MakalaSiasa

WANDERI: Jubilee ikome kutumia kifua dhidi ya Wakenya

September 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

UHESABU wa watu ni shughuli ambayo imekuwepo kwa miaka mingi. Ni shughuli muhimu ambayo ilichukuliwa kwa uzito na falme nyingi ambazo ziliweka msingi kwenye mfumo wa utawala duniani.

Ni kutokana na ufahamu wa watu ambapo watawala wa falme hizo waliweza kuendesha shughuli muhimu kama uajiri wa watu katika jeshi.

Katika falme kama Ugiriki na Roma, watawala wake walitumia takwimu za watu waliopata kuzigawanya katika maeneo ya kiutawala ambayo yaliwasaidia sana katika utoaji wa huduma muhimu kwao.

Sensa vile vile ni zoezi ambalo linakubalika kidini, kwani katika Ukristo, Yesu alizaliwa wakati mtawala Herode wa Israeli alikuwa ameagiza watu wote katika ufalme huo wahesabiwe.

Hivyo, zoezi hili ni muhimu sana kwa nchi ama falme yoyote ile duniani.

Hii ikiwa sensa ya sita tangu Kenya kujinyakulia uhuru kutoka kwa Waingereza mnamo 1963, kuna maswali mengi ambayo Wakenya wengi wanajiuliza licha ya kukubali kuhesabiwa.

Baadhi ya maswali hayo ni kuhusu umuhimu wake, ikizingatiwa kuwa inafanywa miezi miwili tu baada yao kuagizwa na Serikali ya Kitaifa kujisajilisha kupata Huduma Namba.

Zoezi hilo liliendeshwa kwa uzito mkubwa kiasi kwamba Rais Uhuru Kenyatta alilazimika kuongeza muda wa usajili wake kwa wiki moja ili kuwaruhusu Wakenya ambao hawakuwa wamejisajilisha kufanya hivyo.

Na licha ya kumalizika kwa mchakato huo, maswali yangalipo kuhusu umuhimu wake. Je, umuhimu wake ulikuwa upi? Maelezo ambayo Wakenya walitoa yatatumiwa vipi? Yatakuwa na manufaa yoyote kwao?

Tashwishi hizi zinachangiwa na hali kuwa hata Wakenya wanaoishi ng’ambo waliagizwa kujisalilisha, la sivyo wangekumbwa na vikwazo vingi, hasa kwenye taratibu za kuchukua upya stakabadhi kama paspoti.

Serikali ilitoa maagizo kwa mabalozi katika nchi mbalimbali kuhakikisha kuwa kila Mkenya anajiandikisha.

Ingawa zoezi hilo lilitumia jumla ya Sh8.8 bilioni, asilimia kubwa ya wananchi hawana ufahamu wowote kuhusu umuhimu na maana yake.

Hii ni kwa kuwa baadhi ya maswali ambayo wanaulizwa kwenye zoezi la sensa ni yale yale waliyoulizwa walipokuwa wakijisajilisha kwa Huduma Namba.

Hofu hizi zinapojiri wakati ufisadi umegeuka kuwa jinamizi kuu kwa utawala wa Jubilee, ni muhimu kwa asasi husika kujitokeza wazi kuwafafanulia Wakenya kuhusu uhusiano wa zoezi hizi mbili.

Baadhi ya Wakenya wenye ghadhabu wamesikika wakitishia kususia kuhesabiwa, wakilalama kwamba hawaoni mabadiliko yoyote kwa maisha yao licha yao kutoa maelezo mengi kwa Serikali.

Ni kinaya kwa Serikali kuendesha mazoezi hayo bila kuwafafanulia Wakenya umuhimu wake, ikizingatiwa pia huwa inachukua maelezo muhimu ya mtu anapojisajilisha kupata stakabadhi muhimu kama paspoti ama kitambulisho cha kitaifa. Pia mtoto anapozaliwa, anapoingia shule husajiliwa na pia kila anayekufa huandikishwa.

Imefikia wakati uongozi wa Rais Kenyatta ufahamu kuwa kuendeleza sera kimabavu kwa wananchi bila kutoa ufafanuzi kuhusu maana yake ni njia ya kuongeza hasira miongoni mwao. Utawala shirikishi unapaswa kuwachukulia raia kama washikadau, lakini sio kama maadui wachapwao kwa viboko.

[email protected]