WANDERI: Afrika itahadhari kuhusu nia halisi ya Urusi
Na WANDERI KAMAU
BAADA ya Rais Uhuru Kenyatta kujiunga na viongozi wengine wa Afrika majuma mawili yaliyopita nchini Urusi kwa kongamano maalum la Urusi na nchi za Afrika, maswali yameibuka kuhusu lengo kuu la Urusi barani humu.
Hilo linatokana na hali kuwa badala ya kongamano hilo kuangazia mikataba ya kiuchumi, lilijikita sana katika kuwaonyesha viongozi hao silaha za kisasa za kivita.Viongozi hao zaidi ya 40 walitembezwa katika vituo mbalimbali ambako walionyeshwa miundo ya kisasa ya bunduki, makombora, ndege, vifaru, mizinga kati ya zingine.
Hicho kilionekana kuwafurahisha sana baadhi yao na baadhi wakapigwa picha wakionyesha weledi wao katika matumizi ya silaha hizo.
La kushtua ni kuwa, ingawa ajenda kuu ya kongamano hilo ilikuwa kuangazia changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazokumba Afrika, suala la mauzo ya silaha barani humu ndilo lililojitokeza sana.
Kwanza, ni muhimu kufahamu kwamba Urusi na mataifa yenye uwezo kama Amerika na Uchina yanashindana kuidhibiti dunia kiuchumi na kisiasa.Katika historia, hii si mara ya kwanza kwa Amerika na Urusi kujikuta katika ushindani huo, kwani hali hiyo ndiyo iliyokuwepo wakati wa Vita Baridi vya Dunia kati ya 1947 na 1990.
Wakati huo, Amerika ilitumia uwezo wake wa kijeshi kuvamia maeneo mbalimbali ambayo Urusi, wakati huo ikiwa Muungano wa Mataifa ya Usovieti (USSR) iliyadhibiti duniani ili kupunguza ushawishi wake.Mbinu hiyo ndiyo iliifanya muungano huo wa USSR kuvunjika, hivyo kuifanya Urusi kuwa nchi moja.
Tangu 1990, Amerika imekuwa ndiyo nchi yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi na kijeshi duniani, ambapo imekuwa ikitumia ushawishi wake kubuni mwelekeo wa kisiasa ambayo dunia itachukua.Na licha ya kutoshiriki kwenye vita hivyo, Afrika ilijipata kama mwathiriwa wa mzozo kati ya Amerika na Urusi.
Mojawapo ya nchi iliyojipata mateka wa mzozo huo ni Angola, ambapo Urusi ilidaiwa kuwafadhili wapiganaji wa chama cha UNITA kilichoongozwa na marehemu Jonas Savimbi dhidi ya serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Jose Eduardo dos Santos.
Mapigano hayo yalisababisha maelfu ya raia wasio hatia kuuawa, huku Urusi ikikana kumfadhili Bw Savimbi kwa kuwapa wapiganaji hao silaha.Kimsingi, kinachojitokeza ni kuwa huenda Urusi inafufua mbinu kama hiyo kuendeleza makabiliano yake na Amerika kwenye harakati za kung’ang’ania udhibiti wa maeneo mbalimbali duniani.
Ni dhahiri kuwa tangu 1990, uwezo wa kiuchumi wa Amerika na nchi za Magharibi unaendelea kupungua kutokana na kuchipuka kwa nchi kama Uchina, India na Japan ambazo zinaonekana kuwa tishio kwa Amerika na washirika wake.
Rais Kenyatta na viongozi wengine wa Afrika wanafaa kutahadhari kuhusu mikataba wanayotia saini na nchi kama Urusi. Hii ni kwa kuwa huenda wanazifanya nchi zao kuwa uwanja wa mapigano tena bila kujua kwa manufaa ya nchi kama Amerika na Urusi. Lazima Afrika itambue nia fiche ya mikataba hiyo