Makala

WANDERI: Falsafa ya Mbaya Wetu inaliponza taifa hili letu

March 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Gavana wa Kericho Paul Chepkwony aliyejitokeza kumtetea Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Bi Lily Koros. Picha/ Maktaba


Na WANDERI KAMAU

HATUA ya viongozi wa Ukanda wa Bonde la Ufa kujitokeza kumtetea Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Bi Lily Koros dhidi ya kutowajibika kwake ni ya kutamausha.

Wakiongozwa na Gavana Paul Chepkwony wa Kericho, viongozi hao wamedai kwamba makosa ambayo yamefanyika katika hospitali hiyo chini ya usimamizi wa Bi Koros ni “njama za mahasidi wake” ili kumwondoa mamlakani.

Kauli hii imeibua tena mtindo wa kawaida ambao umekuwa kama sehemu ya mtindo wetu wa kimaisha, ambapo jamii anakotoka “mkosa” hujitokeza kumtetea kwa vyovyote vile, bila kutathmini kwa kina ikiwa alikosa au la.

Ni mtindo ambao umetaasisika kote barani Afrika, hali ambayo imeathiri uwepo wa uwazi na uwajibikaji.

Katika kesi ya Bi Koros, kilichopo ni kwamba viongozi hao wanamtetea kwani anatoka katika eneo hilo, na pia ni Mkalenjin, sawa na wao.

Hii ni bila kuzingatia maovu yote ambayo yametokea katika hospitali hiyo; kutoka visa vya wizi wa watoto, madai ya kubakwa kwa kina mama waliojifungua na wahudumu wa mochari, visa vya wizi na majuzi kupasuliwa kwa mgongwa asiyefaa.

Kwa hayo yote, msimamo wa viongozi hao ni kwamba Bi Koros “kasingiziwa na mahasidi wake!”

Naam, mantiki ya haya ni kwamba hii ni hadaa ya nafsi. Ni wazi kwamba huu ni mwendelezo wa falsafa mbaya ya ‘Mbaya Wetu.’

Ni mtindo hatari, ambao umeizalia Afrika viongozi mazimwi, ambao wamegeuka kuwa balaa kuu kwa nchi zao.

Mazimwi hao huwanyonya damu wana waliowachagua, kwa kuwadhulumu na kutaasisisha udikteta katika nchi hizo.

 

Mifano

Mifano dhahiri ni viongozi kama marehemu Mobutu Seseseko (DRC Kongo), Idi Amin Dada (Uganda), Meles Zenawi, Haile Mengistu Mariam (Ethiopia), Mohamed Siad Barre (Somalia), Hastings Kamunzu Banda (Malawi), Daniel arap Moi (Kenya) kati ya wengine wengi.

Katika enzi zao, viongozi hao waliziteka nchi zao na kuzigeuza kama makazi yao. Waligeuka kutoka wanadamu hadi miungu wa kidunia, waliosifiwa na kila mmoja.

Cha kushangaza ni kwamba, licha ya dhuluma hizo zote, walibaki kuwa “mashujaa” katika jamii zao! Aidha, jamii hizo ziliwaona kama ‘wakombozi’ wakuu waliotumwa kutoka Kuzimu!

Ujinga na uzumbukuku huo nao umeigeuza Afrika kuwa kama jaa ya utumwa wa nafsi. Bara lililoonyesha dalili za ukombozi liligeuka kuwa mtumwa wa tamaduni hafidhina zisizo na umuhimu wowote.

Mfano halisi wa baadhi ya ujuha huo ni hafla ya kitamaduni ya ‘Umhlanga’ ambayo hufanyika kila mwaka nchini Swaziland, ambapo Mfalme Mswati III huwa anamchagua bibi mpya kila mwaka. Hii ni licha ya taifa hilo kuwa moja ya nchi zinazokabiliwa na kiwango cha juu sana cha maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Kwa ufahamu huo, hatuna jingine kama jamii, ila kupanua mawazo yetu, ili kujikomboa kutoka utumwa huo. Si haki, hata kidogo, kutetea makosa, hata yaliyo dhahiri.

[email protected]