MakalaSiasa

WANDERI: Murathe anaharibia Rais akidhani kuwa anamjenga

August 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

KABLA ya kifo chake mnamo 2017, aliyekuwa kiongozi wa Kanisa la PCEA, Dkt John Gatu, aliandika wasifu wake ‘Fan into Flame’ ambao unarejelea maisha yake kwa upana.

Wasifu huo pia unaangazia historia ya Kenya, hasa vita vya Mau Mau, kwani wakati huo Dkt Gatu alikuwa mtu mkubwa aliyeelewa yaliyokuwa yakiendelea nchini.

Kando na simulizi za kawaida kuhusu vile wapiganaji walikuwa wakijitayarisha kuwashambulia wazungu, marehemu pia alirejelea hafla za siri za kuwalisha watu viapo kuwa ‘wazalendo’ kwa viongozi fulani wa kisiasa na jamii zao.

Ingawa wasifu unawataja bayana viongozi waliohusika kwenye shughuli hizo, kinachosikitisha ni mbinu walizotumia kulipiza kisasi dhidi ya wale ambao walikiuka ‘kanuni’ za viapo.

Kitabu kinaeleza kwamba uasi wa viapo hivyo ndio ulikuwa chanzo kikuu cha baadhi ya mauaji tata ya viongozi maarufu wa kisiasa.

Viongozi waliochukua uongozi wa nchi walitumia mbinu hizo kumtisha yeyoye ambaye angepinga vitendo vyao ama kufichua udhalimu waliofanya kwa wananchi.

Alipochukua uongozi wa nchi mnamo 1978 baada ya kifo cha Mzee Jomo Kenyatta, Daniel Moi aliendeleza mbinu hiyo kwa kusisitiza lazima kila mmoja angekuwa “mzalendo” kwa Kanu.Mzee Moi alitumia vitisho kujijenga kisiasa kiasi kwamba, yeyote ambaye angempinga kwa vyovyote vile angetajwa kama “adui wa nchi na maendeleo” na kufunguliwa mashtaka bila kufanyiwa kesi.

Cha kusikitisha ni kuwa, mwelekeo wa kisiasa nchini kwa sasa unaonekana kuturejesha katika enzi hizo.Dereva mkuu wa mwelekeo huo hatari ni Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee David Murathe.Tangu aliporejea kwenye wadhifa huo baada ya kutangaza kujiuzulu Januari 2019, Bw Murathe ameibukia kuwa kiongozi ‘anayewaadhibu’ viongozi wa chama ambao wanaonekana kukosoa ama kuwa na mawazo huru.

Ni chini ya uongozi wake ambapo baadhi ya wabunge na maseneta wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ kama Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Kithure Kindiki (Tharaka Nithi) kati ya wengine walipoteza nyadhifa zao za uongozi kwenye Seneti na Bunge la Kitaifa.

Kwa sasa, maseneta hao ndio wanaoongoza harakati za kupinga Mfumo Mpya wa Ugavi wa Mapato, unaoungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Hata hivyo, maseneta hao wameapa kufanya lolote kuhakikisha mfumo wowote wa ugavi wa mapato unazingatia usawa.Kutokana na misimamo yao kupinga mfumo huo, Bw Murathe amenukuliwa akiwaonya maseneta Murkomen na Johnson Sakaja (Nairobi) kwamba wataadhibiwa vikali na chama.

Kimsingi, ni dhahiri kuwa chama chochote kile cha kisiasa kina masharti na kanuni zake ambazo lazima zizingatiwe na wanachama wake.

Nidhamu ya chama ndiyo imeviwezesha vyama kama Chama cha Mapinduzi (Tanzania), African National Congress (ANC, Afrika Kusini) kati ya vingine kuiendelea kuwa bora.

Hata hivyo, matumizi ya vitisho ni sawa na kuirejesha nchi katika enzi ya chama kimoja. Busara itakuwa ni kufanya mashauriano kwa manufaa ya nchi.

[email protected]