Wanasayansi wagundua molekuli inayosaidia mimea kuhimili baridi kali
WATAFITI na wanasayansi kutoka Korea Kusini wamegundua molekuli inayowezesha mimea kuhimili baridi kali, hatua inayoashiria kuendelea kupata suluhu katika sekta ya kilimo haswa kipindi hiki imelemewa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Barani Afrika, hususan Kenya, mojawapo ya mataifa kwenye Upembe wa Bara iliyoathirika zaidi na tabianchi, ubunifu huo wa molekuli huenda ukawapa wakulima afueni.
Kenya, kilimo ndio uti wa mgongo wa nchi na nguzo muhimu ya pato la taifa (GDP).

Kikosi kutoka Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Chonnam (CNU), Korea Kusini, kimegundua jinsi joto la kiwango cha chini linavyochochea jenetiki fiche kwa mimea “switch” na kubadilisha ukuaji, hasa kwenye mizizi, na kuwezesha miche kuzoea haraka ugandaji.
Matokeo ya utafiti wa wanasayansi hao yanaonyesha kuwa kupitia molekuli iliyovumbuliwa, msongo wa baridi haupunguzi tu ukuaji wa mimea, bali pia hupanga upya mifumo ya homoni ili kusaidia ustahimilivu.

Utafiti huo ulioongozwa na Profesa Jungmook Kim wa kitengo cha Bioenergy Science and Technology CNU, unaonyesha kuwa mimea kukumbwa na baridi husababisha kuharibika haraka kwa protini za auxin/indole acetic acid (Aux/IAA). Protini hizi kwa kawaida huzuia jenetiki zinazohusika na ukuaji.
Zinapoharibika kupitia msongo wa baridi, huachilia vidhibiti viwili muhimu—Auxin Response Factors ARF7 na ARF19—ambavyo huamsha jenetiki kuu ijulikanayo kama Cytokinin Response Factor 3 (CRF3).

Uanzishaji wa CRF3 hubadilisha muundo wa mizizi, kusaidia mimea kudumisha ukuaji na kuishi kwenye udongo wenye baridi.
“Kupitia molekuli tuliyogundua msongo wa baridi haupunguzi tu ukuaji wa mimea, bali hupanga upya homoni ili kufanikisha ukuaji wa mizizi,” anasema Prof Kim.
Utafiti wa Chuo Kikuu cha Chonnam, pia, unaonyesha kuwa baridi huchochea cytokinin, na kusababisha uanzishaji wa jenetiki nyingine, CRF2.

CRF2 hufanya kazi pamoja na CRF3 kusawazisha uundaji wa mizizi midogo wakati wa msongo wa baridi.
Kwa pamoja, jenetiki hizo husaidia mimea kuhimili mikumbo ya kiwango cha joto na baridi.
“Mimea inafanikiwa kwa sababu inaweza kusawazisha msongo wa nje na programu za ndani za ukuaji wake,” anaelezea Prof Kim.
“Molekuli – switch tuliyovumbua, inasaidia mimea kunawiri haswa siku za kwanza-kwanza inapochipuka licha ya uwepo wa mikumbo ya baridi,” anaongeza mtafiti huyo.

Mizizi huwa kwenye hatari kubwa haswa nyakati za awali za ukuaji, na kushindwa kuhimili baridi kunaweza kusababisha upungufu wa virutubisho, kudumaa na hivyo kusababisha mimea kutoa mazao kiduchu.
Utafiti huo ulifanywa na Prof Kim pamoja na wanasayansi Uyen Thu Nguyen, Na Young Kang na Dkt Dong Wook Lee, wote kutoka CNU.
Aidha, matokeo yalitangazwa rasmi kwa mara ya kwanza Septemba mwaka huu, 2025.
