WANDERI KAMAU: Ufalme huenda ukarejesha siasa komavu ulimwenguni
Na WANDERI KAMAU
MKWAMO wa kisiasa ambao umejitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa urais nchini Amerika umeibua maswali kuhusu ufaafu wa mfumo wa kidemokrasia, hasa katika nchi zenye chumi za kadri.
Ingawa huenda matokeo ya uchaguzi huo yakawa yametangazwa kufikia wakati wa kuchapishwa kwa makala haya, ushindani mkali kati ya Rais Donald Trump na Bw Joe Biden umeibua mdahalo mzito duniani kuhusu mustakabali wa mfumo wa kidemokrasia.Mara tu baada ya matokeo ya uchaguzi kuanza kutangazwa Novemba 4, Rais Trump, aliyewania kwa tiketi ya chama cha Republican, alianza kudai uwepo wa njama za kumuibia kura.
Kwa upande wake, Biden, ambaye alipeperusha bendera ya chama cha Democratic, alimlaumu Trump kwa “kuwa mwoga” ilipodhihirika kulikuwa na ushindani mkali baina yao.Kwa wakati mmoja, Trump alipuuzilia mbali matokeo hayo, huku akitishia kusimamisha taratibu za kuhesabu kura.
Semi za viongozi hao wawili zilianza kujenga taharuki kali za kisiasa miongoni mwa wafuasi wao, ripoti zikisema kuwa nusura ghasia zitokee katika baadhi ya majimbo nchini humo.
Kijumla, bila kujali atakayeibuka mshindi, swali kuu linalojitokeza baada ushindani huo ni ikiwa huu ndio wakati nchi mbalimbali duniani zianze kutathmini uwezekano wa kurejelea mfumo wa serikali wa kifalme.
Ni mdahalo ambao umeibuliwa na baadhi ya wasomi wa historia, sayansi ya siasa na mifumo ya utawala, wakisema nchi ambazo bado zinaendelea kuzingatia mfumo huo huwa na uthabiti mkubwa kisiasa na kiuchumi.
Hadi sasa, baadhi ya mataifa yanayoegemea mfumo huo ni Ubelgiji, Norway, Japan, Uingereza, Saudi Arabia, Jordan kati ya mengine.Kwa utathmini wa kina, ni pendekezo ambalo huenda likaonekana kuwa la kikale, hasa katika bara Afrika, ijapokuwa lina uzito wake mkubwa.
Kwanza, nchi nyingi ambazo zimekuwa zikidai kukita siasa zake katika mfumo wa kidemokrasia zimegeuka kuwa chemichemi za ghasia za kisiasa, kila chaguzi kuu zinapokaribia ama zinapokamilika.
Kenya ni mfano mwema wa hali hiyo. Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992, imekuwa kawaida kwa saratani ya kisiasa kututeka, kutupofusha na kupumbaza tusijue mwelekeo kuihusu nchi.Viongozi hugeukiana wao kwa wao, wakitumia kila mbinu kutusiana na kuchafuliana majina ili kujizolea umaarufu mkubwa.
Imekuwa kawaida kwa nchi nyingi kuwachagua “wabaya wao” kama viongozi ‘mashujaa,’ kuwawakilisha kwenye nyadhifa mbalimbali muhimu.
Pendekezo la kurejelea mfumo wa kifalme linatokana na hali kwamba jamii nyingi za Kiafrika zilitumia mfumo huo kuendesha siasa zake. Ni mfumo ambao ulihakikisha uthabiti mkubwa wa kisiasa na kitamaduni miongoni mwazo.Kwa mfano, miongoni mwa Wamaasai, hakuna yeyote ambaye angekaidi usemi wa kiongozi wao maalum aliyeitwa ‘laibon.’
Wakikuyu walikuwa na ‘muthamaki’ huku ‘mfalme’ wa Wakalenjin akiitwa ‘orkoiyot.’Binafsi, nahisi ni wakati tukite kaida asilia za Kiafrika kwenye siasa zetu ili kurejesha uthabiti na hekima iliyokuwepo hapo awali.Kwa kufuata njia hiyo, tutajenga jamii yenye mwelekeo mmoja, sauti moja na mtazamo sawa, bila mafarakano yasiyofaa.