WANDERI: Kama Sauli, Rais Kenyatta ana nafasi kukomboa Kenya
Na WANDERI KAMAU
ALIPOKUWA akielekea Dameski kutekeleza mauaji dhidi ya Wakristo, safari ya Sauli ilikatizwa ghafla na sauti kubwa iliyoandamana na mwanga mkubwa uliomfanya kupata upofu kwa muda.
Kulingana na Biblia na vitabu kadhaa vya historia, Sauli alikuwa miongoni mwa Wayahudi walioogopwa sana na Wakristo, kwani aliwaua kwa kutumia njia zote, kwa msingi wa “kufuata dini isiyofaa.”
Inaelezwa kuwa, Mungu alikasirishwa na vitendo ya Sauli na kuapa kukabiliana naye, ili kukomesha ukatili wake.
Lakini wazo la Mungu halikuwa ni kumwadhibu hasa, ila lengo lake lilikuwa ni kumgeuza kuwa mtume wake, ili kuendeleza “habari njema” katika nchi zingine.
Inaelezwa kwamba baada ya kupata upofu huo na kunyamazishwa na ngurumo hiyo ya kutisha, Sauli aligeuza nyenzo zake, na kuwa kiumbe kipya, kiitwacho Paulo.
Naam, Mtume Paulo alibadilika kutoka muuaji hadi mtetezi wa haki, ukweli na mhubiri wa Kikristo anayedhaniwa kuyafikia maeneo mengi zaidi akihubiri “habari njema” za dini hiyo.
Vivyo hivyo, kumezuka mjadala mkali miongoni mwa wakosoaji wa Rais Uhuru Kenyatta, wa ikiwa atafaulu kurejesha imani ya Wakenya kwa utawala wake kutokana na vita vinavyoendelea kuhusu ufisadi.
Katika mijadala hiyo, kuna makundi mawili; wale waliopoteza imani kabisa na uongozi wake na wale ambao wanashikilia kuwa anapaswa kupewa nafasi kudhihirisha umahsusi katika utendakazi.
Binafsi, nimo katika kundi la pili. Ninaamini kwamba Rais Kenyatta ni binadamu kama wale wengine. Tuna udhaifu wetu. Kuna kipindi ambacho huwa tunakosea.
Vivyo hivyo, ninaamini kwamba asilimia kubwa ya Wakenya hairidhishwi na mwelekeo wa nchi, hasa gharama kubwa ya maisha na msururu wa sakata za ufisadi.
Hata hivyo, hili halipaswi kutufanya kupoteza imani katika nchi yetu wenyewe. Sababu kuu ni kwamba kama mwanadamu mwenye hisi ya uhalisia wa kimaisha, huenda hatimaye amepata ufahamu kwamba hali si nzuri hata kidogo-ndipo akaanza harakati za kupambana na rushwa.
Kwa sasa, kile rais anahitaji ni uungwaji mkono wa kila Mkenya. Kama Sauli, rais ana nafasi ya kubadili hali na kuwa ‘Mtume Paulo Mpya wa Kenya.’ Kwa hayo, tutaanza upya safari yetu mpya ya kuelekea ‘Kanani’, nchi ya nyama na asali.