji siku saba kwa wiki lakini mambo yalibadilika pindi idadi ya watu ilipoanza kuongezeka,”Kimani alifichulia Taifa Leo.
Anasema kufikia sasa maeneo yanayopata maji yamegawika katika sehemu tatu ambazo ni Kayava,Sigei,na Sobea.
“Tangu rais Moi astaafu siku za kuwapatia wakazi maji zilipunguzwa kutoka siku saba kwa wiki hadi siku tatu,”Kimani alisema.
Anasema kuwa majuzi wakati wa mazishi ya Kabage maji yalifunguliwa kwa siku nzima lakini ,pindi mazishi yalipokatika maji yalifungwa na wakazi kurejelea ugumu waliokuwa wamezoea.
Anaeleza kuwa kampuni ya maji NARUWASCO katika eneo la Rongai ilikuwa imefungwa, wala haikuwa katika nafasi ya kuwasaidia wakazi kutatua matatizo ya maji.
“Nimelazimika kupunguza idadi ya ng’ombe wangu kutoka 20 hadi 10 kwa sababu sikuwa na maji ya kutosha kuwahudumia,”akasema.
Alipozuru Nakuru Rural Water and Sanitation Limited NARUWASCO hakupata usaidizi kwani wasimamizi walimhepa.
“Kila mara ninapozuru ofisi za maji huwa ninaelezwa kuwa meneja yuko mkutanoni,jambo linalonifanya nisubiri hadi nianpochoka na baadae kuondoka,”akasema.
Hali ni mbaya zaidi katika kituo cha polisi cha Rongai ambapo hakuna mfereji wowote unaotiririka maji.
OCPD wa Rongai Richard Rotich anasema waliacha kutegemea maji ya NARUWASCO, na wao hulazimika kununua maji kutoka kwa wachuuzi na wakati mwingine kutegemea mvua.
Alieleza Taifa Leo kuwa kituo cha polisi cha Rongai kinabeba zaidi ya nyumba 69 ambazo ni makao ya GSU,polisi wa kawaida na wale wa trafiki.
“Nilipopata uhamisho hapa nilikuta polisi wakihangaika kutokana na tatizo la maji na ikabidi nibuni mbinu mbadala ya kuhakikisha kuwa wanapata maji,” Rotich alisema.
Mkurugenzi wa NARUWASCO Reuben Korir alisema watu wamekuwa wakipata mgao wa maji kila siku ya Jumanne,Alhamisi na Jumamosi kutegemea na eneo.
“Mikondo mingine hupata maji mara tatu kwa wiki ilhali mingine ikilazimika kupata mgao mara moja kwa wiki,”aliongezea.
Mnamo 2017 rais Uhuru aliamuru maji kutoka bwawa la Chemususu kutumika baada ya mradi huo kukamilika.
Pigo jingine kubwa lililopiga kaunti ya Nakuru ni pale mradi wa bwawa la Itare,lilipokwama kutokana na ufujaji wa Sh38 bilioni.
National Water Master Plan ya serikali ya Jubilee ndiyo iliasisi miradi hii ambayo bado haijaanza kuwafaidi wakazi wa Nakuru.
Bwawa lenyewe ambalo lina kina kirefu linatarajia kuwasaidia wakulima kunyunyizia mimea katika maeneo ya Mogotio,Rongai,Eldama Ravine na Emining.