WANDERI: Dawa ya masaibu ya Sossion ni kujiuzulu
Na WANDERI KAMAU
MFALME Sobhuza II wa Swaziland (inayoitwa Eswatini) alitawala nchi hiyo kwa miaka 82.
Anatajwa kuwa kiongozi aliyetawala kwa muda mrefu zaidi katika historia.
Kulingana na wanahistoria, kipindi hicho kinaweza kulinganishwa tu na muda ambao baadhi ya Mapapa wa Kanisa Katoliki wamekuwa wakichukua kuliongoza kanisa hilo.
Mfalme huyo alianza kuhudumu tu baada ya kuzaliwa mnamo 1899, lakini akachukua muda kabla ya kuanza kuitawala nchi hiyo kutokana na umri wake mdogo.
Alifariki mnamo 1983. Kijumla, alitawala karibu uhai wake wote duniani. Lakini hatimaye aling’atuka –kupitia kifo.
Humu nchini, si wengi walioamini kuwa Rais Mstaafu Daniel Moi angeondoka mamlakani mnamo 2002, baada ya chama cha Kanu kushindwa vibaya na muungano wa Narc, ulioongozwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.
Vivyo hivyo, inafikia wakati ambapo mtu huondoka katika nafasi yoyote anayoshikilia ili kudumisna heshima, hata atakapoondoka.
Ninatoa ushauri huu kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) anayekumbwa na utata, Bw Wilson Sossion, kwamba huwa inafikia wakati ambapo busara kuu huwa ni kung’atuka na kuacha nafasi unayoshikilia.
Sababu kuu ni kwamba kuendelea kuwepo kwake katika chama hicho kumezua mgawanyiko mkubwa, kiasi kuwa baadhi ya wanachama wake wameanza kuhamia katika Chama cha Walimu wa Vyuo (KUPPET) wakimlaumu Bw Sossion kwa kuendesha chama kama mali yake binafsi.
Vilevile, wanasema kuwa ni vigumu kwake kukiongoza kwa njia huru, ikizingatiwa kuwa anahudumu kama mbunge maalum, aliyeteuliwa na chama cha ODM.
Tayari, Baraza Kuu la Chama (NEC) lilisema Ijumaa kuwa limepiga kura ya kumwondoa Bw Sossion katika nafasi hiyo na kumteua Bw Hesborn Otieno.
Kwa upande wake, Bw Sossion ameshikilia kwamba ataendelea kuhudumu, akidai kuwa wanachama hao hawakufuata taratibu za kisheria kumwondoa uongozini.
Anadai kuwa njia ya pekee ambapo anaweza kuondolewa mamlakani ni kupitia uamuzi wa wajumbe wote wa chama, kwenye mkutano wao mkuu ambao hufanyika kila mwisho wa mwaka.
Licha ya kujipiga kifua, Bw Sossion anapaswa kusoma ishara za nyakati na kuona kuwa kuwepo kwake katika chama hicho kunazidi kukigawanya, badala ya kukiunganisha.
Ni dhahiri kwamba yeye atabaki miongoni mwa makatibu wakuu ambao walijitolea sana kuwatetea walimu. Kwa wakati mmoja, aliwahi hata kuzuiliwa na polisi akiwaongoza walimu kwenye maandamano ya kuishinikiza serikali kuongeza mishahara na marupurupu.
Hata hivyo, huenda akaharibu sifa alizojijengea kwa kuendelea kukwamilia mamlakani, badala ya kung’atuka uongozini kwa hekima.
Ni busara kama hiyo aliyotumia Mzee Moi mnamo 2002, ambapo licha ya pendekezo lake Rais Uhuru Kenyatta kushindwa uchaguzi wa urais na Mzee Kibaki, alikubali matokeo hayo na kustaafu kwa heshima.
Kwa sasa, wanasiasa huwa wanafurika kwake wakitafuta ushauri wa kisiasa. Kwa uamuzi huo, aliwasahaulisha Wakenya dhuluma zote walizotendewa na utawala wa Kanu.
Kwa Bw Sossion, busara kuu kwa sasa ni kung’atuka kwa hiari, ili kudumisha heshima.