Makala

WANDERI: Je, matatizo yetu ni 'laana' ya Mau Mau?

August 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

SIKU chache kabla ya kukumbana na mauti yake, marehemu babu yangu alinieleza kuhusu masikitiko makubwa aliyokuwa nayo kuhusu namna wapiganaji wa vita vya Mau Mau walivyotelekezwa na serikali.

Katika uhai wake wote, babu alijivunia sana ushujaa ambao wapiganaji hao walidhihirisha dhidi ya serikali ya Mwingereza kiasi cha kumshinda, licha ya yeye kuwa na silaha kali kama bunduki.

“Ushindi wetu ulitokana na ukakamavu na kujitolea kwetu, bali si uelewa wa mbinu za kivita,” alinieleza babu.

Naam, kauli zake zinawiana na zingine za maelfu ya mashujaa wa Mau Mau, ambao waliacha familia zao, mashamba na shughuli nyingi za kiuchumi ili kuitetea Kenya dhidi ya unyakuzi kutoka mikononi mwa wabeberu na walowezi wa Kizungu.

Hata hivyo, wengi wameeleza majuto makubwa, kwani ndoto na malengo waliyokuwa nayo wakati wa vita zimesalitiwa na kundi ndogo la “miungu Weusi.”

Kwa undani, “miungu” hao ni kundi la viongozi ambao walichukua uongozi mara tu baada ya nchi nyingi za Kiafrika kupata uhuru wake.

Kinyume na kuendeleza ndoto za wapiganaji hao, wengi waliwageuka.

Mashamba waliyopigania yalinyakuliwa. Misitu waliyotetea iligawanywa kuwafaidi “viongozi” hao na washirika wao wa karibu.

Kilichobaki ni vilio, majuto na masikitiko kwa mashujaa hao, watoto wao, vitukuu, vilembwe na vilembwekeza wao. Hawana popote pa kwenda. Wamebaki maskwota au wakimbizi wa ndani kwa ndani katika nchi zao wenyewe.

Na kabla ya kifo chake, babu alisema kuwa ni lazima “laana” ya wapiganaji hao ziandame nchi husika, kundi la watawala hao na vizazi vitakavyofuata.

Ingawa siendelezi dhana za ushirikina, kauli ya babu yangu huenda ikawa kweli. Sababu kuu ni kuwa licha ya juhudi nyingi za ‘kuistawisha nchi kiuchumi’ deni la kimataifa la Kenya linaendelea kuongezeka. Kwa sasa, deni letu limefikia Sh5.1 trilioni, huku gharama ya maisha ikizidi kupanda.

Pili, ingawa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ulizinduliwa kwa matumaini na shamrashamra kubwa, yanayoibuka ni kwamba imebadilika kuwa “laana” kwa Kenya kwani Wachina tayari wameteka shughuli zote za reli hiyo.

Tatu, licha ya juhudi za serikali kuendeleza vita dhidi ya ufisadi, kwa kubuni makumi ya tume za uchunguzi, saratani hiyo imebaki donda lisiloisha. Kenya inaporwa katika kila sekta.

Nne, mporomoko wa kimaadili unatishia mustabali wa kizazi cha sasa. Maovu kama uavyaji mimba, ukahaba, ushoga, utekaji nyara wa watu, ugaidi, dhuluma za kinyumbani kati ya mengine yamegeuka kuwa “habari za kawaida.” Vifo vimegeuka kuwa “chakula chetu cha kawaida.”

Je, tiba kuu kwa misururu ya mikosi hii ni ipi? Kwanza, lazima uongozi wa Rais Kenyatta utekeleze ahadi zote kwa wazee wa Mau Mau ili kutuliza ghadhabu walizo nazo dhidi ya uongozi wa sasa. Hii ni pamoja na kuwalipa fidia nyingi walizoahidiwa na serikali za awali.

La sivyo, ‘laana’ ya ghadhabu yao itazidi kutwandama.

[email protected]